Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo


Habari ya leo rafiki yangu na ndugu yangu naamini unaendelea vyema katika hatua za kufikia mafanikio.

Ni kawaida sana mtu akikua huwa anaanza kujivunia mambo makubwa sana aliyoyafanya akiwa mdogo au katika enzi za ujana wake. Utasikia mtu anakwambia nilipokuwa mdogo nilikuwa nacheza mpira wa miguu vizuri sana, yaani kama ningekosa basi siku hiyo mechi inahairishwa. Mwingine atakwambia mimi nilikuwa mwimbaji mzuri sana yaani nilikuwa nategemewa kila sehemu. Ukweli ni kwamba sijawahi kumsikia mtu akisema “mimi nilikuwa mwizi au jambazi maarufu sana kiasi kwamba kama ningekosa siku hiyo wizi haufanyiki. Wala sijawahi kusikia mtu akisema kwamba nilikuwa mzembe maarufu sana kiasi kwamba kama ningekosa uzembe usingefanyika. Kiujumla kila mtu huwa anajinenea mambo mazuri sana na maarufu ambayo amewahi kuyafanya enzi za ujana wake.

Je wewe umefanya nini cha kujivunia ili baadae uweze kuhadithia kitu kizuri ambacho umewahi kufanya. Ni fahari kubwa sana kuhadithia jambo zuri sana ambalo umewahi kufanya.

Kama wewe ni mzazi mtoto wako unamuandaaje ili aweze kuwa na historia nzuri. Kumbuka mtoto anaiga kutoka kwa wazazi au walezi juu ya kile wanachofanya. Ukimfundisha mambo mazuri basi moja kwa moja atakuja kufanya mazuri. Ukimfundisha mabaya lazima tu atakuja kufanya mabaya.

Je, kama mtoto wako anakuona wewe mzazi unaharibu maishani yeye atakuja kufanya vizuri na kuwa mwenye mafanikio makubwa sana.

Soma zaidi hapa: Kumbe Huwa Hawafanyi Haya

Ebu tuone mfano huu

Baba mmoja alisafiri na mtoto wake kwenye gari la familia kwenda kutembea. Walipofika njiani askari wa usalama barabarani walimsimamisha baba, kiukweli baba alikuwa na makosa ambayo alipaswa kuchukuliwa hatua za kisheria moja kwa moja. Basi alichofanya baba alitoa kiasi cha hela (rushwa) na kumpa askari, na aliruhusiwa kuondoka na kuendelea na safari.
Kwa kuwa mtoto alishafundishwa shuleni kwamba rushwa ni mbaya na haifai kutoa rushwa, basi mtoto alimuuliza baba yake.
                   Mtoto: umempa nini askari

                    Baba:  pesa kidogo tu

                    Mtoto: Lakini hiyo si rushwa

                    Baba.  Tulia! kila mtu hapa mjini hufanya hivyo.
Basi mtoto alinyamaza lakini kitu hicho kilibaki akilini mwake na hakuwahi kukisahau.

Siku nyingine mtoto alienda na mama yake dukani kununua matumizi. Walipofika mama aliagiza vitu vya sh elfu tatu (3000/-) na kutoa noti ya shilingi elfu tano (5000/-), baade mama yake akarudishiwa shilingi elfu saba (7000/-) kama chenji. Wakaanza kuondoka lakini mtoto  akaamua kumuuliza mama yake.
                  Mtoto:  Kwani mama umenunua vitu vya shilingi ngapi?
                  Mama: shilingi elfu tatu
                   Mtoto:  umelipa shilingi ngapi?
                    Mama: shiling elfu tano (5000/-)
                     Mtoto: Umerudishiwa shilingi ngap?
                    Mama: elfu saba (7000/-)
                     Mtoto: sasa mbona chenji inazidi hata ile uliyoitoa
                      Mama: Tulia! kila mtu hapa mjini hufanya hivyo.

Soma zaidi zaidi Je, Wewe Una Matamanio Au Ndoto?

Basi siku zikaendelea na hatimaye mtoto akapata kazi na kuanza kuuza nyanya kwenye soko. Mtoto akawa anaingiza pesa nyingi sana. Baba yake “alipomuuliza unawezaje kuingiza pesa nyingi kiasi hicho”
Mtoto alisema “Nachukua nyanya nzuri naziweka chini, mbaya naziweka katikati na nyingine nzuri naziweka juu.
Baba yake akamwambia “wewe ni mjanja sana mwanangu”

Itaendelea wiki ijayo..

Endelea kusoma makala za kuelimisha na kuhamasisha kutoka kwenye blogu hii.


Kujiunga na mfumo wetu wa kupokea makala maarumu kutoka SONGA MBELE   kila wiki bonyeza HAPA na ujaze fomu.


Ni mimi rafiki na ndugu yako,
Godius Rweyongeza
Tuwasiliane
godiusrweyongeza1@gmail.com
0755848391
Asante.


One response to “Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X