Habari za leo ndugu msomaji wa SONGA MBELE BLOG ni imani ya yangu unaendelea vyema katika safari ya kuelekea mafanikio. Hongera sana na karibu katika mada ya leo.
Yawezekana unaona hauna, bahati. Yawezekana ukafikiri labda umelogwa.
Katika safari ya mafanikio kuna mambo mengi sana utakutana nayo. Hakuna njia nyoofu katika kuelekea mafanikio. Na kama hii njia ingekuwepo basi watu wangepigana sana na pengine hadi kuumizana, kwa sababu kila mtu angetaka awe wa kwanza kuifuata hiyo njia. Hivyo mvutano ungekuwa mkubwa sana.
Katika safari ya mafanikio utakutana na vikwazo vingi lakini haupaswi kuacha kufanya kile ambacho tu apaswa kufanya.
Leo naomba nitoe mfano wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa). Wakati anatetea uhuru wa Watanzania alikutana na vikwazo vingi sana. Moja ya vikwazo alivyokutana navyo ni pale walipomwambia achague au aendelee na siasa au aendelee na ualimu. Mwalimu alichagua kuendelea na siasa, akapambana mpaka taifa letu likapata uhuru.
Kitendo cha mwalimu kuachishwa ualimu tayari mlango ulifungwa, badala yake sasa hakukaa na kuanza kuhuzunika kwa sababu ya kuukosa ualimu uliokuwa unamuingizia kipato, bali aliendelea kupambana kuikomboa Tanzania japo hakukuwa na maslahi katika siasa. Leo hii tunaufurahia uhuru kwa sababu ya mlango mmoja wa mtu uliofungwa kipindi kile, lakini akifahamu kwamba upo mingine saba akaitumia hiyo.
Je wewe umekata tamaa? Labda wewe ni mwanafunzi uliyehitimu kidato cha sita mwaka huu na haujashinda mtihani au hujapata vigezo vya kwenda chuo, usikate tamaa. Habari njema ni kwamba ipo milango mingine saba. Je,wewe ni mfanyakazi na umepoteza kazi, usikate tamaa. Habari njema ni kwamba ipo milango mingine saba. Je, wewe umepata ajari ya bodaboda au gari na kuvunjika mguu au mkono? Usikate tamaa. Habari njema ni kwamba ipo milango mingine saba.
Katika hali yoyote ile uliyonayo haupaswi kukata tamaa na kuona sasa dunia imefika mwisho. Unaweza kufanya mambo haya matatu kuutafuta mlango mwingine.
- Kwanza kabisa tambua tatizo.Je tatizo lako ni lipi? Je tatizo lako ni la mda mfupi au ni la mda mrefu?
- Pili weka mpango. sasa anza kuweka mpango ambao utautekeleza. Weka malengo yako na yagawe katika malengo madogo madogo. Anza kuutekeleza mara moja
- Mwisho utekeleze mpango. Ni muhimu sana kuutekeleza mpango wako bila kujali watu watasemaje, usiogope kwa kusema watanionaje, anza sasa kuutekeleza.