Moja kati ya hazina kubwa sana ambazo dunia yetu inazo ni vitabu. Vitabu ni hazina kubwa sana ambayo ndani yake kuna kila aina ya madini.
Kama umewahi kusikia kwamba watu wanachimba dhahabu ardhini basi dhahabu pia inaweza kuchimbwa kwenye vitabu. Na dhahabu hii itakusaidia sana wewe kuweza kusonga mbele na kupiga hatua kubwa sana.
Mwezi uliopita. Yaani mwezi wa sita, nilipata nafasi ya kusoma kitabu kimoja kizuri sana katika dunia hii. Na kitabu hiki sio kingine bali ni kitabu cha NAPOLLEON’S HILL GOLDEN RULES. (Kwa kiswahili KANUNI ZA DHAHADU ZA NAPOLLEON HILL)
Kurasa za kitabu hiki hapa zimeeleza kwa umakini kanuni ambazo Napolleon Hill alikuwa akizisisitiza enzi za ujana wake wakati anaandika katika majarida mbali mbali kwa wakati huo.
Kama wewe ni mtu ambaye amewahi kusoma vitabu vya Napolleon Hill utakuwa unafahamu kanuni ambazo Napolleon Hill anasisitiza siku zote haswa katika kitabu chake cha Think and Grow Rich.
Katika kitabu hiki hapa kanuni hizi hapa hajaziacha nyuma. Ikiwemo kanuni ya kujenga picha, kuvumilia n.k
Kikubwa sana na ambacho kinanifanya leo hii nikwambie usome kitabu hiki ni upekee wa kitabu hiki wa kuzungumzia juu ya saikolojia ya binadamu. Na jinsi unavyoweza kuitumia wewe kupata unachohitaji.
Katika makala haya hapa nitakushirikisha kitu kidogo sana kati ya kile nilichokisoma. Baada hapa utapaswa kukisoma kitabu hiki wewe mwenyewe ili upate kujifunza kikubwa zaidi. Kama utahitaji kitabu hiki tafadhari sana wasiliana nami, ili niukuelekeze njia nzuri ya kukipata bure kabisa (kwa mfumo wa nakala tete au soft copy)
Mwandishi anatushirikisha kwamba watu wanapokuwa katika kundi fulani basi kufikiri kwa watu hao kunakuwa katikati. Yaani kunakuwa hakuna hata mtu mmoja anayefikiri yeye kama yeye. Badala yake ule mkumbo wa kikundi (ambao kiuhalisia sio akili ya mtu yeyote) ndio unawaongoza watu. Hivyo watu hujikuta wakifanya maamuzi kwenye kikundi huku wakiwa hawajafanya maamuzi sahihi.
Mfano unaweza kukuta watu wanaandamana wakisema, tunataka haki zetu. Lakini kwenye kikundi hicho ukimchomoa mmoja na kumuuliza je, haki yako unayoitaka ni ipi?
Unaweza kushangaa hata haki zenyewe anazodai hazijui kabisaaa!
Lakini kwenye kikundi mtu huyuhuyu anajiona ameonewa. Hajatendewa haki na anayimwa uhuru.
Kwenye kikundi mtu huyu haki zake zimevunjwa kwa asilimia mia moja.
Sasa kitu gani kilimfanya mtu huyu aandamane bila kujua hata haki zake ni zipi? Jibu ni kwamba alienda na mkumbo wa kikundi.
Kikubwa nikichojifunza hapa ni kwamba kabla ya kufanya maamuzi, hasa yale yanayohusisha kikundi unapaswa kukaa na kufikiri kote kote na kuangalia faida na hasara za kile kitu.
Kama kitu kinakufaa basi endana nacho. Kama hakikufai usijishughulishe nacho.
Kwa kufanya hivi utaepuka hatari nyingi sana. Mfano mnaweza kuwa katika ofisi mtu mmoja akaamua kusema kwamba sasa tuwe na sherehe ya kupongezana kwenye ofisi yetu. Watu wote wanaweza kukubaliana juu ya hili hapa. Lakini ukiangalia je, wanapongezana kwa lipi? Hata huoni.
Kwa hiyo wewe ukiangalia vitu kwa jicho hili la kutoongozwa na kikundi, utaepuka mengi sana.
Utaepuka kupoteza muda bila ulazima.
Utepuka pia kupoteza pesa.
Maamuzi ya kikundi ni mazuri lakini maamuzi yako binafsi yanayoambata na tafakari ni muhimu zaidi
Rafiki yangu kuna mengi sana ya kuongelea kutoka kwenye kitabu hiki hapa. Ila kikubwa sana naomba wewe sasa uchukue jukumu la kusoma kitabu hiki hapa ili upate kujifunza zaidi na zaidi.
Kiukweli kama mwezi huu unapaswa kusoma kitabu basi soma hiki. Kama mwaka huu unasoma kitabu kimoja basi wewe soma hiki hapa.
Asante sana rafiki yangu. Nakutakia wakati mwema, na mchakato mwema wa kufanyia haya tunayojifunza.
Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391
Asante sana