Katika hatua fulani maisha watu huwa na ndoto za kufikia vitu au kuwa aina fulani ya maisha. Ndoto hizi huwa ni nyingi hasa kwa watoto maana huwa wanazisema kwa kujiamini kuliko watu wazima. Ndio maana ukiongea na mtoto mdogo na kumwuliza kwamba unataka kuwa nani basi bila ya shaka na bila kukwama sehemu atakuambia anataka kuwa daktari, nesi, rubani, mwanasheria n.k. wakati anakupa jibu hilo hakwami popote wala haogopi chochote.
Sasa swali hilo hilo ukimwuliza kijana utashangaa sana. Utasikia mwingine anakwambia kwamba wewe hiyo hapo inakuhusu nini. Au utasikia mwingine anasema kwamba nasubiri kitu fulani kitokee ndio nitajua. Kama ni mwanafunzi basi atakwambia kwamba nasubiri nifaulu mitihani ndio nitajua kinachoendelea. Mwingine atakwambia kwamba nasubiri serikali itangaze ajira ndio nitajua. Hii ndio kusema kwamba mtu huyu sio tu amepoteza ndoto yake bali pia kwa sasa hivi hajui ni wapi anaenda. Lakini mtu huyu huyu miaka ya nykazikidogo ndiye alikuwa na ndoto kubwa ya kuwa raisi, daktari au rubani. Sasa ni nini hiki ambacho huwa kinatokea na kuua ndoto za watu. Leo hii nimekuandalia vitu vitano ambavyo vinasababisha watu kuua ndoto zao. Vitu hivi vinaweza pia kuwa vimechangia kuua ndoto zako ambazo umekuwa nazo maishani mwako, pengine usipokuwa makini vitaua na ndoto zako za sasa hivi.
1. Watu wengine wamekuzuia kuwa na ndoto kubwa
Kuna watu wengi ambao kazi yao ni kuua ndoto za watu. Watu hawa wanaweza kuwa ni watu wa karibu yako. Au wanaweza kuwa wale ambao kwa hakika wanajua ukiweza kuifikia ndoto yako basi kitendo kama hicho kitawafanya wawe watu wa chini. Hivyo wanachofanya ni kukutatisha tamaa na kukuonesha kwamba haiwezekani kabisa kufanya wala kutimiza ndoto kama hiyvo hapo.
Na watu wanaoua ndoto zako wanaweza kuwa ni watu wa karibu yako. Wazazi, ndugu jamaa na marafiki ambao pengine wao walijaribu kufanya kitu wakawa wameanguka au waliwaona watu wengine wakifanya kitu hicho wakawa wameshindwa. Hivyo wanachukua hizo kumbukumbu na kuzileta kwako, kuonesha kwamba na wewe hutaweza, tena watu hawa watakuja na kila aina ya sababu ya kuonesha ni kwa namna gani huwezi, na pengine watakupigia hesabu za kuonesha kwa nini ndoto unayotaka kuifanya haitawezekana.
2. watu wengine wanaugulia maumivu ya nyuma au kukatishwa tamaa
Kukata tamaa na maumivu ni uhalisia kati kile ambacho unategemea na ukweli. Kila unayemowna amefikia mafanikio makubwa sana maishani basi ujue kwamba amepitia hali kama hii hapa. Na kuna nyakati maumivu yanaweza kuwa mazito kiasi cha kukufanya wewe upoteze matumaini uliyokuwa nayo. Hata hivyo unapaswa kuchukua somo na maumivu ambayo unakutana nayo kwa wakati husika. Maana siku zote matatizo huwa sio tatizo, bali fursa ya wewe kusonga mbele ya kufanya makubwa zaidi ya hapo.
Usipojifunza kutokana na matatizo basi utakuwa kama paka ambaye akikaa kwenye jiko la moto likamuunguza basi hatakaa tena kwenye jiko hilo hata kama ni la baridi. Siku zote chukua somo kutokana na changamoto ambazo unakutna nazo kasha songambele.
Kamwe usije ukajiambia kwamba sitarudia kufanya kitu hiki baada ya kuwa umeshindwa. Hilo hapo ni kosa kubwa kwa ndoto zako. Ni ukweli kwamba utashindwa mara kwa mara kabla ya kufikia ndoto zako ila usiache kuendelea na safari ya kutimiza ndoto yako. Ndio maana aliyekuwa waziri mkuu wa uingererza Magreth thatcher amewahi kusema, kuna nyakati utapaswa kupigana vita zaidi ya mara moja ili kushinda. Kwa hiyo wewe kila mara chukua somo ujifunze na usonge mbele.
3.kuna watu wanatulia na ukawaida
Kuna watu wanaamua tu kutulia na kile walichonacho. Ila cha kufahamu ni kwamba unapoamua kutulia na kile ulichonacho, hata kile ulichokuwa nacho kinaanza kupungua. Ni katika nykati kama hizi hapa utajikuta unaanza kuilalamikia serikali, wazazi au watu ambao wewe utawachaggua kuwalalamikia.
Kama kweli kwa sasa unajua kwamba unaishi maisha ya kawaida na umetulia basi amua sasa kuanza kufikiri tofauti. Kumbuka kwamba uwezo wako ni mkubwa na hhivyo unapaswa kuutumia. Ukitulia na kuridhika na hali ya sasa unakuwa umeamua kuuzika uwezo wako kaburini. Tunaweza kusema kwamba unakuwa na sawa na mtu ambaye anachukua meli kubwa ambayo imetenegezwa ili kusafirisha watu na mizigo kwenye maji makubwa ya bahari, sasa meli hii inawekwa kwenye kijito kidogo tu. Huhitaji mtu wa kukwambia kwamba hapo sio mahala pake. Na wewe hivyo hivyo, ukitulia na hali ya sasa unajjikwamisha.
Kuna shida gani katika kutulia na kuridhika?
Hili hapa ndilo linaweza kuwa ni swali lako ambalo unajiuliza. Ngoja ni kwambie kitu. Vitu vilivyotulia ndivyo huja na madhara makubwa. Mbu huzaliana kwa wingi kwenye maji yaliyotulia na kutuama. Hata konokono wanaoeneza magonjwa wanakutwa sehemu kama hizi zilizotulia. Yaani naweza kusema kwamba kila kitu ambacho kinakaa kwa muda mrefu kimetulia kinaoza, hata mdomo ukikaa muda mrefu umetulia unaanza kutoa harufu. Unaona sasa, kumbe ni wakati wako wako wewe kuhakikisha sasa hautulii tu kuridhika na hali ya sasa. Kwa sababu unaweza kufika mbali zaidi ya hapo na unaweza kuwa zaidi ya ulivyo sasa hivi kama utaammua kuzifanyia kazi ndoto yako.
4. watu wengine wanakosa ujasiri unaotakiwa ili kuzifikia ndoto zao,
Ni ukweli kwamba ndoto huwa ni kubwa. Lakini pia huwa zinahitaji muda ili kuweza kuzifikia ndoto hizi. Cha ajabu zaidi kuhusu ndoto ni kwamba wewe ndiwe unakuwa unaona kule unapoenda ila wengine hawapaoni. Pia wewe ndiwe unakuwa unajua ni wapi unaenda na kwa nini unaenda huko ila wengine ndio kwanza wanakushangaa. Sasa katika nyakati kama hizi hapa unahitaji ujasiri mkubwa kuendelea kuifanyia kazi ndoto yako kila siku hata kama watu wengine wote watabaki u kukucheka, kukutania na kukutukana. Inahitaji ujasiri mkubwa. Kadri unavyokuwa na ujasiri wa kuiongelea ndoto yako ndivyo unakuwa pia na ujasiri wa kuifanyia kazi na kuifikia.
5. kuna watu wanakosa fikra za kuota ndoto kubwa.
Hivi watu huwa wanaanzaje kuwa na ndoto kubwa? Hili ni swali ambalo pia tunapaswa kujiuliza na kulitafutia majibu yake kwa kina. Nakumbuka mvumbuzi Thomas Edison akiwa na umri wa miaka 21 alisema kwamba “ningependa kutumia maisha yangu nikiwa navumbua vitu. Kuna vitu vingi sana vya kufanya na ninaaweza kufa kabla sijafikia hatua kubwa, hivyo nitatumia muda mwingi kuhakikisha kwamba navumbua hivyo vitu”. Kwa hiyo yeye ndoto ya maisha yake ikawa ni kuwa mvumbuzi. Na unaweza kuona hapo kilichofanyika ni kwamba alianza kuwa na fikra juu ya kitu ambacho angekifanya ili kufanya thamani na maisha ya watu kuwa bora zaidi.
Kama kuna kitu kimoja ambacho utapaswa kuhakikisha unakifanyia kazi basi ni kuwa ndoto kubwa ya maisha yako.
Rafiki yangu hivi ni vitu ambavyo vinawazuia watu walio wengi kuweza kufikia ndoto za maisha yao. Hivi ni vitu ambavyo vimekuwa vikikuwamisha pia na wewe. Sasa ni wakati wako kuhakikisha kwamba unasonga mbele na kufanya makubwa zaidi. Hakikisha kwamba unakuwa na ndoto na uifanyie kazi
2 responses to “Vitu vitano vinavyofanya watu waue ndoto zao na hivyo kushindwa kuzifikia”
Ni kweli kabisa God nimejifunza kitu hapo
Nimetumia Eid yangu kuzikalia, kuzisoma vizuri,kusummarize na kuweka action plan kwenye hizi makala. Asante kaka Godius they are helpful