Sababu nne Zitakazokufanya Ukumbatie Matatizo


Hivi umewahi kujiuliza kitu gani kitatokea kama tutaishi duniani bila vikwazo. Hivi ushawahi kujiuliza kama tungeishi katika dunia ambayo haina matatizo?

Watu wengi sana huwa wanasema kwamba ingekuwa ni dunia bora sana na njema sana kwa ajili yetu kuishi maisha mazuri na yanayopendeza. Labda! lakini usemi wako si wa kweli.

Ukweli ni kwamba Dunia bila matatizo ingekuwa mbaya, mbaya, mbaya sana.
Yaani, hii ni kusema kwamba hata vitu vizuri ambavyo tunaviona siku ya leo basi visingekuwepo. Tonny Robins Mwandishi na mjasiliamali wa kimarekani anasema kwamba “kila tatizo ni zawadi bila matatizo tusingekua”.

Hivyo kwa msingi huo wa Tonny Robbins ina maana kwamba ugunduzi wote ambao unauona katika dunia hii usingekuwapo kama yasingekuwa matatizo.

Yaani ina maana hata simu hii uliyonayo hapo mkononi mwako usingekuwa nayo! Unashangaa! Kwani hujui simu ni matokeo ya matatizo?
Aya ngoja nikuulize gari limetengenezwa au lipo kama matokeo ya nini?
Je, ndege unayoijua ni matokeo ya nini?

Sina hakika umejibu nini ila jibu lako linapaswa kuwa ni MATATIZO. Robin  Sharma aliwahi kuandika kwamba “hata maumivu yanaweza kuwa mwalimu mzuri”.

Kuna watu huwa wanapenda sana kulalama kila siku. Yaani utawasikia wakisema.
“Kama asingekuwa Adamu na Eva basi sisi tungekuwa bustanini Edeni tunafurahia maisha”?

Pole sana kama na wewe ulikuwa unafikiria hivi?

Binafsi huwa nayapenda sana matatizo. Maana matatizo ni yamezalisha watu wengi sana maarufu. Matatizo yamekuza watu. Matatizo yamejenga mataifa makubwa. Matatizo yametengeneza matajiri. Matatizo yamemeinua waliodaharauliwa. Kumbe ndio maana Padre Faustine Kamugisha anasema kwamba “matatizo si tatizo”.

Kama matatizo yangekuwa ni tatizo basi hata Adamu mwenyewe unayemzungumzia angeishia kulia maisha yake yote baada ya kutolewa katika bustani ya Edeni. Lakini kwa sababu tu alishaaambiwa kwamba anapaswa kupambana na kula kwa jasho lake, basi alishika hatamu ya maisha yake na kuhakikisha kwamba anajijenga vizuri na kuwa mtu bora sana.
Hakika, “matatizo si alama ya kusimama bali ni maelekezo”  kama ambavyo alituasa Robert H. Schuller.

Hapa kuna mambo 4 yananifanya niyapende niyakumbatie na kuyaheshimu matatizo.

1. Matatizo yanatufanya tukue.
Mtoto anapokuwa anajifunza kutembea huwa anaanguka mara nyingi sana. Kuanguka kwa mtoto huwa si kikwazo au kitu ambacho kinamzuia mtoto kuendelea kujifunza kutembea. Tatizo la kuanguka limezalisha wakimbiaji maarufi sana duniani. Limezalisha wachezaji maarufu.

Mtoto anapojifumza kutembea na kuanguka hatusemi kwamba hana miguu.  Sasa iweje wewe unapoanguka ujione kama kilaza? Kwa nini wewe unapoanguka unajiona kama umepoteza mwelekeo?

Umewahi kujifunza baiskeli? Je, ulijisikiaje pale ulipoanguka? Je, uliwezaje kuendesha baiskeli?
Mtazamo wako wakati wa kipindi cha kujifunza na kuanguka ulikuwaje?
Kiufupi naweza kusema hukukubali kuliona tatizo la kuanguka kama tatizo bali uliliona kama kelele tu za chura ambazo huwa hazimuzuii tembo kunywa maji!

2. Matatizo huambatana na ugunduzi mpya.
Kwa kuwa kila tatizo ni somo. Basi lazima tuwe tayari kujifunza kutokana na matatizo hayo.
Ni katika kujifunza huku tunapata kutengeneza kiti kilichobora zaidi

Huwa naipenda sana methali moja ya kimasai ambayo inasema kwamba “ ni matatizo yanayotupeleka mbali”.
Matatizo ya watu kutoonana, yametufanya sasa hivi tuongee kwa kuonana. Zamani iliaminika kwamba “barua ni nusu ya kuonana”. Leo hii ukweli ni kwamba unaweza kuongea na mtu huku ukiwa unamwona. Huu ni ugunduzi uliotokana na matatizo.

3. Matatizo yanatuimarisha.

Huwa naipenda sana historia ya Freddie Roch. Huyu alikuwa mwanamasumbwi wa kimarekani ambaye kila alipokuwa akiingia ulingoni anapandwa na hasira na kuanza kupigana bila kufuata taratibu na sheria za masumbwi. Mwisho wa siku alikuwa anapigwa kwenye hatua za mwanzoni mwa pambano.

Tatizo hili baadae lilikuja kumuimarisha na kumfanya kuwa kocha maarufu wa wanamasumbwi. Hakika kama utaamua sasa kuyaona matatizo katika namna ambayo ni chanya basi hakika yatakuimarisha.

Soma zaidi; maisha unayaonaje?

4. Matatizo ni fursa.
“Fursa siku zote huwa haziji zikiwa na zimewekwa mihuri ya thamani yake” haya ni maneno ya Maltibie Babcock. Wale ambao wanaona chanya katika matatizo ndio ambao huwa wanazitumia. Kama unalalamikia kila tatizo ambalo linakutokea basi maisha yako yote hutakuja kuziona fursa zinazotokana na matatizo.

Kuna kipindi  ambacho kulikuwa na tatizo la kununua umeme TANESCO.  Ndipo waona fursa walipoliona hilo. Wakaamua kuanzisha kitu kinaitwa Max Malipo. Leo hii katika kila kona ya nchi wapo mbashara wanahudumia watu. Tatizo hili kwao halikuwa tatizo. Hakika matatizo si tatizo. Matatizo ni fursa.
Yapende matatizo, zione fursa katika kila tatizo.

Ndimi rafiki na ndugu yako

Kocha Godius Rweyongeza
0755848391
godiusrweyongeza1@gmail.com

Jiunge na mfumo wa kupokea makala maalumu kwa watu maalumu kwa kubonyeza hapa


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X