Vitu Nane (08) Vya Kuzingatia Kabla Ya Kuanza Biashara.


Habari,
Watu wengi sana wamekuwa wakitaka kujihusisha na ujasiliamali kwa sasa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuwa na chanzo kimoja tu cha kipato si jambo la kukumbatia wala kupongeza. Ili kuweza kufikia uhuru wa kiuchumi, ambapo mtu utaishi maisha ambayo hayana hofu ya kesho, ujasiliamali ni jambo ambao haliepukiki. Hata hivyo watu wengi sana wamekuwa hawajui ni vitu gani unaweza kuzingatia kabla ya kuingia kwenye ujasiliamali. Katika makala ya leo nimeanika kila kitu. Isome uielewe kwa ajili ya manufaa yako. Baada ya hapo mshirikishe na rafiki yako, kumbuka vitu vizuri ni vya kushirikishana na marafiki zako. Usipate Maarifa haya na kuamua kujichimbia tu! Mshirikishe na Rafiki yako, mwambie naye amshirikishe na Rafiki yake.
Karibu.

Soma zaidi; Huu Ni Utumwa Ambao Kila Mtu Anapaswa Kuuepuka

1. SOKO
Kabla ya kuingia katika biashara hakikisha kwamba unajua soko lako liko wapi na lina watu gani! Hakuna bidhaa ambayo utaanzisha ambayo haiitaji kwenda sokoni.
Je, kwenye soko lako umelenga wanawake, wanaume au watoto. Kuwa makini usije ukaandaa bidhaa za wanaume ukazileta kwa wanawake kwa kisingizio kwamba wanawake watawanunulia waume zao. Ingawa utakuwa umepeleka bidhaa yako kwa watu lakini utakuwa hujapeleka kwa watu sahihi. Au unaandaa bidhaa za urembo na unazipeleka kwa wanaume. Lijue soko lako sasa.

Je, Soko lako lina kipato kiasi gani?
Je, soko litaweza kumudu gharama za bidhaa yako?
Lakini swali la msingi kabisa ni kujiuliza soko linahitaji nini?
Unapaswa kutatua matatizo ya soko sio kuleta bidhaa ambayo soko halipendi. Ukitengeneza bidhaa unayoipenda wewe mwenyewe tu. Jua kamba utainunua mwenyewe. Tatua matatizo yanayolikumba soko ili upate pesa.

Soma Zaidi; Lifahamu Kusudi Lako

2.  MTAJI
Je, unao mtaji wa kutosha kuhakikisha kwamba unazalisha bidhaa za kutosha?
Ili kujua mtaji unaouhitaji basi unapaswa kuangalia gharama za uzalishaji. Gharama za kodi ya pango. Gharama za Kodi ya mamlaka ya mapato nchini(TRA). Unapaswa pia kujua gharama zote utakazoweka kabla ya kuanza kupata kipato (cashflow).Jumla ya gharama zote zinazohitajika ndizo zitakazotuambia mtaji unaouhitaji.

Soma zaidi; Mambo Matatu Ambayo Kampuni Yako Inapaswa Kuwa Nayo

3. PESA YA DHARURA
Hujaiujua biashara mpaka pale utakapokuwa umeingia katika biashara. Hakikisha kwamba unakuwa na pesa ya dharura ambayo utaitumia kama kutakuwa na jambo ambalo litajitokeza baadavua wewe kuanza biashara. Biashara pia huwa hazina tabia ya kusimama ndani ya kusimama ndani ya siku moja. Kumbe kuna wakati utapaswa kuweka nguvu na muda wako katika kuhakikisha umeisimamisha. pale biashara itakapoyumba wewe ndipo utakapoitumia ile pesa yako ya dharura

4. JINA
Hakikisha kwamba biashara yako unaipa jina. Jina la biashara yako linaweza kuwa ni la kiswahili,kiingereza, au la kilugha.
Pengine jina lako linaweza kuwa na mchanganyiko wa lugha zote hizo au mchanganyiko wa lugha mbili. mfano biashara yako unaweza kuiita Maji Pure Drink.
Unaweza pia kuita biashara yako jina lako. Mfano unaweza kuiita Songambele hotel, James Barber Shop n.k Lakini pia unaweza kuiita jina la sehemu ulipo. Mfano Dar City Bus Service au Mbozi Bus Service n.k.

Kwa mjasiliamali makini kuna majina hawezi kuyatumia kwenye biashara yake. Mfano chukulia mtu anaiita biashara yake KISIWA CHA BANGI TANZANIA. Au unaiita biashara yako POMBE NA MIHADARATI TU!? Loooo! Hapo utakuwa hujaoneaha ukomavu wala utakuwa hujaonesha umakini katika kile unachofanya.
Hakikisha unachagua jina linaloendana na kile unachofanya.

Soma Zaidi; Mambo Mawili (02) Kuepuka Kuhairisha
 
5. Jifunze kuwasiliana.
Mawasiliano ni jambo la muhimu sana katika biashara. Kabla ya kuanza au kuingia katika biashara unahitaji kuhakikisha kwamba umejifunza kuhusu mawasiliano. Ninapozungumzia kuhusu mawasiliano simaanishi kuongea tu. Mawasiliano ni zaidi ya kuongea. Mawasiliano yanahusisha kusoma lugha ya mwili, lugha ya maneno, sauti inayotoka kwa mtu. Yaani kuwasiliana kuna mambo mengi makubwa sana. Kwa hiyo unapaswa ujifunze kuwasiliana kabla ya kuingia katika biashara na baada ya kuingia katika biashara. Mfano kama unauza unaweza kugundua kwamba mteja amechukua bidhaa fulani lakini anaonekana hajatosheka,, yaani bado anaihitaji bidhaa nyingine. Sasa kama wewe hujajifunza lugha hii ya mwili unaweza kupoteza pesa ambayo ingeingia haraka mfukoni mwako.

Muda mwingine mteja anaweza akawa anapita tu dukani kwa kuchungulia lakini ukaisoma  lugha ya mwili wake sasa ukaamua kuchukua hatua na kumkaribisha. Kwa kumwambia tu “karibu sana nikusaidie nini”? Akavutika kuja na ukauza mauzo makubwa sana.
Kumbuka kwamba wewe mfanya biashara ndiye anayemhitaji mteja. Mteja hakuhitaji wewe. Hivyo mpokee vizuri sana. Ongea naye vizuri sana.

Kutokujua kuwasiliana muda mwingine kunaweza kukukosesha fursa nzuri sana. Inawezekana wewe una wazo zuri sana la biashara lakini hauna mtaji wa kuanza nao. Rafiki yako ana mtaji mkubwa ila hana wazo la biashara. Kwa hiyo wewe ukakosa fursa nzuri za kung’aa kwa sababu tu hujui kuwasiliana na watu. Anza kujifunza ujuzi huu wa kuwasiliana sasa. Hata kama hauna biashara.

6. JIFUNZE KUUZA
Kama utazalisha bidhaa bora sana na ukawa huuzi hata ubora wake hauwezi kujulikana. Mauzo ndiyo moyo au damu ya biashara. Kama hakuna mauzo hakuna biashara. Bila mauzo afadhali ukafunga biashara . Unahitaji kujifunza kuuza
 Kuna wakati utakataliwa na kuna wakati utapokelewa vizuri sana. Haya yote ni sehemu tu ya wewe kuendelea kujifunza na kujenga biashara yako. Mauzo ni jambo ambalo unahitaji kulifahamu nje ndani. Kumbuka kwamba washindi siku zote ni wale wanaouza sio wale wenye bidhaa bora. Na mtu nambari moja unayepaswa kuanza kuanza kuuza ni wewe mwenyewe. Uza kwanza ujuzi wako. Watu wakujue wewe ni nani!

7. Huduma kwa wateja.
Hapa ninapozungumzia huduma kwa wateja wengi wanajua labda kwamba huduma kwa Wateja ipo kwenye mitandao ya simu kama vodacom, tigo au kwenye mabenki kama NMB, CRDB. Hii sio imani ya kweli. Huduma kwa wateja ipo katika biashara yoyote. Hata kama una biashara ndogo. Jinsi unavyohudumia na kuongea na watu ambao wamekuzunguka sasa itatuambia ni kwa jinsi gani utakuwa ukiwasiliana na kuhudumia wateja. Kama lugha yako kwa watu sio nzuri jua kwamba kuna kitu utakipoteza kwenye biashara. Ndio walewale unaingia dukani kuulizia bei ya bidhaa.
“Dada kalamu hii shilingi ngapi”? Unasikia anakujibu “kwani wewe huoni hapo bei si imeandikwa, au wewe ni kipofu? Hapa umepotea njia hili si duka la vipofu”
Huduma kwa wateja wako ni jambo la muhimu sana.
Ebu jiulize sasa kama ungekuea tayari dukani ungempokeaje mteja wako? Kama tayari una biashara unampokeaje mteja? Badilika sasa. Jinsi ya kuwapokea na kuwahudumia wateja wako.
Je, unavyompokea ndivyo na wewe ungependa upokelewe?

Soma zaidi;  Nianzie Wapi?

8. WASHINDANI

Hakuna biashara ambayo unaweza kuianzisha ikawa haina washindani kwa asilimia 100%. Kila biashara huwa ina washindani wake. Na wewe unahitaji kuwafahamu washindani wako, wako wapi? Wana nini ambacho wewe huna? Na wewe una nini ambacho wako hawana? Kwa hiyo kabla ya kuanza biashara hakikisha unazunguka maeneo yote ya karibu na wewe ili uweze kuwasoma washindani wako. Angalia mapungufu ambayo wanayo na unaweza kuyatumia kama ngazi yawewe kupandia kuelekea kwenye mafanikio ya biashara yako.

Wewe Ni Zaidi ya ulivyo sasa.
Kujiunga na kundi la wasp la HAZINA YETU BONYEZA HAPA
Ndimi
Coach Godius Rweyongeza
godiusrweyongeza1@gmail.com
www.songambeleblog.blogspot.com
Ili kupata kitabu cha KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI  tuwasiliane kupitia 0755848391

Bonyeza hapa ili uweze kupata makala maalumu kila wiki.


6 responses to “Vitu Nane (08) Vya Kuzingatia Kabla Ya Kuanza Biashara.”

  1. Asante sana kwa mwongozo,hii elimu inafaa sana kwa wajasiriamali na wafanya biashara.Mafanikio katika biashara kweli yanategemea vitu vingi sana siyo tu ubora wa bidhaa,

    kumdumisha mteja ni jambo la msingi sana mana ndio anayeitangaza biashara yako mahali kwingine,hii inakupunguzia hata wewe gharama za kuitangaza bidhaa husika.

    Ukiona unapata wateja wapya tu katika biashara yako au hakuna mteja anàyerudikwa mara ya pili au wanarudi kwa kiasi kidogo sana lazima ufanye utafiti tatizo liko wapi.je, ni ubora mdogo? au huduma mbovu? n.k

    Kauli mbaya katika biashara ndio chanzo kikubwa pia cha kudumaza au kuuwa kabisa biashara yako

    Jambo lingine kama umeajiri jitahidi kuwafundisha waajiliwa wako na uwape stahiki zao kwa wakati ilikupunguza vikwazo na kauli mbovu kwa wateja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X