Ni muhimu sana kujifunza mbinu za kuweka usawa mapato na matumizi, haijalishi uko kwenye hali gani kiuchumi. Watu wengi hawatilii maanani suala la kuwa na bajeti, huku wakisema suala la kuwa na bajeti mpaka pale watakapokuwa wamekuza kipato.
Lakini ili ukuze kipato bajeti ni muhimu sana.
Kile kinachoitwa bajeti ni usawa kati ya mapato na matumizi.
Kuweka usawa katika mapato na matumizi, hukuitaji kwanza kuvifahamu vyote viwili.
Watu wengi huweka bajeti ambayo haiwasaidii chochote, kwa sababu hawana uhakika wa matumizi yao. Unakuta mtu anaweka kiasi fulani cha pesa kwenye bajeti yake kwamba ni cha “ matumizi mengineyo” bila kujua kwa uhakika kwamba kiasi hicho cha pesa kitanunua nini au kitafanya kazi gani? Hii sio njia nzuri. Unahitaji kujua kiasi gani unatumia na kinatumika wapi. Unaweza kutumia mwezi mmoja kufanya utafiti, kuangalia ndani ya mwezi mmoja unatumia kiasi gani cha pesa na kinatumika wapi.
Andika kila senti inayotoka kwenye mfuko wako inafanya nini.
Mwishoni mwa mwezi weka matumizi yote katika nyanja tofauti kama chakula, na vitabu. Kwa kufanya hivyo unaweza kuweka msingi wa kuwa na bajeti.
Baada ya kufuatilia matumizi ya mwezi utagundua kama una tatizo au hapana.
Kama matumizi yako ni makubwa kuliko mapato ujue hapo kuna tatizo! Kuna baadhi ya vitu vinachukua pesa lakini unaweza kvipunguza.
Mfano badala ya kununua maji ya kunywa kila siku unaweza kujiwekea utaratibu wa kubeba maji ya kunywa. Au badala ya kuwa unawapa watu ofa kila unapopata pesa, sasa hiyo tabia iache.
Weka pembeni mambo ya muhimu ambayo utayalipia kama vile bili ya maji na umeme. Angalia kiasi gani kimebaki, hiki kiasi kilichobaki ndo cha akiba.
Tathimini kipato chako.
Je, kuna chochote ambacho unaweza kukifanya kuongeza kipato chako?
Katika hali yoyote kuna njia mbili za kubadili hali ya kifedha. Njia ya kwanza ni kupunguza matumizi na njia ya pili ni kuongeza kipato au kwa kununua raslimali au njia nyingine ambayo ni halali. Hizi ndo njia mbili za kubadili bajeti yako.
Panua uwanja wa akiba yako kwa ajili ya baadae.
Kipengele hiki kinahusiana vitu kama likizo, safari na hela ya masomo au vitu vya aina hiyo. Vitu hivi lazima viwekewe mpango mapema kwa kuwekewa akiba. Kama utasahau vitu hivi vitakuja kubadili mwelekeo wa bajeti yako hapo baadae.
Fikria juu ya matumizi ambayo yanaweza kujitokeza mwishoni mwa mwaka au mwaka kesho na yawekee akiba.
Panua uwanja wa akiba kwa ajili ya matumizi ya baadae kwa kuweka akiba kuanzia mwaka mmoja hadi mitano.
Kama utafuata hatua hizi vizuri utakuwa na bajeti nzuri yenye mpangilio wa mapato na matumizi.
Mpangilio wako wa kifedha ni kitu muhimu sana na ni kitu kinachobadilika. Usitegemee bajeti uliyoweka leo itakuwa sawa na bajeti utakayoiweka kesho.
Ni muhimu sana kuwa na nidhamu ya bajeti yako, kama utafanya hivi utakuwa karibu kuwa huru kiuchumi.
Sio vizuri kununua kila kitu kinachokuja mbele yako kwa sababu una pesa.
Endelea kusoma blogu hii kwa makla za kuelimisha na kuhamasisha.
Ni mimi rafiki na ndugu yako.
Godius Rweyongeza
Tuwasiliane
godiuarweyongeza1@gmail.com
0755848391.