Haya Ni Mambo Ya Kipekee Sana Usiyoyajua Kuhusu Biashara


Hivi ushawahi kuanza kitu baadae ukaja kugundua kwamba picha uliyokuwa nayo juu ya kitu ni tofauti? Au umewahi kupata safari ya kwenda mahali ambapo hukuwahi kwenda kabla, ukawa unajenga picha katika akili yako, ila ikatokea kwamba picha ya eneo uliyojenga ni tofauti na uhalisia? Je, umewahi kuwa unawasiliana na mtu katika simu ambaye hujawahi kukutana naye kabisa maishani mwako, ila ukawa unajenga picha fulani ya huyo jamaa kama vile unamuona?  Unaanza kumwona kama jamaa fulani hivi mnene, mrefu kiasi, mweupe, anayechangamka, ila ile unakutana naye tu unaona ni mtu wa tofauti? 
Najua walau moja ya mambo hayo yamewahi kukutokea au zaidi ya hayo. Ila hayo hayatokei tu kwenye hivyo vitu nilivyotaja peke yake, mambo haya pia hutokea kwenye biashara. 
Kama tayari umeanza biashara, kuna mambo ambayo nina uhakika ulikuwa huyajui na uliingia kwenye biashara kichwaa kichwa bila kuujua uhalisia huu. Ila kama bado hujaingia kwenye biashara, basi hii ni nafasi ya kipekee sana ambayo umeipata kuyajua mambo haya ambayo watu wengine huja kuyajuwa wakiwa wamechelewa. 
1. Kanuni ya 10,000
Mtu anapokuwa na wazo la biashara, moja si moja huwa anaona mafaniko makubwa. Papo hapo huwa anaona biashara yake imefika mbali na yeye tayari amenunua magari binafsi huku akitembea mitaani na kula bata.
Ila ukweli ni kwamba biashara haikui kwa siku moja. Kitaalamu inaonekana kwamba unahitaji masaa 10,000 ili uweze kufanikisha kitu kimoja unachofanya. Yaani ili biashara yako iweze kufikia hatua za kimataifa, unahitaji masaa 10,000 ili iweze kufikia ukuu huo. Na masaa haya hatuwezi kuyapata kwa siku moja wala sio ndani ya wiki. Maasaa haya yanaweza kuchukua miaka na miaka kulingana na muda unaouweka kwenye biashara yako kwa siku moja. Kama kwa siku moja unatumia masaa mawili tu kuiboresha biashara yako, kuitangaza, kuongea na wateja n.k
Basi itakuchukua miaka mingi sana kulinganisha na yule anayutumia masaa matano kwa siku kuifanya biashara yake. 
Kwa hiyo usikate tamaa, kama utakuwa umefanya biashara kwa miaka miwili ukaona biashara yako haifanikiwi, hapa unapaswa kujiuliza, je, nimefikisha masaa 10,000 tangu nimeanza biashara yangu? Kama masaa haya bado basi endelea kuweka juhudi.
Kiufupi ni kwamba, kama utatumia masaa 3  tu kwa siku kwenye biashara yako, basi itakuchukua miaka tisa na zaidi biashara yako kung’aa.
Kama unaweka masaa 5 tu kwenye biashara yako, basi itakuchukua takribani miaka sita ili kuifanikisha biashara yako ya kimataifa. Kwa hiyo usikate tamaa unapoona biashara yako haijafanikiwa kwa mwezi mmoja, endelea kuweka juhudi zaidi na zaidi kwa wakati huo huo maana muda mzuri wa kuifanikisha biashara yako unakuja.
2. Kanuni ya 80/20
Watu wengi wanaoanzisha biashara wanakazana kuuza kila kitu. Ila ukweli ni kwamba huwezi kuwa muuzaji wa kila kitu. Kanuni ya themanini-ishirini inasema hivi, asilimia 80 ya mauzo yako inatokana na asilimia 20 ya bidhaa zako. Ukiifahamu kanuni hii maana yake utawekeza nguvu zako na pesa zako kwenye bidhaa chache ambazo ni sawa na asilimia 20 ila zitakazokupa matokeo makubwa ambayo ni sawa na asilimia 80.
Je, wewe unajua bidhaa chache sana ambazo watu wanapenda kuja kununua kwako mara kwa mara? Hili zoezi unapaswa kulifanya sasa ili kujua asilimia 20 ya bidhaa zinazopendeka sana, ili zikuongezee kipato zaidi. Ukizijua hizi zitakusaidia pia katika kutangaza, maana bidhaa hizi utazitangaza zaidi, na watu watakuja kuzinunua zaidi.
3. Kanuni ya mshauri 
“Njia pekee  ya mkato na ya kufanikisha biashara haraka basi ni kuwa na mshauri”. Maneno haya aliyatamka Robert Greene ambaye ni mwandishi maarufu wa vitabu. 
Kadri ya Greene, ili uweze kupunguza muda wa wewe kufanya makosa basi unapaswa kuwa na mshauri ambaye amefanya kitu ambacho wewe unafanya au ana uelewa zaidi ya wewe kuhusu kitu unachofanya. Mshauri huyu atakusaidia kupunguza makosa mengi ambayo unegeyafanya kwenye biashara yako bila kujua. Mshauri huyu pia anaweza kukupunguzia masaa 10,000 ambayo tumeyaona hapo juu. Yaani badala ya kuchukua masaa 10,000 kufikia ndoto yako ya kuwa na biashara kubwa, basi itakuchukua  hata masaa pungufu ya hayo. 
Je, wewe unaye mshauri wa biashara yako? Mara ya mwisho umewasiliana naye lini? Alikwambia nini? Je, umeyafanyia kazi aliyokuambia?
Hizi ndizo kanuni muhimu sana ambazo ulikuwa huzijui kuhusu biashara na watu wengi huja kujifunza kanuni hizi hapa wakiwa wamechelewa sana maishani mwao. Na pengine kujikuta wameshabadili biashara wakifanya hii, wanakimbia tena kufanya ile n.k ila mwisho wa siku ukweli unabaki kwamba   kanuni hizi zipo pale pale maana wahenga wanatukumbusha kwa kusema kwamba, “kutokujua sheria sio ruksa ya kuvunja sheria”.
Uchambuzi wa Kitabu; SCREW IT, LETS DO IT

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA

KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X