Njia Tano (05) Za Uhakika Za Kupoteza Muda


Ukitaka kujua umuhimu wa mwaka mmoja muulize mwanafunzi aliyerudia mwaka

Habari ya siku hii njema sana rafiki yangu. Imani yangu kwamba leo hii ni siku njema sana kwako na unaenda kuitumia siku hii kufanya makubwa sana.

Moja kati ya rasilimali muhimu sana katika maisha ni muda. Kuna watu kila kukicha wanautafuta muda zaidi kwa kuwaajiri watu wengi ili wapate muda wao, wakati huo huo kuna watu wanapoteza muda kila kukicha na kutafuta mbinu za kuupoteza zaidi.

Na cha kushangaza zaidi ni pale unapokuta watu wanaopoteza muda ni wale wanaojua wazi kwamba muda ni rasilimali adimu. Huwezi amini hawa watu ndio wanaopoteza muda sana.

Unaweza kushangaa mtu anaanza wiki na kuimaliza akiwa hajui kitu gani cha maana ndani ya wiki amekifanya. Mtu anaamka asubuhi mpaka jioni inafika akiwa amechoka ila hana jambo kubwa sana ambalo amelifanya. Je, ni wewe?
Je, unajua ni wapi muda wako unapotelea kila siku?

Katika kufuatilia jambo hili kwa ukaribu wa hali ya juu sana nimegundua kuna njia tano ambazo watu wanazitumia kupoteza muda wao kila siku.

NJIA YA KWANZA
KUPIGA SOGA MUDA WA KAZI
Je, ni mara ngapi marafiki zako huwa wanakufuata kazini ili mpige soga? Je, huwa unafanyaje watu kama hawa wakija kwako. Si jambo la ajabu kukuta kwamba watu wamepiga kambi sehemu, huku mtu fulani akiwa anafanya kazi. Na hawa wengine badala ya kuja kumsaidia walau kazi unakuta wanapiga soga na kupiga soga.
Duh, kweli haya ni maajabu.

Rafiki yangu kama.kuna watu wa aina hii hakikisha kwamba hauwaruhusu, kuja kazini kwako. Waambie haswa kwamba kwako muda wa kazi ni muda wa kazi na muda wa kupiga soga haupo.

Waambie watu wawe wanakuja kwako wakiwa na miadi (appointments) na wewe. Sio mtu anakuja kila anaopojisikia.

Kuwa mkali kweli juu ya suala hili mwisho wa siku utafaulu.

NJIA YA PILI

KUCHATI
Mitandao ya kijamii, imekuja na vitu mbali mbali. Kuna watu imewaimariaha na kuna watu imewabomoa.
Cha kushangaza, kuna watu wanapoteza zaidi ya masaa matano mtandaoni wakizurula. Yaani wanatoka huku wanaenda kule bila jambo la msingi. Kwa hakika mitandao hii ni mwizi mkubwa sana wa muda wako. Iepuke sana. Usiitumie kama hakuna ulazima.

Soma zaidi; Nijibu Sms 1000?Au Nisome Kurasa 1000

NJIA YA TATU,
KUFUATILIA MAISHA YA WATU WENGINE,
Kama mpaka sasa unatumia muda wako kufuatilia maisha ya watu wengine basi hufai. Ndio hufai. Samahani sana kama lugha ambayo imetumiwa utakuwa hujaipenda. Ila.jirekebishe. badala ya kufuatilia maisha ya watu wengine basi kufuatilia maisha ya mtu mmoja tu ambaye ni wewe.

NJIA YA NNE, KUONGEA NA SIMU
kama wewe mpaka sasa kila muda unaweza kuongea na simu jua kwamba hujakomaa. Lazima uwe na muda maalumu wa kuongea na simu kwenye siku yako, lakini pia lazima uwe na muda maalumu wa kujibu jumbe fupi za watu.

Usiwe mtu wa kwamba ukipigiwa simu muda wa kazi unapokea,

Ukipigiwa muda wa chakula unapokea,

Ukipigiwa muda wa kulala unapokea.

Mh, hakikisha unakuwa na muda maalumu wa kupokea simu.
Waambie na rafiki zako watakuelewa tu.

NJIA YA TANO,
KUTOKUWA NA RATIBA
je, baada ya hapa utaenda wapi?
Kama.hujui baada ya kusoma makala haya utaenda wapi jua kwamba hauna ratiba. Usiwe mtu wa kupeperushwa na upepo. Hakikisha unapangilia siku yako kila siku na kuifuata. Hii itakufanya uweze kufanya kazi zako kwa ufanisi mkubwa sana.

Rafiki, chukua hatua kwa haya tuliyojifunza leo.

Ndimi,
Godius Rweyongeza


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X