Mambo Matatu (03) Ambayo Vijana Wa Kitanzania Wanakosea ila Wanayafanya Kuwa Uhalisia


.

“Watanzania siku hizi mmeanza kuamka kidogo, kidogo. Ila bado itawachukua muda kidogo kuweza kufikia viwango vya watu kujituma bila kushurutishwa”
Alisema baba mmoja wa makamo ambaye ni mgeni hapa nchini.

Hongera sana rafiki yangu na leo hii napenda nikwambie mambo ambayo watanzania wengi wamekuwa wanayafanya kimakosa na kuendelea kurudiarudia makosa haya haya kila siku. Ma bado wanageuza makosa hayo yawe ukweli. Yaani wanahararisha uongo kuwa ukweli.

1. Kutojali muda. Kuna usemi kwamba hakuna haraka barani Afrika. Hadi kuna mtu ameandika kitabu kuzungumzia suala hili. Na usemi huu umekuwa unakumbatiwa sana na watu kama vile ni katiba ya Tanzania na Afrika. Hapa unapaswa kubadilika. Anza kujali sana. Unapokuwa na miadi jitahidi kuwahi.
Unapokuwa na kazi, ondoa usumbufu na wala usiruhusu maongezi yasiyo na maana.
Usiahirishe kazi ya leo kwa ajili ya kesho. Hivi ndivyo utaweza kuutumia muda wako vizuri kufanya mambo mazuri.

2. Kuzidisha ujamaa. Watanzania tuna ujamaa wa kiwango cha juu sana kiasi kwamba kizazi cha watoto wadogo wanakua wakijua kwamba maisha yao yote yataendeshwa kijamaa. Wanashindwa kujituma na kufanya kazi.
Unakuta kijana kahitimu chuo, baada ya hapo anaenda kwa mjomba kuwambia kwamba amehitimu Chuo. Na huko anamaliza mwezi mzima anakula na kunywa. Wala haambiwi kafanye kazi upate hela yako unitegemee. Utakuta yeye muda wote tu ni kuangalia tamthiliya na vitu vingine.

Baada ya mwezi kijana anahama na kwenda kwa bibi au shangazi. Huko anawaambia kwamba amehitimu na anatafuta kazi. Anakaa huko mwezi mwingine mzima akila na kunywa.

Kwa hiyo unakuta mtu wa namna hii anakua akijua kwamba maisha sio wajibu wake.
Ndio hawa huwa tunawasikia mitaani wanasema kwamba nikienda kwa mjomba huwa sitamani kutoka, maana pale kila kitu kipo. Vijana kuweni makini sana, ukiona vyaelea vimeundwa.

3. Kutojituma katika kazi. Vijana wengi wa kitanzania bila kusimamiwa kazi hazifanyiki. Na mwingine unakuta anakwambia kabisa kwamba mimi bila kusimamiwa basi kazi zangu zinakwama. Wewe hupaswi kuwa mtu wa namna hii. Unapaswa kuwa na moyo wa kujituma na ujitume kwelikweli.
Jisimamie wewe mwenyewe. Ukiweka malengo yako hakikisha kwamba unajisukuma ili uweze kuyafikia malengo yako ambayo umejiwekea.

Vijana wa kitanzania amkeni. Tanzania ya kesho inajengwa na mimi pamoja na wewe. Asante sana, tukutane kileleni.

Umekuwa nami,
Godius Rweyongeza
0755848391
KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA

HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA
KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X