Vitu Vitano Vinavyoharibu Ubunifu Wa Watanzania


Moja kati ya vitu muhimu sana katika biashara, mahusiano na kazi ni ubunifu. Ni kupitia ubunifu mtu unaweza kuja na mbinu mpya za kuongeza wateja, ni kupitia ubunifu unaweza kujua ni bidhaa gani ukiiboresha zaidi itakuongezea wateja zaidi. Ni kupitia ubunifu utajua ni bidhaa gani ukiipunguza  au ukiiondoa kwenye mfumo wako wa biashara utakuwa hujapungukiwa na kitu. Kwa hakika binafsi nauita ubunifu moyo wa biashara. 
Sasa ubunifu ni nini?
Mpaka hapa utakuwa unajiuliza huu ubunifu unaoongelewa ndio unafananaje? Ndio nini haswa?
Vyanzo mbali mbali vimeudadafua ubunifu kama matumizi ya njia bora zaidi zinazokidhi kutatua changamoto mpya, changamoto ambazo tayari zipo lakini hazijapatiwa ufumbuzi bado, au changamoto zilizopo kwenye soko au jamii kwa kipindi husika.
Hata hivyo kwa mantiki ya makala ya leo, tutatumia maana ifuatavyo UBUNIFU NI HALI YA KUJA NA WAZO JIPYA LA KUBORESHA, KUIMARISHA AU KUBADILISHA KITU KATIKA NAMNA YA UPEKEE.
Ubunifu katika biashara ni wa aina mbili. Kwanza kuna ubunifu mlalo na ubunifu sambamba.
Ubunifu mlalo ni aina ya ubunifu ambapo mtu unakuwa na kitu kimoja ila unakikuza kitu hicho hicho zaidi na zaidi. Mfano  mtu unagundua kwamba kalamu za aina fulani zinapendwa sana na watu katika eneo langu. Basi unaongeza uzalishaji wa kalamu za aina hiyo hiyo ili ziwe nyingi zaidi. Huu ndio unaitwa ubunifu mlalo.
Ubunifu sambamba. Huu ni ubunifu ambao unatokea pale unapokuwa unazalisha kitu kimoja ila ukagundua kwamba ili kitu hiki kifanye kazi vizuri basi hapa tunahitaji kitu kingine cha ziada. Kwa kutumia mfano wetu hapo juu. Unazalisha kalamu ila unagundua kwamba ili kalamu yako ifanye kazi vyema basi inahitaji daftari. Hivyo unaanza kuzalisha na daftari. Huu ndio  ubunifu sambamba. Ubunifu sambamba tunaweza kuuona katika maeneo mengi sana kwenye maisha yetu. Ukiangalia uwepo wa simu umesababisha uwepo wa laini za simu. Huu ni ubunifu sambamba. Uwepo wa viatu umezalisha uhitaji wa soksi huu nao ni ubunifu sambamba. 

Jinsi ya kutumia aina hizi mbili za ubunifu.
Bila shaka mpaka hapo utakuwa unajiuliza, hivi hizi aina mbili za ubunifu zitanisaidiaje kwenye biashara zangu?
Jibu ni rahisi sana. Kama kuna biashara yako unafanya sasa hivi. Angalia ni bidhaa gani inapendwa zaidi na watu. Ukishaipata bidhaa ya namna hii basi izalishe zaidi na hakikisha unaongeza mauzo. Kumbuka mapato makubwa sana kwenye biashara yako hayatoki kwenye kuuza kila kitu. Ila yanatokea kwenye kuuza bidhaa chache kwa wingi sana. Sasa hapa unahitaji kukaa chini na kujiuliza ni bidhaa gani hizi chache ambazo nikizizalisha kwa wingi zitaongeza mapato makubwa sana.
Au ni bidhaa gani nikiziongeza kwa wingi kwenye mzunguko bado nitazidi kuuza sana. Hapa utakuwa umetumia ubunifu mlalo.
Unaweza pia kutumia ubunifu wima kwa kuangalia  aina ya bidhaa ambayo ukiizalisha itakuwa inaendana  na ile ambayo ulikuwa hapo awali. Jiulize ni bidhaa gani inaweza kwenda sambamba na bidhaa ninayouza sasa hivi na ikauza vizuri bila shida? Mfano rahisi sana ni pale unapokuwa unauza majiko ya gesi. Unaweza kuongeza kitu cha ziada kwa kuuza vyombo vingine vinavyotumika jikoni. Ukiweza kuvijua vitu hivi vinavyoenda sambamba na na ile bidhaa ya awali baasi hapo utakuwa umetumia ubunifu sambamba.
Kwani kuna ulazima wa kutumia ubunifu kwenye biashara?
Zama zimebadilika, maisha nayo yamebadilika, lakini pia mfumo wa uendeshaji wa biashara umebadikika. Katika zama za sasa biashara zinazoendeshwa kibunifu ndizo biashara zinazopendwa na watu. Kwa hiyo ubunifu sio tena suala la hiari, ni lazima. Tungekuwa kwenye miaka ya 50 na 60 kabla uhuru ambapo maduka na wafanyabiashara walikuwa wachache sana, hapo suala la ubunifu tungeliweka pembeni na kushughulika na mambo mengine. Ila kwenye zama hizi hapa hakuna jinsi ubunifu ni lazima.
Lazima kuwepo na sababu za kwa nini watu waje kununua kwako na sio kwa rafiki yako mwenye duka na anauza bidhaa kama unazouza. Sasa hapo ubunifu ndipo unaingilia katikati. Kwa hiyo ubunifu ni lazima wala sio ombi?
Ubunifu ni muhimu kwenye biashara, michezo, sanaa, uigizaji, ufundishaji, mziki, upambaji n.k. yaani maisha na ubunifu ni vitu ambavyo hatuwezi kabisa kuvitenganisha 
Sasa kama ubunifu ni muhimu kwa nini watu sio wabunifu?
Mbali na kwamba tumeona ubunifu ni muhimu sana kwenye biashara na maisha ya kawaida bado ubunifu haujapewa kipaumbele hata kidogo kwenye bara la Afrika. Kuna watu wengi sana wamezaliwa na vipaji vikubwa sana vya kubuni na kuja na mbinu mpya ila bado hawajavitumia. Hizi hapa ni sababu zinazofanya watu wafanye vitu kwa namna ile ile kila siku bila kuongeza thamani za kibunifu.

1.  KILA MTU ANAFANYA HIVYO
Mara nyingi sana watu wapo katika mazingira ambayo kila kinachofanyika basi kinafanyika kwa namna ile ile tu. Yaani kwamba ameamka asubuhi, ameoga na kuzunguka  huku na kule, na kila mtu anafanya hivyo basi na yeye anaishi hivi. Maisha haya hayawezi kuzalisha wabunifu wakubwa. 
2. BABU ZETU WALIKUWA WANAFANYA HIVI
Hivi ushawahi kuthubutu kufanya kitu ukasikia mtu anakwambia “usifanye hivyo, babu zetu hawakuwahi kufanya kitu kama hicho”. Yaani watu wanatengeneza sheria zao wenyewe, wanazipitisha wao wenyewe na kutaka ziwe sheria za watu wote. Sasa kwamba baba au babu alikuwa anafanya vile ina athari gani na mimi nikifanya kwa namna nyingine. Maneno haya yanatumiwa sana na watu ila kiukweli ni kwamba hata hayajengi na hayana mantiki. Hivyo ni vyema kabisa kwa wewe kama wewe kujua kwamba tunapaswa kubuni na kuja na mbinu mpya za kibunifu kila wakati.  Kuendelea kufanya vitu kwa namna ile ile kila siku hakuwezi kukuinua na kutusogeza mbele Tanzania na Afrika nzima kiujumla. Nipo nafikiri kama  Albert Einstein angeendelea na fikra zile zile za mababu wetu walikuwa wanafanya hivi angeweza kugundua sheria MC²?
Hivi kama Mark Zuckerberg angeendelea kushikilia imani ya kwamba babu zetu walikuwa wanawasiliana hivi, angeweza kuja na mtandao wa kijamii wa facebook. Ebu watanzania badilikeni kabisa. Achana na mambo ya babu zetu walikuwa wanafanya hivi au vile. Sasa zama zimebadilika, maisha nayo yamebadilika hivyo na wewe unahitaji kubadilika, kubuni na kuja mbinu mpya zinazofanya kazi. Acha ya kale yaitwe ya kale ila sasa panga mambo mapya ya kibunifu.  
3. KELELE ZA DUNIA
Tunaishi kwenye dunia yenye kelele nyingi sana. Kuanzia asubuhi utasikia miziki inapigwa kila kona, magari yanapita kwenye maeneo yetu ya kazi, watu wanaongea na kupiga kelele. Yaani ni vurugu mechi. Bila ya mtu kuamua kuthubutu kujitenga na dunia kwa muda ili kutulia na kujitafakari basi maisha yataendelea hivi hivi tu. Kutokana na hali  hii basi hapa mtu unahitaji muda wa kupumzika, kujitenga na watu na kufikiri kwa kina juu ya maisha yako, biashara, mahusiano n.k hapa ndipo unaweza kuja na mawazo mapya ya kuendeleza na kuibua ubunifu wako
4. UOGA
Hivi watu watanichukuliaje? Hili ni swali lililo kwenye akili za watu walio wengi sana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mtu alikuwa amezoeleka kwa namna ya kawaida kwa watu na yeye tayari amehajijengea picha ya namna hiyo kama vile ni kweli. Ingawa sio. Huu uoga huu sio wa kuendekeza hata kidogo. Vijana wa Tanzania na Afrika, umefika wakati wa kuchukua hatua kubwa sana na kuhakikisha kwamba tunaibua ubunifu ulio ndani yetu.
5. UKOSEFU WA VIPAUMBELE
Watu wengi huwa hawana utaratibu wa kupangilia kazi wanapoamka asubuhi.  Hivyo kujikuta wanafanya kazi kwa mazoea. Kufanya kazi kwa mazoea hakuwezi kuleta ubunifu kazini. Hivyo wewe kama mbunifu unahitaji kutenga muda kidogo wa kuhakikisha unafanya kitu kwa kukiboresha zaidi na zaidi.
Usijifanye umebanwa kiasi kwamba huwezi kuangalia ni kitu gani bora zaidi unaweza kufanya ili kuboresha biashara au kitu chochoe unachofanya.
Na hili litawezekana kama utapangilia ratiba yako kila siku unapoamka.
Haya ndio mambo matano yanayoua ubunifu katika bara letu la Afrika na haswa Tanzania yetu. Ukiyaepuka haya rafiki yangu nina hakika utakuwa mbunifu mzuri kwenye eneo lako la kazi, biashara, michezo kutaja ila vichache.
Soma Zaidi; Vitu Viwili Vitakavyotokea Endapo Utakaa Usipopaswa Kuwa

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA

KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X