Utajiri wa Mataifa
Ukurasa wa 37-47
Kupanda na kushuka kwa thamani ya pesa
Jana tuliona historia ya pesa ilivyoanza na tukaishia kuzungumzia kitu kinachojulikana kama thamani.
Nilisema kwamba thamani ya kitu hutofautiana na leo tunaenda kuona vitu viwili vya awali vinavyofanya pesa iwe na thamani ya juu au chini.
Soma Zaidi: UCHAMBUZI WA KITABU; WEALTH OF NATIONS-2 Historia Ya Pesa
Kwanza kabisa ifahamike kwamba pesa imetokana na baadhi ya madini. Na haya madini ndiyo yanajulikana kama chuma, dhahabu, shaba n.k
Sasa madini haya hupatikana kwa viwango tofauti kati ya nchi moja na nyingine. Kuna nchi unakuta ina shaba ya kutosha ila dhahabu kidogo,
Nchi nyingine ina dhahabu nyingi ila haina chuma.
Sasa turudi kidogo katika historia , watu wa eneo husika walikuwa wanatumia madini yaliyokuwa yamewazunguka kama pesa. Na hivyo madini hayo ndiyo yalikuwa yanapewa thamani kubwa sana kuliko madini mengine.
Kwa hiyo kama ungeenda eneo ambalo lina shaba nyingi zaidi ya dhahabu, maana yake shaba ilikuwa na thamani kuliko dhahabu.
Ungeweza kwenda na ndoo moja ya dhahabu ukabadilishiwa kwa kupewa kikombe kimoja cha shaba, kwa sababu shaba ilikuwa na thamani eneo hilo kuliko dhahabu.
Hivyo kitu cha kwanza kabisa kilichokuwa kinafanya pesa iwe na thamani au isiwe na thamani ni UWEPO wa madini husika yanayotengeneza pesa kwenye eneo husika.
Kitu cha pili ambacho pia hakijapishana na cha kwanza na upatikanaji wa madini husika linapokuja suala la kuchimba. Kadri ilivyokuwa inachukua muda kidogo kuchimba madini ya pesa na kuyapata, ndivyo pia madini haya yalikuwa kwenye hati hati ya kuwa na thamani kidogo.
Na kadri ilivyokuwa inachukua muda kuyapata ndivyo thamani yake ilkuwa inakuwa kubwa.
Kiufupi jambo hili tunaweza kuliweka hivi,
Kadri unavyotumia kiasi kikubwa kuwalipa watu wanaotafuta madini ya pesa ndivyo madini hayo yatakavyokuwa na thamani, mwisho wa siku pesa yake itakuwa na thamani.
Kumbuka jana tulimalizia kwa kuona kwamba, maji yanapatikana kwa wingi ila yana thamani kidogo kulinganisha na dhahabu ambayo haipatikani kwa wingi ila ina thamani kubwa.
Jambo hilo unaweza kuliunganisha hapa maana hapa ndio kwake. Kinachofanya maji yawe na bei kidogo ni kwamba yanapatikana kirahisi kulinganisha na dhahabu.
Ndio maana lita 20 za maji huuzwa kwa bei tofauti kulingana na upatikanaji wake. Katika eneo ambalo maji ni shida unakuta lita 20 wanauza mia tano au hata elfu na zaidi.
Lakini katika eneo ambalo maji sio shida sana, utakuta lita 20 zinauzwa kwa 100,au 200. Wewe mwenyewe utakuwa umeona hili.
Rafiki yangu, bado hatujafika. Tutaendelea kuangalia kilichomo kwenye kitabu hiki kijulikanacho kama UTAJIRI WA MATAIFA. kesho tutaendelea tena kuona ni nini kinafanya pesa iwe na thamani kubwa au kidogo. Usikose.
Lakini pia mpaka hapa najua umeshajaa maswali mengi sana kichwani mwako. Je, una swali gani?
Nitumie swali hilo kupitia wasapu tu 0755848391
Au godiusrweyongeza1@gmail.com
Nitakujibu swali lako.
Asante sana,
Tukutane kwenye jukwaa la wanamafanikio.
Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391
www.songambeleblog.blospot.com