Kuna misemo ambayo imezoeleka kutolewa na watu siku hizi kiasi kwamba imekuwa ni sehemu ya pili ya maisha ya hawa watu. Unakuta mtu anasema “usawa huu wa Magufuri pesa imekuwa ngumu sana”. Utasikia mwingine anasema “vyuma vimekaza” wakati mwingine akitaka kukwambia kuwa hana pesa basi utasikia akisema, “sina hata mia mbovu”. Yaani kumaanisha kuwa hana kitu kabisa mfukoni mwake.
Ukifuatilia kwa umakini. Yaani kwa jicho la tai anayeuangalia mchezo kutokea juu angani na kutoa tathimini, unaona wazi kabisa kuwa suala la vyuma kukaza sio jambo la leo au jana. Historia inaonesha kuwa katika kila nyakati kumekuwa na mambo kadha wa kadha ambayo yamekuwa yakitokea na kusababisha vyuma kukaza. Hata hivyo kitu kimoja kimebaki uhakika siku zote. Wale wanaotengeneza pesa siku zote huwa hawaoni kukaza kwa vyuma Kama tatizo. Badala yake huwa wanaona fursa kwenye hilo.
Ngoja nikueleze kiundani suala hili ili uweze kunielewa. Kukaza kwa vyuma kama wanavyosema wengine maana yake Ni kutokuwepo kwa pesa. Sasa tujiulize ni kitu gani kinakufanya wewe ukose pesa? Unaweza kuwalalamikia watu wote duniani Ila mwisho wa siku mtu anayesababisha kukaza kwa vyuma ni mmoja tu. Na mtu huyu ni wewe. Hii unatokana na ukweli kwamba pesa inafuata mkondo kwa wale wanaoiita. Kama wewe hauiiti ije kwako haiwezi kuja, utapishana nayo njiani tu.
Leo hii nataka nikuoneshe namna utakavyoiita pesa ije kwako na uendelee kuwa ya kwako milele na milele. Siku nyingine kabla hujasema pesa ni ngumu hakikisha unarudi hapa kusoma andiko hili ili uone Kama umelitendea haki. Ila kama utasoma hapa na kuishia tu kusema kuwa huyu jamaa anaandika vizuri basi mimi nakuhakikishia utaendelea kusema kuwa pesa ni ngumu. Kama utasoma hapa na kufanyia kazi ulichojifunza hapa, basi tutakutana sehemu siku moja ukifurahi kwa sababu ya kile ukichojifunza hapa siku ya leo.
MOJA, KAMA PESA NI NGUMU MAANA YAKE HUJATOA HUDUMA KWA JAMII
Zig Ziglar amewahi kusema kuwa utapata kitu chochote unachotaka kama utawasaidia watu kiasi cha kutosha kupata kile wanachokitaka. Kitu ambacho unapaswa kuelewa hapa ni kuwa kuna watu wananpesa zako mkononi mwao. Ila hizo pesa hazitakuja kwako kirahisi. Labda uwakabe (na ukifanya hivyo jela itakuwa rafiki yako). Ila njia pekee ya kuzitoa hizo pesa kwa watu na kuzileta kwako ni kuhakikisha kuwa una bidhaa ambayo unaweza kuwauzia hao watu. Hiki kitu ndicho Zig Ziglar anakiita kuwasaidia watu kupata WANACHOTAKA.
Kuna watu wanahangaika kwa sababu huduma fulani hawaipati vizuri. Lakini wewe ukiweza kuwafikishia hiyo huduma kwa ustadi watakuwa tayari kukulipa na hiki ndicho Zig Ziglar anakiita kuwasaidia watu kupata WANACHOTAKA.
Kuna watu hawajui kwamba wewe ni mtaalamu na umesomea ujuzi fulani chuoni. Sasa huo ujuzi ulilojifunza chuoni ukiweza kuutafsiri na kuuleta kwenye maisha yabm kawaida hapa mtaani. Ukautumia ujuzi huo kuwasaidia watu kupata kitu fulani ambacho unaona kitaalamu hakifanyiki vizuri. Hapo utakuwa umewasaidia watu kupata kitu wanachokitaka.
Nikukumbushe kuwa pesa hazitakuja kwako Kama wewe utakuwa tu umelala afu unaishia kusema pesa ni ngumu au vyuma vimekaza. Pesa itakuja kwako pale ambapo utaamua kutatua matatizo ambayo jamii inakumbana nayo.
Muuza maji hapati pesa kwa kuuza maji bali kwa kutatua tatizo lako la kiu.
Mtu daladala hapati pesa kusafirisha abiria, bali kwa kutatua tatizo lako la kusafiri na kufika eneo husika mapema.
Mitandao ya simu haipati pesa kwa kuuza vocha bali kwa kuunganisha na watu walio mbali na wewe.
Wewe unatatua tatizo gani?
Shida yako wewe imelala kwenye haya maeneo mawili.
Kwanza unaamini kuwa hakuna kitu kingine kipya unaweza kufanya kuondokana na hali hiyo uliyonayo. Yaani umejikatia tamaa mwenyewe. Nan kama umekata tamaa mwenyewe hata akitokea mtu akakupa mamilioni ya pesa hayatakusaidia. Cha kufanya inuka tena anza tena kupambana.
Tatizo lako la pili, unaona kuwa haya ninavyoongea hapa yanawafaa wengine na sio wewe. Huchukui hata hatua ya kuanza, unabaki kusema tu haya yanawafaa watu wenye hela zao bana. Hivi unadhami hao unaosema wana hela zao walizaliwa nazo? Kuna wengine walikuwa na maisha mabaya pengine zaidi ya wewe. Kuna wengine walikuwa na madeni makubwa kuliko hata wewe hapo. Ila walisimama wabeba majukumu yao na Sasa unawaonea gere. Usipochukua hatua UTAJIJU.
2. KAMA PESA NI NGUMU MAANA YAKE UNAWAHUDUMIA WATU KIDOGO
Kiasi cha pesa unachoingiza kinaweza kuniambia ni idadi gani ya watu unaowahudumia. Kama unaingiza pesa kidogo maana yake UNAWAHUDUMIA WATU KIDOGO. Kama Kuna kiasi kikubwa unaingiza maana yake unawahudumia watu wengi. Hii wala hata sio hesabu ngumu kama unavyofikiria.
Ebu tuseme wewe na Paulo mnauza maji. Paulo anawauzia watu 1000 na wewe unawauzia watu 100 kila siku na kipimo mnachitumia kuuza Ni kile kile unadahami atapata pesa zaidi?
Ukiona pesa ni ngumu unapaswa kujua kuwa unawahudumia watu kidogo. Kama umeajiriwa ujue unafanya biashara na mteja mmoja tu ambaye Ni bosi wako. Sasa usitegemee ulipwe kwa viwango sawa na mtu ambaye anatoa huduma kwa wateja mia, elfu au laki moja.
3. KAMA PESA NI NGUMU UJUE KUWA HUJAJUA MISINGI NA MIIKO YA PESA.
Ni kawaida kuwa mwanasheria akienda chuoni lazima atafundishwa misingi ya sheria na miiko kwenye sheria. Daktari pia anafundushwa misingi na miiko. Mwajiriwa kazini ataambiwa Mambo anayopaswa kufanya kazini na yale anayopaswa kuepuka. Pesa pia ina misingi yake na miiko yake. Ukiona ni ngumu kwako basi ujue hii misingi hujaijua.
Hujajua kuwa unapaswa kuweka akiba kwa kila kiasi unachopata
Hujajua pia kuwa unapaswa kupunguza matumizi yako na kubaki na mtumizi ya lazima tu.
Hujajua kuwa unapaswa kuanza kuwekeza ili pesa yako ikuzalie pesa zaidi.
Hujajua kuwa haupaswi kutumia zaidi ya kipato chako.
Hujajua pia kuwa haupaswi kukopa pesa ili utumie ili uje ulipe.
Hujajua pia kuwa mtu akikuahidi pesa, haupaswi kuiweka kwenye hesabu zako mpaka utakapokuwa umeipokea mikononi mwako.
Hiyo ndio misingi ya pesa miiko ya pesa.
HITIMISHO.
Naamini baada ya kuwa umesoma hapa, hutakuja kukosa mia mbovu kuanzia leo. Maana tayari unajua jinsi pesa inavyopatikana mpaka inavyotumika. Nikutakie kila la kheri.
Makala hii imeandikwa na Godius Rweyongeza
Unaweza kuwasiliana naye kupitia 075584891
2 responses to “Kama Hauna Hata Mia Mbovu Jua Unakosea Hapa”
[…] SOMA ZAIDI: Kama Hauna Hata Mia Mbovu Jua Unakosea Hapa […]
[…] “vyuma vimekaza” wakati mwingine akitaka kukwambia kuwa hana pesa basi utasikia akisema, “sina hata mia mbovu“. Yaani kumaanisha kuwa hana kitu kabisa mfukoni […]