Jambo Moja Litakaloinua Biashara Yako Popote Duniani.


Ukuaji ni jambo la muhimu sana. Na mwanadamu ni mtu ambaye tunategemea akue kila siku. Ukuaji huu wa kila mwanadamu tunategemea utokee kwenye sekta zote zinazomhusu ikiwa ni kiroho, kimwili na kiafya.

Kama wewe unasema kwamba utabaki jinsi ulivyo basi jua kwamba unazidi kupitwa na wakati. Maana dunia dunia yenyewe tu haibaki ilivyo bali inazidi kubadilika.

Furaha ya mwanadamu siku zote huwa ni kukua. Mtoto akizaliwa tunategemea akue na afikie mafanikio makubwa sana. Macho ya wazazi na jamii nzima huwa yanawekwa kwa mtoto huku kila mtu akiwa anamwangalia kwa jicho la pekee.

Mtoto akianza kutambaa furaha ya wazazi huongezeka mara dufu. Kama ni picha kupigwa basi zitapigwa nyingi, kuonesha kwamba hili ni tukio la kihistoria. Hapo sijazungumzia furaha kubwa zaidi inayokuwepo mtoto anapoanza kutembea, anapoenda shuleni n.k

Kumbe furaha yetu sisi binadamu ni kuona vitu vinakua. Hakuna anayependa kubaki kama alivyo hata kama muda mwingine hatujui ila ukuaji ndio asili yetu…

Hata hivyo ili mtoto akue huwa anahitaji chakula, mavazi na kuhakikisha anatunzwa vizuri ili asishambuliwe na magojwa.

Kama matunzo mazuri hayatafanyika magonjwa, kudorora kwa afya na ukuaji usioleweka hutokea! Hakika hili si jambo jema sana.

Suala la ukuaji halionekani kwa wanadamu tu! Hata kwa viumbe vingine.

Lakini kama ambavyo tumeona mpaka sasa, nyuma ya kila ukuaji wowote kuna UWEKEZAJI.

Hili utake, usitake ndio ukweli.

Ili mtoto akue basi tunamlisha, kumvisha, na kumjali sana huu ni uwekezaji hata kama  huwa hatusemi hivyo.

Soma Zaidi;  Kilichofanywa Na Huyu Na Mimi Naweza Kufanya

Hivi ukinunua ng’ombe anayetoa maziwa kwa wingi kila siku si utafurahi?

Na je, ukiendelea kumkamua kila siku bila kumlisha utaendelea kupata maziwa yale yale? au kiasi kitabadilika? Jibu bila shaka ni KIASI KITABADILIKA tena kwa herufi kubwa. Unajua kwa nini?

Hii ni kwa sababu tu! Hujafanya UWEKEZAJI. Yaani kwa ufupi ni hilo.

Sasa hili suala la uzembe wa kuwekeza limetawala watu wengi sana.

Yaani hadi leo naandika makala hii, nimefuatilia na kujiridhisha na sasa ninasema hivi “watu wengi wanapenda kufanikiwa haraka sana, ila hawapendi kufanya uwekezaji” kama wewe ni mmoja wapo. My friend umepotea.

Wewe unasema kwamba una kigugumizi na unaogopa kusimama mbele ya watu kuongea mwezi wa ngapi sasa! Lakini ni dakika ngapi ndani ya masaa 24 unazitumia kuhakikisha kwamba unaondokana na hilo? Kwa nini hutaki kufanya uwekezaji? Hakika kuondokana na hali hiyo itakuwa vigumu sana. Ukiomba usaidiwe lazima uanze kuweka juhudi binafsi huo ndio ukweli.

Aya wewe mkulima huu mwaka wa ngapi sasa unalalamika kwamba mavuno yamepungua! Je, ushafuata mbinu za kitaalamu unazoambiwa na watu waliobobea katika sekta ya kilimo? Unaona sasa! Hutaki kutumia mbolea, hutaki kununua mbegu KUTOKA kwenye maduka ya mbegu (yaani wewe kwa mwaka wa tano sasa unatunza mbegu) na unategemea matunda ya tofauti. Hakika kwa mwenendo wako huu mafanikio yako nayaona ICU!

Naona umekasirika! Samahani sana mheshimiwa maana sijasema ni wewe! Kwa hiyo usijisikie vibaya!

Soma zaidi; Njia Tisa (09) Za Kuongeza Thamani Katika Kazi Zako
Ndugu yangu mfanyabiashara shikamoo! Nasikia eti! Una ndoto za kumiliki Biashara kubwa sana inayofahamika nchi hii! Hivi hii ni kweli au nimesikia vibaya!
Na Biashara yako unataka iwe na ofisi katika kila kona ya dunia hii. Aisee hongera sana! Ndoto zako nzuri sana! Ebu endelea kuzifanyia kazi.
Tatizo lako moja tu! Unataka biashara yako ikue ila hutaki kuwekeza.

Tangu umeweka mtaji wako wa kwanza hujawahi kuongeza mtaji mwingine tena! Unachofanya pesa yote unayoipata kutoka kwenye biashara unakimbilia kuitumia. Unasema unakula bata! Bata?? Bata wakati unachezea sindano kwenye shimo! Kwa hiyo wewe lengo lako ni kuwa mla bata maarufu au?

Ebu sasa nisikilize! Anza kuwekeza kwenye Biashara yako zaidi ya unavyowekeza kwenye  bata!

Kuna watu walishawahi kula bata, na tena sio vijibata unavyokula wewe kwa sh 10,000 mara moja kwa mwezi. Kuna watu walishakula bata kweli. Jamaa hao wapo kwenye  biblia ila leo ngoja niwaache tu! Maana sikuwa na mpango wa kuwaandika hapa.
Ila ukipata muda kamsome Ayubu! Huyu alikuwa anakula bata kweli! Watoto wake wanafanya sherehe (wanakula bata) na kuwaalika wengine, leo hii wewe unaniambia unakula bata! Kwa elfu kumi tu!!!

Uwekezaji katika jambo lolote lile ni muhimu ili kuleta matokeo bora.
Anza kuwekeza katika wewe
Wekeza katika Biashara yako.
Wekeza katika kipaji chako. Wekeza! Wekeza! Wekeza!

Wewe Ni Zaidi Ya Ulivyo

Kujiunga na kundi la wasp la HAZINA YETU BONYEZA HAPA

Ndimi
Coach Godius Rweyongeza
godiusrweyongeza1@gmail.com
www.songambeleblog.blogspot.com
Ili kupata kitabu cha kutokaa sifuri mpaka kileleni tuwasiliane 0755848391


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X