Mambo Matano (05) Ya Kuzingatia Kabla Ya Kuanza Jambo Lolote


Habari za leo rafiki yangu na ndugu msomaji wa SONGA MBELE BLOG. Ni imani yangu unaendelea vyema katika hatua kutekeleza na kufikia malengo yako ili uweze kufikia mafanikio. Karibu sana katika mada yetu ya leo.

Katika mada yetu ya leo tutaanza kwa kuona stori nzuri kutoka kwenye Biblia (kitabu cha mwanzo 11:1-5)

Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja

Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. 


 Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. 

Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. 

 Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga

Je, ni nini kilikuwa kwenye akili za hawa watu wazururaji?  Hawa ni watu walioopona baada ya mafuriko.  Lengo langu kukushirikisha hicho kifungu ni kwamaba ninataka tujifunze mambo matano yafuatayo ambayo mimi binafsi nmepata kujifunza.

1. Umoja (lugha moja na usemi mmoja).
Suala zima la umoja ni kitu ambacho kimekuwa kinazungumziwa sana na watu wengi sana. Kuna misemo mingi sana inatumika kuhusu umoja mfano “umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”, “umoja wetu ndio ushindi wetu”, kwa pamoja tunaweza” na misemo mingine mingi sana.  Tukirudi kidogo sana katika uumbaji Mungu alisema “na tumuumbe mwanadamu kwa mfano wetu”.
Mpaka hapo inaonesha kwamba Mungu anafanya kazi kwa umoja. Lakini pia kwa mwanadamu kaumbwa kwa mfano wa Mungu lazima aweke nguvu  kuhakikisha anafikia kipawa ambacho amepewa na mwenyezi Mungu.
Ili tuweze kufikia umoja huu lazima umoja uanzie kwenye akili zetu.
Najua utauliza kivipi?
Ni mara nyingi sana sisi tunakuwa na akili zetu zimegawanyija kufanya mambo mengi sana. Inashika kitu kimoja na kuacha na kugusa kingine. Hii hali haioneshi umoja na umakini wa akili. Kuna umuhimu sana wa kuanza jambo fulani na kulimaliza. Kuna umuhimu sana wa kuanza kusoma kitabu na kukimaliza.
Umoja unahitajika pia katika kazi na shughuli zinazohusisha zaidi ya mtu mmoja. Tunapaswa kuwa na kauli moja hata kama tupo wengi sana. Lakini kauli moja itakuja kuwepo kama akili zetu zitakuwa na umoja kwanza. Katika shughuli yoyote ile tuifanyayo tunahitaji kwa pamoja kuwa na kauli ya umoja kama watu wakiofika SHINARI walivyosemana “tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni”
Ebu na sisi tujisemee kwenye shughuli zetu kwamba “na tufanye kitu fulani”  “na tuimbe”  “na tucheze mpira kwa umoja”  “na tulime” na mambo mengine mengi sana.

2. Ubunifu
Walipofika Shinari walifurahishwa sana na eneo hilo na kuamua kuanza kuishi pale. Sasa wataishije? Watalifanyaje lile eneo liwe na thamani? Kuna maliasili gani zipo wanaweza kuzitumia? Je wachukue hatua gani? Akili ya ubunifu huwa inaangalia kutengeneza mambo mapya katika mazingira yoyote yale. Bila shaka Shinari ulikuwa ni msitu mkubwa sana. Tofauti na uasili wake wa mazingira hakuna kitu chochote kilichokuwa kimewekwa? Ni nani sasa aliwaambia hawa kuhusu habari za kujenga mnara mkubwa kiasi hicho? Ni nani aliwafundisha sasa hawa watu kuhusu kutengeneza matofali? Ni ukweli kwamba watu hawa walikuwa hawajaenda shule wala hawakujua habari za vyuo vikuu. Ebu tujikumbushe kidogo kwenye uumbaji “na tuumbe mtu kwa mfano wetu”. Hii inaonesha kwamba ubunifu ulio ndani ya Mungu wetu tumemegewa kidogo, hivyo haijalishi tumeenda shule au hatujaenda shule bado tunaweza kufanya mambo makubwa kama hawa ndugu zetu wa Shinari walivyoweza kubuni kitu kikubwa sana. Kama hawa wameweza kwa nini wewe usiweze, usikate tamaa songambele

Soma zaidi hapa:  Je, Unafahamu Una Uwezo Sawa Na Hawa Watu

3. Kufikiri
Hili ndilo jicho la akili. Unaona nini hata kama macho yako yamefungwa? Je, unachokiona kina uzuri kiasi gani?  Kila hatua iliyopigwa na kila mapinduzi yanayofanywa yametengenezwa akilini mwetu kwanza.
Huwezi kufika sehemu kimwili kabla yakuwepo pale kiakili. Uko jinsi ulivyo kwa sababu ya kile unachofikiri”. Kwenye stori yetu walisema “na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. 
Wajenge mji  na mnara wenye kilele wapi? Mbinguni. Hakuna utani!! Tafadhari sana usidharau kipawa kilicho ndani yako. Kitumie vizuri. Najua utajiuliza hivi kweli wangeweza kujenga mnara  kufika mbingun? kabla sijajibu swali lako soma pointi inayofuata.

Soma zaidi hapa; Hili Ndio Duka Lako Lenye Kila kitu

4.  Weka malengo.
Watu walijua kabisa ni nini walitaka na walikuwa na malengo akilini mwao. Kama tutafanya vitu bila malengo tutaendelea kuzunguka kwa miaka mingi bila kufika tunapotaka na tutaendelea kutamani mambo mazuri mpaka pale tutakaposindikizwa makaburini.
 Hakutakuwa na kitu cha ziada tunaacha kama kama kumbukumbu duniani. Kumbuka mwanadamu atakumbukwa kwa matendo yake na sio kwa maneno yake. Kuna msemo mmoja wa kiingerza huwa napenda sana kuutumia, msemo huu unasema “easier said than done”. Ni rahisi kusema kuliko kutenda.  Kuwa mtendaji mkubwa sana kuliko msemaji.

5. Matendo.
Dunia haipungukiwi hata kidogo na watu wenye matamanio. Wanatamani kupata vitu mbalimbali bila kuweka juhudi za kuvipata. Dunia inapungukiwa sana na watendaji, watu wanaofanya kile wanachofikiri, watu wenye uwezo wa kuanza kitu kipya ambacho hakikuwahi kufanyika duniani ni wachache, ni wachache sana. Katika stori tumeona Mungu anashuka kuuona mji na mnara ambao walitaka kuujenga.  Walikuwa wamefikiri, wameweka mipango na sasa walikuwa wanaanza matendo. Mungu alitaka kutembelea kile walichokuwa wanafanya. Sijawahi kusikia mtu anatembelea wazo la mtu, labda nimewahi kusikia mtu anatembelea vitu vinavyoonekana na vinavyoshikika. Ni muhimu kujua kwamba wazo halioneshi matokeo,  lakini matendo hufanya. Unaweza kutengeneza tofauti kubwa sana kwenye maisha yako kama utaanza sasa kufanya. Anza kuziweka katika matendo ndoto yako na maisha yako yatakuwa na maana zaidi.

Endelea kusoma makala za kuelimisha na kuhamasisha kutoka kwenye blogu hii. 

Kujiunga na mfumo wetu wa kupoksa makala maarumu za kila wiki BONYEZA HAPA UJAZE FOMU ILI UJIUNGE



Ni mimi rafiki na ndugu yako 
Godius Rweyongeza
Tuwasiliane
godiusrweyongeza1@gmail.com
0755848391
Asante


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X