Ukitaka kutuma ujumbe mfupi kwa rafiki yako, huwezi kuandika herufi zote za kishwahili kuanzia A mpaka Z na kumwacha rafiki yako ajitugie ujumbe mwenyewe. Au huwezi kuandika maneno tu kutoka kwenye kamusi bila mpangilio maalumu na kutuma kama ujumbe.
Ni lazima utatengeneza sentensi inayoeleweka na kuituma ili aisome na kukupa jibu kulingana na sentensi uliyotuma. Na hiyo sentensi inayoeleweka unayotuma kwa rafiki yako ndiyo inaitwa UJUMBE.
Rafiki yangu, leo naomba ukae vizuri na uvute pumzi kwa nguvu maana hapa tunaenda kuongea mambo makuu na kuona kosa ambalo umekuwa unafanya siku zote. Lakini sitakuacha hivi hivi. Mwisho kabisa nitakupa suluhisho la kosa hili ambalo umekuwa unafanya.
Bila shaka utakuwa umeona wazi kuwa kutuma herufi A mpaka Z kwa rafiki yako kama ujumbe ni kitu cha kijinga ambacho huwezi kufanya. Na kama mtu atakutumia ujumbe wa aina hiyo wewe, ni wazi kwamba hawezi kupata kitu anachotaka kutoka kwako. tuseme kwamba rafiki yako anataka wikendi hii mtoke kidogo na kwenda ufukweni kutembea. Ila rafiki huyo anakuandikia hivi, B, G, W,K, Z, S,Q,A,P,M, N,B,V,C,X,Z. Wewe utajibu nini? ni wazi kwamba hawezi kupata anachotaka kutoka kwako.
Lakini kitu hiki hapa ndicho umekuwa unafanya kila siku rafiki yangu. Yaani kila siku, kila wiki, kila mwezi na kila mwaka. Na kosa hili hapa ndilo limekufikisha hapo ulipo sasa hivi. Kosa hili ndilo limekukfanya upate hali hiyo, iwe ni kushindwa kutimiza malengo yako, madeni, kukosa furaha na kazi unayofanya, kushindwa kuanza biashara, kushindwa kufanya hicho kitu ulichokuwa unapenda kufanya kwa siku nyingi kama kuandika n.k.
Hili ni kosa la kutokuweka wazi kitu ambacho wewe utafikia. Yaani haujui nini haswa unachotaka. Ni wazi kuwa, kama haujui unapokwenda basi kila njia itakupeleka. Vivyo hivyo wewe kama haujui wapi unaelekea na maisha yako, basi kila kitu kitakachotokea kitakuwa sahihi kwako.
Hivi kwa mfano nikikuuuliza unataka kuwa wapi baada ya miaka 5, 10 au 20 ijayo unaweza kuniambia? Na kwa nini unataka kwenda huko?
Watu wengi hawapati kile wanachotaka kwa sababu hawajui kitu wanachohitaji. Hivyo sasa
HATUA YA KWANZA YA wewe kupata kitu chochote unachotaka ni kujua hicho kitu ni kipi. Hii ndio kusema kwamba unapaswa kuwa na picha ya hicho kitu ambacho unataka.
Mfano unakuwa na picha kwenye akili yako ya kuwa baba bora kuliko wote duniani, unakuwa na picha ya kuwa mwandishi bora na muuzaji bora wa vitabu, unakuwa picha kutengeneza utajiri wa milioni tano, unakuwa na picha ya kuwa daktari n.k.
HATUA YA PILI ni kuiweka hiyo picha kwenye maneno yanayoelewa ikiwa ni pamoja na kuiwekea ukomo wa muda ambapo utakuwa umeifikia. Ikumbukwe kwamba kwenye hatua ya kwanza, ulijenga hiyo picha kwenye akili yako. Lakini sasa unaandika chini kabisa kitu ambacho utafikia na muda wa kukifikia.
Mfano unaweza kuandika; mimi…..kufikia….ninamiliki…
Kama umeona vizuri, hapo juu nimetumia neno NINAMILIKI. Hii inakufanya uone kwamba hicho kitu umekifia tayari, hata pale ambapo unakuwa bado hujafikia hicho kitu
HATUA YA TATU, ni kuwa na imani isiyoyumbishwa kwamba unafikia hicho kitu. Tatizo la watu wengi ni kwamba leo asubuhi anaweza kusema hiki, baadae kidogo akasema kingine kinachopingana na hicho, baadae akasema kingine cha tofauti. Yaani anakuwa haeleweki ni kutu gani kinapaswa kuja kwake.
Wewe hapo unapaswa kusema na kuwa na kitu kimoja na kushikilia hicho. hakikisha kwamba hausemi wala kusikiliza watu ambao wanasema kitu ambacho kinapingana na kile ambacho wewe umeamua kufanya.
HATUA YA NNE; nenda weka mpango wa kufikia hicho ambacho umeandika. Ni kweli unataka kuwa mwandishi bora, lakini je utafikaje huko? Ni gharama gani ambayo utalipa ili kuufikia huo ubora. Ni kitu gani utatoa ili kupokea hicho unachotaka wewe? Hapo, sasa ndipo unaorodhesha hatua ambazo utachukua. Unakuwa na melengo ya mwaka, malengo ya kila mwezi, malengo ya kila wiki mpaka malengo ya siku.
HATUA YA TANO; FANYIA KAZI MPANGO WAKO
Wazungu wana usemi wao kuwa actions speak louder than words. Wakimaanisha kuwa matendo huongea zaidi ya maneno. Hivyo nenda kafanyie mpango wako kazi ili uweze kupata matokeo ambayo unataka. Matendo yako yaongee zaidi ya maneno yako unayoongea.
HATUA YA SITA, PIMA MWENENDO WAKO
Kuna watu ni wazuri wa kuanzisha vitu ila sio waendelezaji wa hivyo vitu. Na kuna mtu anaweza kufanya kazi wiki nzima ila hawezi kutoa dakika 20 tu kwa ajili ya kujihoji kuona ni wapi ametoka, yuko wapi na wapi anaenda. Huwa inatokea mara nyingi tu, unakuta watu wanajadili maisha ya watu na kuona kwamba mtu angeweza kufanya hivi au kufanya vile ili kuweza kupata kitu fulani. Ila wao wenyewe hawajui wafanye nini na maisha yao. Sijui nimekugusa na wewe. Hahah
KWA HIYO kuwa na nguvu ya kufuatilia maisha yako, kujua kwamba ni kitu gani unapaswakufanya na maisha yako, kuliko kuwekeza kuwajua watu wengine.
HATUA YA SABA, JIFUNZE.
Kama kuna kitu utahitaji kufanya mara kwa mara ni kujifunza na kufanyia kazi vile vitu ambavyo unajifunza. Na unaweza kujifunza kutoka vitabuni, kutoka kwa watu, kutokana na mazingira n.k.
Rafiki yangu, kwa kufanya hivi unakuwa umeondokana na hilio kosa la kuandika barua yenye herufi peke yake. Badala yake sasa unauwa umeandika ujumbe wenye sentensi inayoeleweka na sentensi hiyo inaenda kujibiwa na wewe utapata matokeo chanya.
Nina neno moja la mwisho kwako wewe. Na neno hili hapa ni kwamba ACHA KUANDIKA UJUMBE WENYE HERUFI ZISIZOPANGILIWA.
Sura ya pili kwenye kitabu cha kutoka sifuri mpaka kileleni, itakufundisha vizuri sana kuhusiana na haya masula ya kuweka malengo na hatua za kufuata ili kuweza kuyafikia. PATA NAKALA YAKO YA BURE SIKU YA LEO kwa KUBONYEZA HAPA.
Kamautakuwa na swali, usisite kuaniandikia (kutuma ujumbe) kwenda 0755848391 (whatsapp tu)
Au barua pepe, songambele.smb@gmail.com