Habari za leo rafiki na ndugu msomaji wa
SONGA MBELE BLOG . Imani yangu unaendelea
vyema katika hatua ya kutafuta na kuelekea
mafanikio.Karibu sana katika makala yetu ya
leo.
Je, nawezaje kuondokana na umaskini wa kipesa? Je nawezaje kuingiza pesa kwenye mzunguko ikawa msaada mkubwa kwangu? Siku zote pesa haionekani kutosha. Kuongezeka kwa mshahara hakuonekani kuondoa matatizo ambayo mtu anayo. Kuna mtu aliwahi kusema “mahitaji yako huongezeka kuendana na mshahara wako.”
Katika makala ya leo nitakushirikisha mbinu muhimu ambazo zitakufanya ukuze kipato na kuondokana na usumbufu na hali mbaya ya kiuchumi. Hizi mbinu mshirikishe na rafiki yako ili naye aweze kupata kitu kizuri ulichokisoma.
1. Jilipe mwenyewe kwanza sehemu ya kipato unachoingiza.
Hii kauli najua ni ya kushangaza sana kwa baadhi ya watu lakini lazima nisisitize hiki ndicho chanzo cha kuwa huru kiuchumi.
Kuna imani isiyo sahihi kwamba kinachoingia mfukoni mwako ni chako na hivyo unaweza kukifanyia chochote unachotaka au unachojisikia kufanya. Ebu sasa tuangalie kwa umakini juu ya kile ambacho hutokea kwenye mshahara wako au kipato chako.
Sehemu ya kipato chako hutumika kununua chakula na hivyo kiasi hicho ni cha mkulima au muuzaji wa chakula gengeni.
Nyingine hutumika kununua nguo na hivyo kiasi hicho ni cha mwenye duka, nyingine hutumika katika afya kumbe kiasi hicho ni cha daktari au mtalaamu wa afya.
Kingine unakitumia katika uasafiri na hivyo kiasi hicho ni cha konda. Mambo mengine ambayo hutoa na kupeleka pesa yako kutoka mfukoni ni elimu na mawasiliano.
Je wewe ya kwako inaendaje?
Hii ndiyo sababu inayonipa ujasiri wa kusema jilipe mwenyewe kwanza sehemu ya kipato unachoingiza.
Katika hali kama hiyo tuliyoina hapo juu ina maana mtu utaishia kufanya kazi kubwa sana lakini kipato unachopata kinashibisha tumbo na kinachukuliwa na wengine.Je nitawezaje kujilipa mwenyewe na ninapaswa kujilipa kiasi gani? soma zaidi makala hii ina maelezo ya swali hili.
Siri Ya Babilon Kuwa Mji Tajiri Kuliko Yote Duniani
2. Ongeza uwajibikaji wako
Je akiba yako unaifanyia nini?
Najua kuna baadhi ya watu ambao wakiwa na pesa mfukoni hawatulii mpaka pale watakapokuwa wameitumia yote imeisha.
Na mwingine anapokuwa na pesa ananunua chochote kinachokuja mbele yake. Bila kujali kimo kwenye bajeti au la.
Je wewe ni mmoja wapo? Huu ni ugonjwa ambao kila mtu anapaswa kupambana kuutibu mpaka pale utakapopona.
Usiongozwe na majirani au marafiki katika matumizi. Yaani usifanye kile unachoona wanafanya. Unanunua gari au friji au kabati au meza kwa sababu jirani, rafiki, dada, kaka, mjomba au mtu yeyote wa karibu kanunua?. Nunua kwa sababu kimo kwenye bajeti. Amua kuitumia vizuri kila sarafu na iangize ikufanyie nini?
Kwa wengi chenji ianyorudishwa baada ya kununua kitu huwa inaonekana haina maana sana. Hakikisha hauipotezi hii pia.
Soma zaidi hapa; Wafanyabiashara waliofanikiwa wanavyotunza muda
3. Chagua uwekezaji sahihi.
Baada ya kujilipa mwenyewe kiasi fulani baada ya muda fulani utagundua kwamba akaunti yako inaanza kutuna. Unachohitaji kujua ni kwamba pesa siku zote lazima iwe katika mzunguko na unahitaji pesa ikufanyie kazi. Siri ya mafanikio ni kuwa na pesa inakufanyia kazi.
4. Ifanye nyumba yako iwe sehemu ya kukuingizia kipato.
Nampenda sana Robert Kiyosaki mwandishi wa kutabu cha RICH DAD POOR DAD ambaye ameeleza vizuri sana ni lini nyumba yako inakuwa raslimali na kini nyumba yako inakuwa dhima.
Siwezi kusisitiza kwamba unapaswa kuwa na nyumba yako nzuri na ya kuishi ila anachokisema Kiyosaki ni kwamba unapokuwa na nyumba yako mwenyewe ya kuishi haikupi faida yoyote bali itakachokifanya ni kuondoa sehemu ya kipato chakk na na kukitumia kulipa kodi, umeme na mengine.
Kiyosaki anashauri ununue raslimali kabla ya kununua au kujenga dhima kama nyumba ya kuishi. Raslimali utakayonunua ndiyo itakayogharamia nyumba ambayo utaijenga au kununua.
Kwa wale ambao tayari wana nyumba unaweza kufanya moja kati ya haya au yote kwa wakati mmoja.
- Weka bustani mbele ya nyumba yako ambayo itakuingizia kipato cha kuendeshea nyumba lakini pia itakupa chakula.
- Toa sehemu ya nyumba au vyumba ambavyo huvitumii na uvipangishe vikusaidie kuingiza kipato.
- Unaweza pia kuamua kufanya uwekezaji kwenye nyumba yako mwenyewe mfano unaanzisha duka au kitu kingine ambacho unafikiri unaweza kuwekeza.
5. Ongeza kipato chako.
Kama unajua matumizi yako yanazidi kipato chako, jua hapo kuna shida kubwa sana na hilo lazima lirekebishwe haraka iwezekanavyo.
Unahitaji kuongeza ubora wa kazi yako na kuifanya kuwa bora na ya hali ya juu sana.
Kadri utakavyotoa huduma bora zaidi ndivyo utakavyopata wateja wengi zaidi na hivyo kipato chako kitaongezeka.
6. Kuwa na uhakika wa kesho.
Hatuwezi kuukwepa ukweli kwamba itafikia hatua uwezo wetu wa kufanya kile tunachofanya sasa utapungua. Tumezoea kulima kwa muda mrefu sana lakini utafikia wakati ambapo hatutaweza kulima kama hapo awali.
Tunapendwa sana kazini kwetu lakini utafikia wakati ambapo watakuja vijana na sisi tumezeeka basi hakuna jinsi lazima tuwapishe vijana wachape kazi.
Sasa wakati huo ukifika utafanyaje?
Wazo hili litupe mwanga wa kwamba tusitumie kila kitu bila kujua kwamba kuna kesho inakuja. Umejiaandaaje rafiki?
Nakumbuka kuna watu wengi sana waliuza mashamba yao kijijini kwetu kwa sababu tofauti tofauti leo wapo wanahangaika.
Wapo waliosema “ ngoja niuze maana nikisha kufa hakuna atakaye nijali”
“ watoto watajitafutia wenyewe “
Na wengine walitoa sababu kama hii “ ngoja niuze maana sina hata mtoto wa kurithi mali zangu nikifa sasa hivi nani atarithi mali zangu”
Kwa hakika watu hawa wameuza mashamba yao kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita kwa visingizio kama hivyo na kiukweli wapo wanahangaika wanatafuta watapata wapi mlo wa mchana. Walidhani wanaenda kufa mda huo kumbe bado wanayo safari ndefu ya maisha.
Je wewe ni mmoja wapo?
Je wewe una mawazo kama haya.
Tafakari chukua hatua.
Endelea kusoma makala za kuelimisha na kuhamasisha kutoka kwenye blogu hii.
Ni mimi rafiki na ndugu yako
Godius Rweyongeza
Tuwasiliane
godiusrweyongeza1@gmail.com
0755848391
Asante.
2 responses to “Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Umasikini Wa Kipesa.”
Hongera Sana kwa kutupa mwanga wa kuelekea katika mafanikio. Nimefurahishwa na makala hii yenye mafunzo makubwa.
Mungu akubariki katika Kuendelea kutupatia elimu ya mafanikio kila siku.
karibu sana