Vitu Vitatu (03) Vitakavyoongeza Ufanisi Kazini Kwako


Naam, hongera sana kwa siku nyingine ya kuishi hapa duniani. Ukiona umeamka tena ndani ya siku nyingine basi jiulize kitu gani kikubwa leo unaenda kufanya?

Ni thamani gani unaenda kuiweka siku hii ya leo?
Hayo ni maswali muhimu sana ambayo unapaswa kujiuliza.
Wakati kujiuliza maswali kutakufanya uongeze ufanisi mkubwa sana. Lakini bado nakuongezea vitu vingine vitakavyokufanya uongeze ufanisi kwenye kazi ndani ya siku hii ya leo.

1. PATA DAKIKA TANO ZA MAPUMZIKO KILA BAADA YA KUKAMILISHA KAZI FULANI
Ukifika ofisini pangilia kazi kulingana na umuhimu wa kazi. Kazi zile ambazo wewe unaona kwamba ni za lazima na unapaswa kuzifanya basi hakikisha kwanza unaanza na hizo.

 Baadae fuatisha hizo nyingine ambazo sio muhimu sana kwako.

Kila mara unapomaliza kazi za muhimu basi pata dakika tano za kupumzika. Kama ulikuwa umekaa kwenye kiti, basi toka kwenye kiti. Kama kazi yako ilikuwa ni ya kuandika kwenye kompyuta basi badilisha hata hata kazi kwenye dakika hizi tano za mapumziko.

Dakika hizi chache za mapumziko zitakufanya upate nguvu kubwa sana pale utakaporudi kuendelea na kazi zako.
Kama kazi yako ni moja na inachukua muda mrefu, basi unaweza kuiweka kwenye vipengele. Kipangilie kila kipengele muda wake. Ukimaliza kipengele hicho basi pumzika kwanza kabla ya kuendelea.

2. PATA MWANGA WA JUA
Katika zama za sasa ni rahisi mtu kukaa kwenye ofisi muda mrefu bila hata kutoka nje kuuona mwanga wa jua. Ila jambo ambalo wewe mwanamafanikio unapaswa kulifahamu ni kwamba kwenye dakika tano zile za mwanzo za mapumziko, basi unaweza kutoka nje kidogo kwenye mwanga wa jua. Kitu hiki kidogo sana kitakupunguzia hali ya kusinzia utakapokuwa umekaa ofisini.  Maana kwa kawaida ubongo wa binadamu unapokaa kwenye giza unafahamu kinachofuata ni kulala. Ila ukipata nafasi kama hii ya kuwa unaona mwanga wa jua, basi ubongo utakuwa makini sana.

3. VUTA PUMZI KWA NGUVU KILA MARA
Kila unapopata muda kupumzika. Au ndani ya dakika tano hizo za mapumziko basi, wewe pata pia muda wa kuvuta pumzi kwa nguvu walau mara tano. Hali hii itaondoa msongamano wa hewa chafu mwilini na kuongeza hewa safi. Lakini pia chakula katika mwili wako kitapata nafasi ya kumengenywa na kuvunjwa vunjwa zaidi. Hivyo utazidi kupata nguvu zaidi ya kufanya kazi zako.

Tena unapovuta pumzi hakikisha unaangalia jinsi tumbo lako linavyopanda na kushuka. Furahia kitendo hiki maana ni watu wachache sana huwa wanafanya. Mwingine tangu januari mpaka disemba hajawahi kukaa na kupumua kwa nguvu. Yeye ilimradi kaamka basi anatembea tu. Hata hajui kama anavuta pumzi au la!

Rafiki, naomba niseme kwamba  kama unafanya kazi, basi ifanye kwa ufanisi. Kiasi kwamba watu wajue kwamba wewe huwa huna utani kwenye utendaji wa kazi.

Na nilichokushirikisha leo lengo lake ni kwamba uongeze ufanisi kwenye kazi zako unazofanya.

Ubora wa bitu vitatu nilivyokushirikisha leo ni kwamba vyote unaweza kuvifanya kwa pamoja. Na ubora zaidi ni kwamba unaweza kuanza leo. Hata kama umebanwa kiasi gani hakikisha unapata muda huu. Hata kama utaopunguza dakika zikawa tatu. Ila hakikisha unapata muda huu.

Asante sana rafiki,
Tukutane kwenye jukwaa la wanamafanikio

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA


HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA


One response to “Vitu Vitatu (03) Vitakavyoongeza Ufanisi Kazini Kwako”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X