TAFAKARI YA WIKI: Unatumia Mabadiliko Mitandao Ya Kijamii Na Intaneti Au Inakutumia?


Hongera sana rafiki yangu kwa zawadi ya maisha ndani ya wiki nyingine mpya kabisa. Wakati tunaendelea kupumua na kufurahia maisha, mambo pia yanazidi kubadilika. Kwa sasa tumekuwa kwenye zama za mabadiliko makubwa sana, ambapo ukilala na kuamka unasikia au kuona mabadiliko mapya ambayo yametokea.
Kwa hiyo mabadiliko ni makubwa sana kila iitwayo leo. Na sisi pia hatupo nyuma, kutaka kuona mabadiliko zaidi na zaidi. Ndio maana utasikia watu wakiomba, “Ee mwenyezi Mungu nijalie maisha marefu niweze kuona yanayotokea mpaka nitakapokuwa na miaka 80/90/100″
Hii ndio kusema kwamba watu hawapendi kupitwa na mabadiliko haya.

Mabadiliko haya ni mazuri sana maana yanarahisisha sana kazi na mawasiliano.
Mfano zamani iliaminika kwamba barua ni nusu ya kuonana. Ila kwa ulimwengu wa sasa, barua ni sawa na kutoonana kabisa😀😀😀. (Japo barua bado ni muhimu sana).

Ulimwengu wa sasa hivi nusu ya kuonana imehamia, kwenye mitandao ya kijamii. Maana unaweza kuongea na mtu ukimwona alipo na anachofanya kutoka kwenye kila kona ya dunia. Hii imerahisishwa na uwepo wa mitandao ya kijamii kama wasapu kupitia (whatsapp video call), facebook, instagram, skype na mitandao mingine mingi.
Kwa sasa hivi msemo wa barua ni nusu ya kuonana  hautumiki tena, badala yake unasikia msemo wa DUNIA NI KAMA KIJIJI.

Sasa wiki hii tutafakari unanufaikaje na dunia hii kuwa kijiji? Au unaishia kuwanufaisha watu.

Kama kawaida kwenye kila zama huwa kuna watu ambao huwa wananufaika na zama husika. Kwenye zama za viwanda akina Thomas Edison, Henry Ford, Rockfeller, Edwin C.Burns na wengineo wengi, walikuwa watu walionufaika.
Kwenye zama za sasa hivi tunaona wamiliki wa mitandao ya simu wakifaidika (maana imefikia hatua mtu kuwa na kifurushi limekuwa ni hitaji la muhimu). Akina Zuckerberg, Bill Gates na wengineo wengi pia wananufaika na zama hizi. Sasa swali langu kwako unanufaikaje na mitandao hii?

Jibu lako hapa👇🏾👇🏾 kwanza kabla hujaendelea kusoma.
……………………………………………………………………………………………………………

Sasa leo hii nina njia chache za kukuwezeha kunufaika na mitandao hii.

1. WAFANYE WATU WAKUJUE UNAFANYA NINI
Hivi kwa siku unaingia mara ngapi mtandaoni? Bila shaka hata hukumbuki hata hujui ni mara ngapi! Pengine unafungulia data tangu asubuhi mpaka jioni ili ujumbe wowote ukiingia uuone ukiwa wa kwanza.

Swali jingine, je, kwa muda wote huo unaokuwa mtandaoni watu wangapi wanajua wewe unafanya nini? Nakuuliza wewe?

Ni kosa kubwa sana kukaa kwenye mitandao hii ukizurura bila ya watu kujua wewe ni nani, na unafanya nini?
Ni kosa kubwa kuwanufaisha watu kila siku bila ya wewe kupata hata senti moja. Yaani ni bonge la kosa!!!

 Sasa wafanye watu wakujue wewe ni nani!

👉kama umebadilishana namba na mtu na huu ni mwezi wa tatu ila hajui wewe ni nani jua ulifanya kosa, ila usirudie tena.

👉anza kuwaelimisha watu juu ya kile unachofanya

👉kupitia kuwaelimisha unaweza kuwaambia bidhaa zako

👉lakini pia utajenga timu ya watu wanaopenda kuwa na wewe

👉utaanza kuandika jina lako.

2. KUWA NA SEHEMU AMBAPO WATU WATAKUJA KUTEMBEA
Zamani matembezi yalikuwa ni kwenye vijiwe ili kupiga soga. Kwa sasa, vijiwe vimehamia mtandaoni. Yaani huku ndipo kuna stori na kila aina ya taarifa. Sasa je, wewe unatembelea vijiwe gani?

Tengeneza kijiwe chako ambacho watu watakuja kupiga stori na kuondoka. Na vijiwe hivi kwa sasa vinaweza kuwa ni blog au you tube channel. Huku unapata nafasi ya kuonesha kipaji, ubunifu na uwezo wako. Watu watakuja huku kutembea na wataanza kulijua jina lako wewe!!

3. KUWA NA BIDHAA INAYOTATUA TATIZO
Kwa zama za sasa hivi matatizo sio tena matatizo, bali matatizo ni biashara, daraja na nguzo ya kuelekea mafanikio makubwa. Kwenye zama hizi   hakikisha unakuwa na bidhaa fulani ambayo inatatua matatizo ya watu. Kwako matatizo yasiwe tatizo kama ambavyo wengine wanayaona, kwako matatizo liwe daraja.

4. PUNGUZA MITANDAO UNAYOTEMBELEA ILA ONGEZA VITABU UNAVYOSOMA
Zama za sasa hivi zina taarifa nyingi, nyingi kweli. Unaweza kukuta habari moja imeandikwa na zaidi ya blogs 100 na imewekwa kwenye you tube chanell zaidi ya 10. Na unaweza kukuta mtu unazunguka huku kote ili usome kila kitu.

Naomba nikwambie kwamba huhitaji kutembelea mitandao hii yote.
Kwa punguza mitandao hii ambayo unatembelea. Ila ongeza vitabu unavyosma.
Kama bado ulikuwa hujaanza kusoma vitabu basi leo hii kachukue vitabu hivi vitatu na uanze kusoma kikojawapo
👉THINK AND GROW RICH
👉LEAD THE FIELD
👉RICH DAD POOR DAD
Ili uweze kuishi kwenye ulimwengu ambapo ugunduzi mkubwa unafanyika kila kukicha basi, unapaswa kuwa na maarifa makubwa. Na maarifa makubwa yapo vitabuni.
Kwa hiyo soma, vitabu kadri ya uwezo wako.
Yaani, soma, soma, soma vitabu!

Ila
👉👉achana na habari za umbea
👉👉achana na kupoteza muda kufuatilia maisha ya watu.

5. USIFUATILIE TENA MAISHA YA WATU
Najua kwa sasa utakuwa umekuwa bingwa na mtaalamu wa kufuatilia maisha ya watu. Yaani uanafuatilia nani anafanya nini?
Unafuatilia nani anatoka na nani? Na mambo mengine kama hayo.
Sasa achana na hizo biashara. Anza kuwa wewe, ishi kama wewe na nenda kama wewe.

Kuna mambo mengi sana ambayo mpaka sasa hivi huyajui kuhusu wewe. Hivyo hakikisha unaanza kujijua kwanza.

Asante, sana.
Kuwa na wiki njema sana

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA


HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA

KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X