Maswali Matano (05) Ya Kujiuliza Siku Yako Ya Kuzaliwa


Juzi tarehe 05/08 ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa. Nashukuru sana wale wote mlionitumia salamu za pongezi. Hakika kwangu siku hiyo ilikuwa ni siku ya muhimu sana. Miongoni mwa mengi yaliyofanyika ilikuwa ni mimi kukaa chini na kujiuliza maswali kadha wa kadha haswa kuhusu uwepo wangu hapa duniani.

Ni maswali ambayo katika hali ya kawaida ni vigumu mtu kujiuliza. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu wanakuwa  wanakimbizana na mambo mengi sana. Hivyo kama mtu hataamua kutenga muda wa kukaa peke yake na kujiuliza maswali haya, basi anaweza kuishi miaka 80 bila kujiuliza maswali haya na kuyapatia majibu yake.

Maswali haya yanahitaji utulivu wa akili na yanahitaji nidhamu katika kuyajibu. Unaweza kuanza kuyajibu lakini kama hauna nidhamu basi yakaishia tu juu juu bila ya wewe kuyajibu kwa undani.

Kwa hakika maswali haya ni muhimu mno kila mtu akapata kujiuliza maswali haya, sio tu siku yako ya kuzaliwa bali kujiuliza maswali haya kila mara unapopata nafasi.

Maswali haya kama utajiuliza ukaona kwamba yamekusaidia sana, basi mtafute rafiki yako mmoja tu na umshirikishe maswali haya.
Kiukweli utakuwa umefanya jambo la maana sana na utakuwa umenisaidia mimi kutimiza kusudi langu la kuwepo hapa duniani.

Sasa haya hapa ndio maswali matano ya kujiuliza

MIMI NI NANI?
Swali hili ni gumu kuliko maswali mengine matano ambayo nitakuandikia siku ya leo. Ni swali ambalo linakuhitaji wewe kukaa chini kufikiri ili kupata jibu sahihi.
Watu wengi katika kujibu swali hili huwa wanajikuta wanasema kwamba wao ni mawaziri, mimi ni daktari, mimi ni mwalimu na majibu mengineyo mengi ya aina hiyo.
Ingawa wanakuwa wamejibu lakini sio kwamba majibu wanayotoa ni sahihi.

Jibu la mimi ni nani linapaswa kuonesha ni kitu gani ulikuja kufanya hapa duniani. Kinaweza kuwa kitu cha kisiasa, kinaweza kuwa ni kitu cha kibiashara, kibunifu n.k

Kabla ya wewe kuwa daktari ulikuwa wewe. Sasa huo uwewe wako wa awali ndio tunautaka kwenye kujibu hilo swali wala sio cheo.
Kusudi lako linaweza likawa limekupelekea kupata cheo cha uwaziri lakini  uwaziri usiwe kusudi. Ni ngumu kidogo kumeza ila ukitulia kutafakari utaweza kunielewa ninachoongea hapa.

Ebu angalia viumbe vingine. Viumbe hivi pia vina kusudi la kuwa hapa duniani. Ndege kusudi lao kuruka, lakini bado kwenye urukaji wanatofautiana. Wapo ambao wanaweza kuruka hata kama kuna kimbunga maana kusudi lao liko hivyo na wengine hawawezi.

Hata rangi za mmea unazoziona zina kusudi la kuwepo hapa duniani. unaweza kuangalia mti fulani una rangi fulani, ukajisemea moyoni au hadharani kwamba rangi fulani huipendi, ila kumbe ile rangi ipo kuvutia aina fulan ya wadudu. Na wadudu hao wasipoiona ile rangi basi wao hata hawajisikii vizuri. Sasa wewe kama wewe unahitaji kuwa makini na kulijua hili hapa.

Unapaswa kujua kila kitu kipo hapa kwa kusudi maalumu uwe unataka au hutaki. Na kusudi hilo ndilo likitimizwa kila kiumbe kitafurahishwa na uwepo wa kiumbe kingine.
Lakini kama kusudi hilo halitatimizwa kuna viumbe vitaumizwa kutokana na ukweli kwamba utimizaji wa kusudi wa viumbe wengine unaweza ukawa unategemea kutimiza kusudi kwa kiumbe fulani. Hahah! Hapa usichanganyikiwe, ngoja nikueleze kwa mfano rahisi sana. Utimizaji wa kusudi la nyuki unategemea uwepo wa maua fulani yanayozivutia. Bila uwepo wa maua haya basi nyuki watashindwa kutimiza kusudi lao. Unaona eeh!
Vivyo hivyo kwa binadamu. Utimizaji wa kusudi lake kuna muda unategemea utimizaji wa kusudi la mtu aliyetangulia au aliye naye. Sasa kama mtu huyo (ambaye ni wewe) hataweza kutimiza kusudi lake. Basi jua kwamba atakuwa amefanya wizi mkubwa.

Na mtu anajua kusudi lake kwa kujiuliza mimi ni nani?
Jibu la swali hili hapa sio cheo, au mamlaka uliyonayo bali ni uwezo ulio ndani yako. Sasa kaa chini ujiulize swali haya. Je, mimi ni nani?

Soma Zaidi: Uchambuzi Wa Kitabu: THE ALCHEMIST

NIMETOKA WAPI?
Wanasayansi, wanadini na watu mbali mbali wamejaribu kujibu swali la binadamu ametoka wapi? Swali hili limekuwa linajitokeza kwenye vichwa vya watu tangu uwepo wa dunia. Swali hili hapa limepewa majibu mbali mbali kulingana na watu mbalibali.

Sasa nikuulize wewe, umetoka wapi? Jibu la swali hili hapa ni muhimu sana kwako kulijua.

Kwa nini kujihangaisha kutafuta jawabu la swali hili hapa wakati watu walishajibu kwenye vyanzo mbali mbali vya vitabu.

Ni kweli, watu mbali mbali walishajaribu kujibu swali hili hapa ila wewe pia unapaswa kujua jibu la swali hili hapa?

Hii ni kutokana na ukweli kwamba chanzo chako ndicho kinaweza kutupa jibu sahihi la swali la kwanza. Yaani jibu la mimi ni nani?

Kwa sababu mtengenezaji wa kitu ndiye huwa anasema kwamba hiki kipo duniani kufanya kazi hii na hii. Mtengenezaji wa kitu ataenda mbali kukwambia kwamba ili kitu hiki kifanye kazi basi hauna budi kuweka hiki au kile ili kitu hiki kifanye kazi.

Mfano mtengenezaji wa gari ndiye anayejua kabisaa kwamba gari hili ni maalumu kwa ajili ya mizigo, na gari hili ni maalum kwa ajili ya kutalii, jingine kwa ajili ya ksafirisha watu. Kitu hicho anakijua mtengenezaji kwanza kabla ya mtu mwingine yeyote. Sasa ukijua mtengenezaji wa kitu ni nani unaweza kumuuliza je, hiki kazi yake ni ipi?

Ni kwa jinsi hii hii huwezi kuhangaika kutumia gari lako. Kama magari yangekuwa tu yanakutwa njiani na kuokotwa bila maelekezo ya kimiminika gani kitumike basi kila mtu angekuwa anafanya  majaribio kujua kimiminika gani kinafaa zaidi. Huyu angejaribu maji, mwingine pombe, mwingine petroli, na mwingine uji n.k
Lakini kwa kuwa mtengenezaji wa kile kitu yupo ndio maana anatupa maelekezo kwamba humu petroli. Na gari linaanza kazi mara moja. Au anasema humu weka dizeli na gari linafanya kazi bila kusita.

Kumbe ni muhimu kwako kujua wewe umetoka wapi ili sasa uweze kuenenda katika njia sahihi. Badala ya kujaribu kila kimiminika yaani, uji, maji, petroli, dizeli n.k utaenda moja kwa moja kwenye kimiminika husika na kuanza kutumia hicho kimiminika.

SWALI LA TATU NINAENDA WAPI?
Sasa baada kujua wewe ni nani? Na umetoka wapi, sasa kifuatacho ni wewe kujua unaenda wapi!

Je, wewe unaenda wapi?
Kama umeweza kujibu maswali ya kwanza vizuri basi swali hili hapa litakuwa rahisi sana.
Unakwenda wapi? Kwa nini unakwenda huko? Je, unakwenda na nani?
Je, kuna uzuri kiasi gani unauona mbele yako?
Hayo ni maswali muhimu sana unayopaswa kujiuliza kwenye kipengele hiki.

JE,  NIKO WAPI SASA HIVI?
Mpaka sasa hivi umeshajua ni wapi unaekea ila je, kabla hujaelekea huko, unajua kwa sasa hivi uko wapi?
Jiulize swali hili pia. Kama umeweza kujibu swali la kwanza na la pili vizuri kabisa hapo sina shaka swali hili nalo  litakuwa rahisi.

Soma Zaidi: Hiki Ni Kitu Ambacho Wewe Unacho Peke Yako

 JE, NIKIFA NATAKA HISTORIA YANGU IANDIKWEJE?
Hivi ushawahi kijiuliza ukifa watu watasemaje juu yako. Je, ungependa kitu gani kisemwe kwenye msiba wako.
Hiki ni kitu muhimu sana ambacho unahitaji kuwa nacho kwenye akili yako.

Na kurahisisha kazi basi hapa jenga picha ya wewe uko kwenye jeneza na watu watano wamesimama kwenye jeneza lako
Wa kwanza ni mama, mtoto au mje wako, wa pili ni rafiki yako, wa tatu ni mwalimu wako, wa nne ni mshauri wako wa kiroho na wa tano ni mgeni kabisa hujawahi kumwona. Je, watu hawa wanasema nini juu yako. Je, wanachosema unakipenda? Sasa kuanzia leo hii anza kufanyia kazi kile ambacho ungependa watu hawa waongee juu yako.

Soma Zaidi: Iko wapi Sehemu Tajiri Duniani Nikatengeneze pesa

Haya ndio maswali matano muhimu sana, sana ambayo kila mtu anapaswa kujiuliza. binafsi nilijiuliza maswali yote haya juzi ambayo ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwangu. Hata baadhi ya maswali huwa najiuliza mara kwa mara walau mara moja kwa wiki ili kujua kama nipo kwenye njia sahihi au tayari nimepotea.

Rafiki na wewe anza kujenga utaratibu wa kujiuliza maswali haya. Jiulize maswali haya mpaka pale utakapokuwa umepata majibu yanayokufaa.

Soma Zaidi: Jua Kusudi Lako

Haya Ndio Mambo Unayopaswa Kuyazika

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA


HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA

KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X