Vitu Vinne (04) Vinavyowafanya Waajiriwa Kuendelea Kuajiriwa


Habari ya siku hii njema sana rafiki yangu. Imani yangu kwamba leo umekuwa na siku njema sana na bado kuna juhudi zaidi unazidi kuweka ili kuhakikisha kwamba unaweza kufika unapotaka kufika. Hongera sana rafiki yangu.

Hivi ushawahi kujiuliza kwa nini watu wanaendelea kukaa ajirani ingawa wanajua wazi kwamba kukaa ajirani hakuwezi kutoshereza mahitaji yao?
Ukiongea na watu walio ajirani watakwambia kipato ni kidogo na njia pekee ya kuondokana na hili ni kuwa na biashara zako lakini bado wanaendelea kuajiriwa?  Sasa kwa nini inakuwa hivi? Kwa nini watu hawawezi kuanzisha biashara hata kama wanajua faida zake.
Leo hii napenda kukishirikisha sababu zinazowafanya watu waendelee  kukaa ajirani.
Mwisho nitakushirikisha jinsi ya kuondoka kwenye mtego huu.

1. Uhakika wa mshahara

Ajira siku zote zinakupa uhakika wa mshahara. Yaani kila mwisho wa mwezi unakuwa na uhakika kwamba mshahara upo tu. Lakini kwenye kwenye biashara kitu kama hiki hakipo. Kuna wakati biashara inalipa hadi mwenyewe unafurahi na kuna wakati biashara inahitaji kiasi cha pesa kutoka kwenye mfuko wako. Sasa kutoeleweka huku, kunawafanya watu walio wengi waogope ajira. Kitu wanachofanya ni kuamua tu kuendelea na ajira.

2. Usalama wa kazi
Ajira inakuwa na usalama. Yaani unakuwa na uhakika kwamba ukiumwa mwajiri wako atakupa likizo, au hata mambo yasipoenda vizuri unaweza kuomba likizo ya wiki na kupumzika. Lakini kwenye biashara wewe ndiwe mwenyewe. Ukishinda ni wewe mwenyewe. Ukishindwa ni wewe pia. Sasa hali hii inatia hifu kidogo ndio maana watu walio wengi wanaogopa kabisa kuanza biashara.

3. Uoga wa maamuzi
Ukiwa ajirani kuna maamuzi hayakuhusu kabisaa!  Yaani wewe unachofanya ni kufuata maamuzi ya bosi, basi maisha yanaendelea. Lakini kwenye biashara maamuzi yote ni juu yako. Ukifanya maamuzi sahihi ni wewe. Ukishindwa kufanya maamuzi sahihi ni juu yako pia. Sasa watu wengi wakiwa na hofu hii hapa wanaogopa kuingia ajirani.

4. Wameandaliwa kuwa waajiriwa
Elimu yetu tangu shule ya msingi mpaka chuo kikuu inasisitiza na kuwapa wanafunzi aina kuu mbili za maarifa na ujuzi.
>>elimu ya kusoma na kuandika
>>elimu ya kazi

Aina hizi mbili za elimu zinamwandaa mwanafunzi kuwa mwajiriwa. Hivyo kwa namna moja au nyingine mtu mwenye elimu hizi lazima tu ataendelea kuishikilia ajira maisha yake yote. Hakuna jinsi ambavyo mtu huyu anaweza kuacha ajira.

Sasa hizi ndizo sababu zinazowafanya watu waendelee kuajiriwa. Lakini sisi hatuwezi kuendelea kuzikumbatia sababu hizi hata iweje.

Moja ya sifa ya mjasiliamali ni kuvunja sheria ambazo zinakuwa zinaaminiwa na kushikiliwa na watu walio wengi na kuja na zake. Basi kama hizo sababu zilizoandikwa hapo juu ni sheria sisi tunaenda kuzivunja.
Tutazivunja ili tuje na za kwetu, mpya na zinazotufaa. Usiogope. Na hapa ndivyo unaweza kuzivunja

1. Badala ya kuogopa kwamba itakuwaje endapo nitaishi bila ya kuwa na mshahara, jua kwamba ukianzisha biashara na kuikuza itakulipa zaidi ya hapo. Lakini pia biashara inaweza kukulipa zaidi ya mshahara unavyoweza kukulipa.

2. Jiulize kama kuna watu wameweza kufanya biashara wakaweza.
Chochote kile ambacho kimefanywa na mwanadamu akaweza kukikamilisha kwa ubora jua kwamba na wewe unaweza. Hivyo rafiki yangu chukua hatua sasa.

3. Kama unaogopa juu ya hali itakavyokuwa endapo utaacha ajira na kuingia kwenye ujasiliamali. Yaani unajiuliza itakuwaje? Uko wapi mshahara? Basi, hapo jua kwamba unapaswa kujipanga juu na kuweka akiba ya kukutosha wewe kuweza kuishi miezi zaidi ya sita wakati utakapokuwa hauna kipato cha uhakika kwenye ajira.

4. Maamuzi ni sehemu ya maisha. Hivyo hakuna siku ambayo unaweza kusema maamuzi ambayo nimeyafanya sasa ni sahihi kuliko ambayo nitayafanya kesho. Kitu kizuri kuhusu maamuzi ni kwamba ukifanya maamuzi mabovu leo, hutakuja kurudia maamuzi yale yale kesho yaani utakuwa tayari umepata somo. Maana kosanhuwa harirudiwi mara mbili. Hivyo chukua hatua, fanya maamuzi hata kama yanaonekana ni mabovu.

5. Wakati shuleni umefundishwa na kupewa ujuzi wa aina mbili kama ambavyo tumeona hapo juu. Sasa ni juu yako leo kuongeza aina mbili nyingine za ziada.
>>elimu ya pesa
>>elimu ya kujitambua

Hizi elimu zitakufanya ujitambue kwa undani wewe ni nani? Lakini pia elimu ya pesa itakupa uwezo mzuri wa wewe kutumia vizuri pesa yako.

Rafiki yangu, ninaamini kama utazitumia vyema aina hizi za elimu, kwa hakika utakuwa bora sana kila siku.

Hayo ndio machache ambayo nilipenda kukushirikisha rafiki yangu kwa siku hii ya leo. Imani yangu kwamba umenufaika kwa kiasi kikubwa sana. Anza kuyafanyia kazi haya haya ambayo tumejifunza.

Tukutane kwenye meza ya wanamafanikio.

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X