Usishindane Kwa Bei Labda Kama Wewe Ni Rockefeller. Vitu Sita Ambavyo Vinaweza Kukufanya Uwe Wa Kipekee Kwenye Soko Bila Kupunguza Bei


 

Kwa sasa hivi dunia ina mabilionea zaidi ya elfu 2. Hata hivyo,h haikuwa hivo mwanzoni mwa karne ya 19 ambapo mamilionea tu walikuwa wanahesabika, sasa mabilionea ndio walikuwa wachache kabisa kulinganisha na zama hizi hapa ambapo mabilionea wanaongezeka kila mwaka.

Kipindi hicho Rockefeller aliibuka kuwa mtu mwenye fedha nyingi sana kuliko mtu yeyote aliyekuwa anaishi kwenye huu uso wa dunia. Rockefeller alikuwa anajihusisha na biashara ya mafuta.  Alichofanya Rockefeller baada ya kuwa fedha nyingi, ilikuwa ni kupunguza bei ya mafuta kiasi kwamba wanunuaji wote wa mafuta wakawa wanaenda kwake na washindani wake wakawa wanashindwa kuuza. Tuseme kwa mfano kama sasa hivi lita moja inavyouzwa kati ya elfu moja mia nane mpaka elfu moja mia tisa. Basi Rockefeller angeuza kwa elfu moja au hata mia tisa! Kitu hiki kiliwafanya washindani wake wauze biashara zao maana walikuwa hawapati faida yoyote na mtu waliyekuwa wanamwuzia biashara zao alikuwa ni Rockefeller mwenyewe. Hali iliendelea hivi kwa siku nyingi kiasi kwamba makampuni yote ya mafuta yakawa yameuzwa na yote aliyanunua Rockeffeller mwenyewe.

 

Sasa labda unaweza kujiuliza, kwa kuuza kwa bei ya chini Rockefeller alikuwa anapata faida? Jibu ni HAPANA. Tena hapana ya herufi kubwa. Ila ukweli ni kwamba alikuwa anauza mafuta kwa hasara sema kwa sababu alikuwa na fedha alikuwa bado na uwezo wa kuendesha bishara zake bila shida yoyote. 

Lengo lake lilikuwa ni kuyanunua makampuni mengine ya mafuta na kuyaweka chini ya himaya yake. Lakini kitu kingine alichofanya Rockefeller kwa sababu alikuwa na fedha alinunua reli zote muhimu zilizokuwa zinatumika kusafirishia mafuta. Na reli ndio ulikuwa usafiri wa uhakika wa kusafirisha mafuta kutoka eneo moja kwenda jingine. Baada ya kununua reli alipandisha kodi kwa makampuni mengine yaliyokuwa yanasafirisha mafuta kupitia reli zake. Hivyo, kitu hicho kikawasukuma zaidi wamiliki wengine wa makampuni  kuuza makampuni yao.

 

Kilichotokea baada ya yeye kuwa amenunua makampuni yote, ikawa sasa yeye ndiye anazalisha mafuta na yeye ndiye anauza mafuta peke yake. 

Hivyo, aliamua kuuza mafuta kwa bei aliyokuwa anataka yeye na kuanza kurudisha hata ile hasara aliyoipata kipinda anauza mafuta kwa bei ya chini.

 

Sasa sidhani kama wewe una fedha za kutosha kama za Rockefeller kiasi kwamba upunguze bei kwa kiwango cha chini kulinganisha na washindani wako kwa muda mrefu mpaka watakapokuwa wameshindwa kuendesha biashara zao na kuziuza kwako, ndio maana leo hii napenda nikwambie kwamba ushindane na watu kwa bei labda tu kama wewe ni Rockefeller. Na hapa kuna vitu vitano ambavyo unaweza kufanya:

 

HAKIKISHA KWAMBA UNAKUWA NA HUDUMA BORA.

 

Hiki ni kitu cha kwanza kabisa ambacho unahitaji kuhakikisha kwamba unakuwa nacho. Hakikisha kwamba mteja wako anapokuja kwenye biashara yako basi anapata mapokezi ya kifalme. Hakuna haja ya mteja kufika kwenye biashara yako na ikawa kama vile amepotea njia. Tena ukiweza kabisa unaweza kuwa na kitengo cha huduma kwa wateja au mapokezi ambapo mteja wako atapokelewa kifalme na kama kuna kitu au maswali anayo basi anaanza kuhudumiwa hapohapo kwa ukarimu wa hali ya juu. Wape watu wako huduma ambayo hawawezi kuipata pengine.

 

HAKIKISHA UNAKUWA NA HUDUMA YA UHAKIKA

 

Siku hizi kuna biashara nyingi zinafanyika kupitia mitandaoni, hivyo kitu kimoja ambacho mteja wako angependa kujua na kupata ni huduma ya uhakika. Hakikisha kwamba unatoa huduma ya uhakika. Sio unapata fedha halafu huduma hamna au wewe mwenyewe unapotea kabisa.

Lakini bado hata kama biashara yako siyo ya mtandaoni, mteja anahitaji uhakika wa kupata huduma. Kwa hiyo anahitaji uhakika muda (akija muda wowote anakukukuta)

Anahitaji pia uhakika wa bidhaa, ana uwezo kuzipata muda wowote ule atakapokuja na

Uhakika wa huduma. So leo anahudumiwa vizuri halafu kesho anapata huduma mbovu kuliko zote duniani.

 

HAKIKISHA UNAKUWA NA HUDUMA YA HARAKA

 

Siku hizi hakuna mtu anayependa kupata huduma kwa kuchelewa. ndio maana utasikia vitu kama intaneti yenye kasi, magari ya mwendokasi…yaani, kiufupi ni kwamba huduma ya haraka ndio huduma inayohitajika kwenye zama hizi. Kwa hiyo, kama kuna kitu unaweza kuwapa watu wako basi ni huduma ya haraka. Na kitu hiki kitakutofautisha na watu wengine bila ya wewe kuathiri bei zako.

 

TAFUTA NAMNA UNAVYOWEZA KUWAFIKISHIA WATEJA WAKO HUDUMA WANAYOTAKA

 

SIKU hizi moja ya kitu kinachofanyika sana ni kuwafikishia wateja huduma husika mlangoni. Hiki ni kitu kidogo ila chenye nguvu kubwa sana na wewe unaweza kufanya kitu kama hiki pia

 

ONGEA NA WATEJA WAKO KUJUA HUDUMA WANAOIPATA KWA WASHINDANI WAKO, KISHA IWEKE HUDUMA HIYO KWENYE BIASHARA YAKO

 

Kama kuna huduma ambayo wateja wako wanaipata kwa mwingine ila kwako haipo na hivyo kusababisha wateja hao waondoke kwenye biashara yako, basi unaweza kuongea nao na kuwauliza kuhusu huduma ambayo wanapata huko pengine na kisha kuhakikisha kwamba hiyo huduma uaileta pia kwenye biashaar yako.

 

TUNZA KUMBUKUMBU NA MAWASILIANO YA WATEJA KILA WANAPOKUJA KWENYE BIASHARA YAKO

 

Hizi kumbukumbu zitakusaidia wewe kuweza kuwasiliana nao hata baada ya wao kuondaka. Kitu hiki kitawafanya wateja wako wajue kwamba wewe sio mtu wa fedha peke yake muda wote lakini pia unakuwa unawajulia hali pia. Au kama una mafunzo mazuri ambayo unaona yanawasaweza kuwasaidia basi unawatumia.

Lakini pia kitu kingine ni kwamba unaweza kutumia mawasiliano haya kuhakikisha kwamba unawaambia wateja wako juu ya bidhaa zako na huduma mpya ambazo zinaendelea kuja kwenye biashara yako.

 

 

Rafiki yangu hivyo, ni vitu ambavyo unaweza kufanya kabisa hata kama hauna fedha nyingi kama alizokuwa nazo Rockefeller. Ni imani yangu kuwa umejifunza mengi hapa ambayo unaenda kuyafanyia kazi. kila la kheri


Umekuwa nami rafiki yako wa ukweli Godius Rweyongeza

Hakikisha Umesubcribe kwenye Channel yangu ya youtube kwa KUBONYEZA HAPA

Jiunge na mfumo wa kupokea makala maalumu kwa njia ya barua pepe kwa KUBONYEZA HAPA

Jipatie nakala za vitabu vyangu vya kiswahili kwa KUBONYEZA HAPA

Kama ungependa kujifunza kuhusu uandishi kutoka kwangu wasiliana nami kwa 0755848391

Kupata blogu yako ya kitalaam tuwasiliane kwa 0755848391

kila la kheri


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X