Jinsi Hofu Invyoua Biashara Kabla Hata Haijaanza


Biashara nyingi huwa hazifi sokoni. Hazifi kwa kukosa wateja, hazifi kwa ushindani, wala hazifi kwa kukosa mtaji. Biashara nyingi hufa kabla hazijazaliwa—zinauawa na hofu.

Hofu ni adui wa kimya. Haina kelele, haina sura, lakini ina nguvu kubwa sana. Inamfanya mtu akae na wazo zuri kichwani kwa miaka, bila kuchukua hata hatua hata moja. Inamfanya mtu ajifariji kwa kusema “bado nafikiria”, wakati kiuhalisia anaogopa.

Hofu huanza na maswali madogo yanayoonekana ya kawaida: vipi nikishindwa? vipi nikipoteza pesa? vipi watu wakinicheka? vipi nisipofanikiwa kama wengine? Maswali haya yakikaa kichwani bila majibu sahihi, hugeuka kuwa minyororo inayokufunga usianze kabisa.

Moja ya hofu kubwa inayoua biashara ni hofu ya kushindwa. Watu wengi wanaamini kushindwa ni mwisho, wakati ukweli ni kwamba kushindwa ni sehemu ya mchakato. Hakuna mfanyabiashara aliyefanikiwa bila kufanya makosa. Lakini hofu humfanya mtu atake uhakika wa asilimia mia moja kabla hajaanza—uhakika ambao haupo kwenye biashara wala maisha.

Hofu nyingine ni ya maoni ya watu. Wengi huacha kuanza biashara kwa sababu wanafikiria wataonekanaje mbele ya familia, marafiki au jamii. Wanaogopa kuulizwa maswali, kudharauliwa au kuonekana hawajafanikiwa haraka. Lakini biashara haijengwi kwa makofi ya watu, inajengwa kwa maamuzi ya mtu binafsi.

Hofu pia hujificha kwenye kisingizio cha maandalizi yasiyoisha. Mtu anasema bado anajifunza, bado anafanya utafiti, bado anapanga. Kujifunza ni muhimu, lakini hofu hutumia kujifunza kama kisingizio cha kutokuchukua hatua. Ukweli ni kwamba baadhi ya mambo hujifunzwa kwa kufanya, na si kwa kusubiri.

Kinachoumiza zaidi ni kwamba hofu haichukui pesa zako, bali huchukua fursa zako. Pesa inaweza kupatikana tena, lakini muda uliopotea kwa kuogopa hauwezi kurudi. Miaka inapita, mazingira yanabadilika, na mtu anabaki na majuto ya “ningeanza mapema.”

Biashara haihitaji ujasiri wa kutokuwa na hofu. Inahitaji ujasiri wa kutenda licha ya hofu. Hofu haitapotea kabisa, lakini inaweza kudhibitiwa. Hatua ndogo moja inaweza kuizidi nguvu hofu yote iliyokaa kichwani kwa muda mrefu.

Ukweli ni huu: biashara inayokaa kichwani bila kuchukuliwa hatua si biashara, ni ndoto. Na ndoto zisizochukuliwa hatua hugeuka kuwa mzigo wa mawazo.

Kama kuna biashara unayoifikiria leo, swali ni: utaiacha hofu ikuamulie maisha, au utaamua kuchukua hatua licha ya hofu?


Kama hofu ya kuanza au kuchukua hatua imekuwa kikwazo kwako, vitabu hivi vitakusaidia kubadilisha mtazamo na kuchukua hatua kwa vitendo:

  • NGUVU YA KUCHUKUA HATUA YA KWANZA – Kwa yeyote anayekwama kwenye mawazo bila kuanza.
  • KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI – Safari ya hatua kwa hatua kutoka pale ulipo hadi unapotaka kufika.
  • MAISHA NI FURSA – Kukusaidia kuona fursa hata pale ulipojaa hofu na mashaka.

Kwa mawasiliano ya moja kwa moja na mwandishi au kupata vitabu vilivyopendekezwa (hardcopy, softcopy au audiobook):

👉 WhatsApp 0755 848 391
https://wa.me/255755848391

👉 WhatsApp 0684 408 755
https://wa.me/255684408755

Usiruhusu hofu iue biashara yako kabla haijazaliwa—chukua hatua leo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X