Kati ya vitu ambavyo huwa havipendwi na watu walio wengi sana ni ngazi. Yaani kupanda ngazi hatua kwa hatua ni jambo ambalo huwa linachukiza watu walio wengi. Ndio maana unakuta mtu anadiriki kupanda ngazi tatu kwa mkupuo ili awahi kumaliza kuzipanda ngazi hizi.
Watu wengine wameenda mbali zaidi kwa kuhakikisha kwamba wanaweka lift katika maeneo mbali mbali ili kuepusha watu kupanda ngazi.
Hivi ushawahi kujiuliza umuhimu wa kupanda ngazi moja baada ya nyingine?
Ebu tuchukue tu mfano wa kawaida. Ulipokuwa shule ya msingi darasa la tano ungeambiwa unarushwa darasa la saba ungejisikiaje? Bila shaka ungefurahi sana, kwa sababu kuna ngazi moja ambayo ungekuwa umeruka.
Je, madhara ya kuruka hiyo ngazi unayafahamu?
Ngazi zipo kukuimarisha, kukujenga na kukufanya wewe kuwa wewe.
Ukiruka ngazi sio kwamba unakuwa umekwepa ngazi, bali jua kwamba kuna wakati utafikia utatamani ungekuwa umepitia hiyo ngazi. Maana kuna kitu utakosa.
Huwezi kujua umuhimu wa kuwa kileleni, kama hujawahi kuwa chini kabisa. Raha ya kuwa kileleni ni kwamba unafurahia manufaa uliyoyapata baada ya kazi.
Huwezi kuburudika kama hujafanya kazi inayostahili kiburudisho unachopata.
Kwa hiyo siku zote na muda wote, kuwa tayari kulipa gharama za kuwa mahali husika. Usipende tu kuruka ngazi. Ngazi zipo ili zikufikishe wewe mahali sahihi kwa namna sahihi.
Sehemu pekee unapoweza kuruka ngazi na ukafika unapoenda bado ukafurahi ni kwenye ghorofa. Ni hapa tu ambapo unaweza kupanda lift na ukafika kwenye kilele na maisha yakaendelea kama vile hujaruka. Lakini maeneo mengine ukiruka ngazi jua kwamba ipo siku tu utapaswa kulipa gharama ya hiyo ngazi uliyoruka.
Kazi ya kufanya siku hii ya leo,
Anza kuzipenda ngazi,
Zione kama sehemu ya kukuimarisha wewe wala sio kukuangusha
Asante sana,
Tukutane kwenye meza ya wanamafanikio.
Hahahah! Tukutane kwenye meza ya wanamafanikio
Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391
KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA
HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA