Fursa zimejificha kwenye matatizo. Matatizo yaliyo kwenye jamii ukiyatatua ni fursa. Hivyo, kaa uangalie jamii yako ina matatizo gani, kisha angalia namna ya kuyatatua hayo matatizo .
Siku siyo nyingi tulikuwa kwenye mlipuko wa ugonjwa UVIKO. Kuna watu mlipuko huu umekuwa fursa kwao wakati wengine umekuwa janga kubwa kwao. Kuna watu waliweza kufanya vitu na kubuni vitu vya kipekee ila wakati huohuo Kuna watu wamejinyonga na kufa. Kuna watu wamepata ajira na kuna watu wamepoteza ajira. Haya yote yametokea ndani ya kipindi hikihiki Cha UVIKO.
Ninachotaka kukwambia Ni kuwa usiwe mtu wa kuacha majanga kama haya yakapita tu, maana hiyo ni fursa ya kufanya ambayo ulikuwa huwezi kufanya kabla ebu fikiria kwamba wewe ulikuwa umejiajiri na unafanya biashara katika kipindi ambapo kila kitu kimefungwa unaweza;
Ila sasa kila kitu kimefungwa, unafanyaje,
· Unaweza kujifunza zaidi kuhusu biashara yako.
· Kujifunza ujuzi mpya mtandaoni.
· Kukaa karibu na familia yako na hivyo kupata muda wa kuwa na watoto. .
· Kuongea na wateja wako.
· Kuweka/kuhamishia biashara yako mtandaoni.
Hizo zote ni fursa. Magonjwa kama haya yanekuwa yakitokea mara nyingi. Kuna kipindi London iliwahi kutokea homa ya mafua na shule zote zikafungwa kama ilivyofanywa kwenye kipindi hiki cha UVIKO. Newton aliyekuwa Cambridge miaka hiyo alienda kwa bibi yake kujifungia na kutafuta suluhisho la majibu ya maswali aliyokuwa akijiuliza. Ni ndani ya kipindi hikihiki jamaa alikuja kugundua sheria ya uvutano.
Kikawaida kipindi cha matatizo huwa ni kipindi ambacho kinaimarisha baadhi ya watu au la huwa ni kipindi ambacho kinabomoa baadhi ya watu. ila uamuzi wa kujengeka au kubomoka kwenye kipindi cha matatizo ni wako mwenyewe.
Siku za karibuni mkoa wa Morogoro umepata shida ya umeme na hivyo kusababisha maji kuwa shida kwenye maeneo mengi. Kuna watu wameona fursa kwenye hili na kuitumia vizuri na hivyo naweza kusema wamejengeka na kuna watu wamebomoka. Kuna watu wanalalamika kwa sababu hawana maji na kuna watu wanaona fursa. Ninachotaka kukwambia wewe ni kuwa ujitahidi kuwa unaona fursa pale ambapo wengine wanakuwa hawaoni fursa.