Madeni ni moja ya kitu ambacho kinawasumbua watu wengi na hivyo kuwafanya washindwe kuwa na uhuru lakini hapohapo kuwanyima mwanya wa kuufikia uhuru wa kifedha. Sasa ukweli ni kwamba, inawezekana wewe hapo kuufikia uhuru wa kifedha na kuondokana na madeni.
Vifuatavyo ni vitu muhimu vya kufanya ili uweze kuondokana na madeni.
Kwanza orodhesha madeni yako yote. Makubwa kwa madogo. Yaorodheshe hata kama ni mengi. Hata kama Kuna mtu ulishapanga kumdhurumu mweke kwenye hii orodha.
Pili, tenga asilimia 20 kutoka kwenye kila fedha unayopata kwa ajili ya kulipa madeni. Wakati huohuo usisahau kuweka akiba asilimia 10 tu. Hiyo asilimia 70 iliyobaki ndiyo unapaswa kutumia. Kwa kipindi hiki unapaswa kupunguza matumizi yako yote makubwa na kubaki na matumizi yale ya lazima tu (Yale ambayo endapo hutayafanya utakufa). Jipange kuachana na anasa katika kipindi hiki hapa.
Tatu, pangilia namna ya kuwalipa wadeni wako wote. Unaweza kuanza kuwalipa watu wanaokudai fedha kidogo, kisha ukaenda kuwalipa wale wanaokudai fedha nyingi. Au unaweza kuanza ma fedha nyingi ukamalizia na wa kidogo japo ukianza na wale wenye madeni kidogo inakupa hamasa ya kuedelea kwa kuwa unakuwa unapunguza orodha ndefu ya wanaokudai na kubaki na watu kidogo. Pia kama Kuna wadeni wasumbufu Basi unaweza kuanza kuwalipa hao ili waache kukusumbua
Nne, Kila unapomaliza kumlipa mtu mfute kwenye daftari au karatasi yako ili wabaki wale ambao ulikuwa hujawalipa tu. Hii itakupa hamasa ya kusonga mbele.
Tano, weka mkakati wa kuongeza kipato chako. Kinachofanya watu wengi waingie kwenye madeni ni kwa sababu kipato hakikidhi mahitaji. Au wengine ni kwa sababu wanapenda vitu vizuri kama gari, nyumba n.k. ila hawana fedha ya kuvilipia. Sasa unapaswa kuweka mpango wa kuongeza kipato chako ili kuondokana na madeni kabisa. Njia ya wewe kuongeza kipato chako ni kuanzisha walau kibiashara kitakachoanza kukuingizia kipato hata kama ni kidogo.
Sita, katika kipindi hiki ni marufuku kukopa tena. Jikite katika lengo lako na kuondokana na madeni hata kama litachukua muda mrefu kulitimiza.
Kila la kheri