NIMEZALIWA MSHINDI; Maneno Huwa.


Ni kawaida yetu kuongea maneno mengi sana kwa siku tangu tunapoamuka, mpaka jioni tunapoenda kulala. Maneno ambayo tunayaongea ni mengi sana. Kuna utafiti uliwahi kufanyika na ukagundua kwamba mwanamke kwa siku anaongea maneno 20,000 wakati mwanaume kwa siku anaongea maneno 7,000. Utafiti huu ulifanyika katika chuo kikuu cha California nchini marekani.

Kuna utafiti mwingine ambao ulifanyika, ukagundua kwamba asilimia 97 ya maneno ambayo mwanadamu anayaongea ni hasi, yaani ni maneno ya kumudidimiza.

 Maneno huwa.

Kama wewe kawaida yako ni kuhakikisha kwamba unajirudisha nyuma, na kuongea maneno ambayo ni hasi, basi jua kwamba unaenda kupata kitu ambacho ni hasi.

Hakikisha kwamba unajijaza maneno ya kiushindi kila siku, hakikisha kwamba unapokuwa na watu unaongea na  kuruhusu maneno chanya. Kama utaruhusu watu wakukatishe tamaa, unaweza kufikia hatua ukaacha kabisa unachofanya.

Unaweza kuona kwamba MTU anapokwambia neno hasi ni kawaida, lakini ukweli ni kwamba hii sio kawaida. Maneno haya yanaingia moja kwa moja kwenye ubongo wako, na kuuaminisha kwamba wewe huwezi hata kidogo.

Kama maneno haya yatajirudia Mara kwa Mara kwenye ubongo wako basi jua kwamba itafikia hatua kwamba utaacha kabisa kufanya Kile ambacho unafanya.

Kinyume chake ni sahihi, kama utajijaza na maneno ambayo ni chanya basi itafikia hatua utaanza kuuona ukweli katika Kile ambacho unaongea. Ndio maana Les Brown anakwambia kwamba “mtu mmoja akikwambia huwezi basi jua kwamba wanahitajika watu 17 wa kukwambia kwamba unaweza” ili uweze kuendelea na shughuli yako.

Ukimwaminisha  mtoto (kwa maneno) kwamba huwezi, jua kwamba hatakuja kuweza.

Ndio maana inashauriwa kwamba umwambie mtoto wako maneno chanya hata kama unaona kabisa kwamba kakosea.

Kuna mlezi mmoja ambaye nilimsikiliza siku moja kwenye redio alikuwa na haya ya kusema “kama mtoto wako atafanya vibaya darasani, usimwambie kwamba wewe ni mjinga sana na inavyoelekea huwezi kitu chochote. Wewe sio kama fulani, akili Yako mbovu kabisa! Sijui kwa nini nilikuzaa!!”

Maneno hayo yataingia kichwani mwake na kugeuka kuwa ukweli. Kwa maana maneno ya mtu mzima ni dawa.

Badala yake unaweza kumwambia maneno chanya hata kama amekosea. Mwambie “mimi nakujua mwanangu wewe ni bigwa sana katika masomo, inaelekea siku ulipoingia kwenye mtihani ulikuwa hujashiba vizuri, siku nyingine kabla ya kuingia kwenye mtihani hakikisha kwamba umekula na kushiba maana wewe siku zote huwa unafanya vizuri” aliendelea mlezi huyo.

Siku chache baada ya kuyasikia maneno kama hayo nikaanza kufanya utafiti ili nisikie wazazi huwa wanawaambia nini watoto wao! Ndipo niliposikia mzazi mmoja akimwambia mtoto wake hivi “ wewe mtoto ni mjinga sana, unapenda sana kucheza, darasani unafeli yaani sijui wewe umemfanana nani? Maana hata baba Yako hayuko hivi?”

Hapo ndipo nilipochukua nafasi ya kuhakikisha kwamba nimetoa dukuduku la moyoni na kumwambia yule mama nilichokuwa nimejifunza redioni siku sio nyingi. Maana siku zote huwa naishi chini ya kanuni ya kwamba kila ninapojifunza kitu kipya lazima niwashirikishe watu ambao sio chini ya watatu ili kwa pamoja tuweze kunufaika na kile ambacho nimejifunza.

Kwa bahati njema sana walikuwepo wazazi wawili pale wakinisikiliza. Waliyapokea maneno yangu kutoka kwa msemaji Wangu wa redioni. Muda sio muda mzazi wa pili ambaye watoto wake hawakuwepo hapo alipigiwa simu kujulishwa kwamba na yeye mwanae kashindwa kwenye mtihani. Akiyepiga simu alikuwa na bugudha kubwa sana na alionekana alitaka mtoto yule aadhibiwe vikali sana kwa kushindwa lakini kwa sababu tu mzazi nilikuwa nimemwambia maneno ambayo yanajenga na maneno chanya. Basi mzazi yule alianza kumrudisha chini yule mpinga simu wa upande wa pili na kumwelekeza ni kwa namna gani mtoto anavyopaswa kuchukuliwa. Hilo lilikuwa neno la faraja kwangu.

Kwa nini nimeandika haya yote? Nataka tunifunze somo juu ya neno ambalo tunaongea jinsi linavyokuwa na nguvu kubwa sana kwa watu ambao wametuzunguka.

Kutokana na maneno hayo hapo juu kuna vitu kadhaa vya kujifunza.

1. Hakikisha kwamba umenena maneno chanya kila unapokutana na watu.

2. Kila unapojifunza maarifa mapya ambayo unaona ni msaada kwako, hakikisha kwamba unawashirikisha na wengine maana yanaweza kuwa msaada mkubwa pia kwa hao watu wengine.

2.  Penda sana kujifunza, ila chagua aina ya elimu na ujuzi ambao unapenda kuwa nao. Sio kila kitu ujifunze. Sio lazima kila kipindi cha redio usikikize ila chagua. Chagua. Chagua.

Kwa leo tuishie hapo, naomba tukutane siku nyingine kwenye makala za kuelimisha na kuhamasisha kama hizi.

Ndimi rafiki na ndugu Yako
Godius Rweyongeza
0755848391


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X