Unapaswa Kuwa Na kitu Hiki Hapa Ili Kupata Mafanikio Makubwa Sana


Hongera sana rafiki yangu kwa nafasi ya leo ambayo ni ya kipekee sana. Hakikisha unaitumia vyema ili uweze kusonga mbele na kupiga hatua kubwa.

Kwa kawaida ili uweze kupiga hatua fulani na kufika sehemu kuna vitu unapaswa kuwa navyo.
Ili uweze kusafiri kutoka eneo moja mpaka jingine unahitaji kuwa na tiketi
Ili upate chakula kwenye hoteli, basi unapaswa kuwa tayari kulipa gharama,

Vivyo hivyo ili uweze kufikia mafanikio makubwa basi unapaswa kuwa na nidhamu.
Ni rahisi sana kuanzisha kitu, lakini pia ni rahisi kuacha. Ni rahisi kuanza kujifunza kozi mtandaoni lakini bila nidhamu utaacha.

Unaweza kuanzisha biashara, lakini bila nidhamu utaacha kabisa.
Kwa hiyo unahitaji nidhamu ili uweze kupata matokeo makubwa sana.

Neno nidhamu limepewa maana tofauti tofauti kutoka kwa watu mbali mbali.
Lakini kwa leo naomba tuseme haya kuhusu nidhamu.
Nidhamu ni uwezo wa kuhairisha raha za muda mfupi kwa sasa ili uje kupata raha za muda mrefu baadae.

Nidhamu pia tunaweza kusema ni hali ya kujikataa wewe mwenyewe, kuwa tayari kubeba majukumu yako na kusonga mbele. Hapa unasema kwamba hata wengine wasemeje, lazima nisonge mbele bila kuacha.

Nidhamu pia ni uwezo wako wa kujizuia kufanya vitu fulani, hata kama una uwezo wa kuvifanya, ila kwa sababu havikusumi wewe kufikia mafanikio makubwa sana unaamua kuachana navyo kabisa.
Mfano mzuri hapa tunauona kwa wachezaji, ili mtu aweze kuwa mchezaji bora na murua kabisa, kuna baadhi ya vitu anapaswa kuachana navyo. Mfano pombe na baadhi ya vyakula.
Vyakula hivyo hivyo vikiliwa na watu wengine havina madhara, ila kwake haifai kuvila vyakula hivi.

Sasa na wewe unapaswa kuijenga nidhamu yako kwa namna hii, kiasi kwamba utakuwa tayari kuachana na baadhi ya vitu kwa manufaa yako mwenyewe.

Tunaweza kuongea mengi sana. Ila kama hauna nidhamu, huwezi kufanikiwa.
Nioneshe mtu mwenye mafanikio nikuoneshe nidhamu ilipo.

Sasa ni wakati wako wa kuamua kuwa na nidhamu. Ebu achana na kughairisha, achana kabisa na sababu za kwa nini huwezi kufanya kitu fulani badala yake weka juhudi ili kuweza kukifikia kitu ambacho unafanya.

Asante sana, tukutane kwenye jukwaa la wanamafanikio.

Soma Zaidi: Viashiria Vitano (05)  Vitakavyokufanya Uendelee Kuwa Masikini Maisha Yako Yote

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA


HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA

KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X