Usifanye Kitu Hiki Kikiwa Cha Kwanza Unapoamka Asubuhi


Habari ya siku hii njema sana ya leo rafiki yangu. Hongera kwa kupata nafasi nyingine ya kwenda kuishi. Nafasi nyingine ya wewe kwenda kuweka alama katika dunia hii. Hakika hii ni nafasi ya kipekee sana, hakikisha unaitumia vyema maana ikipita ndio hiyo imepita.  Haijirudii hata kidogo.

Hivi huwa ukiamka kitu chako cha kwanza kufanya huwa ni kipi? Je, unaagalia simu yako iko wapi? Unasali? Unafanya mazoezi? Huwa unafanya nini?

Tupo katika zama ambazo karibia kila unayekutana naye ana simu tena simu jaja (smartphone).

Uwepo wa simu hizi umefanya watu wengi sana wanapoamka asubuhi kitu kikubwa sana wanachokuwa wanawaza ni kuwasiliana. Hivyo unakuta kwamba mtu analala na simu kitandani kabisa. Akiamka asubuhi kitu cha kwanza kinachofanyika ni kuchukua simu yake ili aanze mawasiliano.

Tena kutokana na uwepo wa mitandao ya kijamii, facebook, instagram n.k basi mtu anapoamka anataka kujua ni kitu gani kinaendelea kwenye mitandao hii. Anataka ajue ile picha yake aliyoiweka kwenye mitandao hii inaendeleaje. Yaani kama vile amefanya uwekezaji mkubwa kwenye mitandao hii, hivyo asipoufuatilia atapoteza.

Soma Zaidi: Swali Unalopaswa Kujiuliza Kabla Ya Kulala

Kibaya zaidi ni pale anapokuwa amepitiwa usingizi jana yake huku akiwa anachati. Basi akiamka atakimbia kuichukua simu ili ajue wale watu aliokuwa anachati nao walimjibu nini. Kwa hakika inasikitisha sana.

Soma zaidi: Njia Tano Za Uhakika Za Kupoteza Muda

Rafiki yangu, mambo haya ni bora ukawa unayasikia kwa wengine lakini sio wewe unayeyafanya. Hivyo unapoamka asubuhi kitu chako cha kwanza kufanya hakipaswi kuwa kushika simu mkononi. Wala sio kuingia kwenye mitandao ya kijamii.

Nakuhakikishia kwamba kama utaianza siku yako kwa kuingia kwenye mitandao hii basi nina hakika utapoteza sana muda wako kwa siku nzima.

Ubovu wa mitandao hii ukishaona kitu kimoja, watakuletea kingine na kukwambia na hicho kinakufaa. Hivyo na chenyewe utataka ukione . Kama ni video utataka uiangalie. Ukimaliza kuiangalia utajulishwa tena kwamba sehemu fulani kwenye mtandao huo kuna kitu kingine kizuri. Hivyo unaweza kuamka saa kumi na moja ukajikuta inafika saa moja hujafanya kitu chochote cha maana. Uuh! Bonge upotezaji.

 Yaani ni aibu kwa mtu mzima kama wewe hapo kupoteza masaa mawili mtandaoni ukiwa hufanyi jambo la maana unafuatilia umbea juu ya umbea.

Hivyo basi, unapoamka kitu cha kwanza kufanya kwako kisiwe kushika simu na kuingia mtandaoni.
Kuna mambo mnne muhimu sana ambayo unapaswa kuyafanya kila unapoamka asubuhi.
Mambo haya nilishayaandikia makala siku za nyuma na hivyo unaweza kuyasoma HAPA.

Na pale unapomaliza mambo haya ukashika simu, usiende kwenye mitandao ya kijamii tafadhari. Chukua simu yako soma kitu chanya. Kinaweza kuwa ni kitabu au makala chanya.

Kiufupi ni kwamba muda wako wa asubuhi wa siku yoyote usiutumie kuingia kwenye mtandao wowote wa kijamii kama wewe hauna jambo la maana unafanya huko.

Utumie muda huu kufanya kazi zitakazokuingizia kipato.
Unaweza kuwa na mradi wako wa kuku ambao unausimamia unapoamka asubuhi kabla ya kwenda kwenye kazi ya ajira.

Ukiona unapoteza muda mwingi sana mtandaoni. Tena asubuhi. Basi ujue kwamba hujapangilia vizuri ratiba yako. Ebu jifikirie tena.

Asante sana rafiki yangu na hongera sana kwa siku hii ya leo. Anza kufanyia kazi kitu hiki tukichojifunza siku ya leo.

Asante sana, tukutane kwenye meza ya wanamafanikio.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X