
Kwa juu juu wanaonekana sawa. Wote wanafanya kazi, wote wanahusika na pesa, na wote wanaweza kusema “niko kwenye biashara.” Lakini ukichimba kidogo, utagundua kuna tofauti kubwa sana kati ya mfanyabiashara na mtu anayetafuta pesa. Tofauti hii haipo kwenye kiasi cha mtaji wala aina ya biashara—ipo kwenye namna ya kufikiri.
Mtu anayetafuta pesa huanza kwa swali la haraka: nitapata pesa kiasi gani? Lengo lake la kwanza ni pesa, na mara nyingi ni pesa ya sasa. Anaangalia kazi au biashara kama chombo cha kumletea fedha za haraka. Akiona mapato hayaji kwa kasi alichoitarajia, hukata tamaa, hubadilisha mwelekeo, au kuacha kabisa. Kipaumbele chake ni matokeo ya leo, si mfumo wa kesho.
Mfanyabiashara, kwa upande mwingine, huanza kwa swali tofauti kabisa: ninatatua tatizo gani? Anaelewa kwamba pesa ni matokeo ya thamani anayotoa. Badala ya kukimbilia faida ya haraka, hujenga msingi—anafikiri kuhusu wateja, ubora, uaminifu na mwelekeo wa muda mrefu. Anaweza kuvumilia kipindi ambacho faida ni ndogo au haipo kabisa, kwa sababu anaelewa anachojenga.
Mtu anayetafuta pesa huona pesa kama lengo. Mfanyabiashara huona pesa kama zao. Ndiyo maana mtu wa kutafuta pesa huweza kubadilisha biashara mara kwa mara, akifuata “kinachoingiza pesa” kwa wakati huo. Leo anaweza kufanya biashara hii, kesho ni ile. Hana mwelekeo, hana uvumilivu, wala kinachomtambulisha. Kwa upande mwingine mfanyabiashara anajenga biashara moja au chache kwa umakini, akizielewa kwa kina, na kuzikuza taratibu.
Tofauti hii inaonekana pia kwenye namna wanavyokabiliana na changamoto. Mtu anayetafuta pesa akikutana na hasara, huona kama amekosea njia. Hujiambia “hii biashara haifai” na kuondoka. Mfanyabiashara huona hasara kama sehemu ya safari. Anauliza: nimejifunza nini? nifanye nini tofauti? Badala ya kukimbia, hubadilika.
Katika matumizi ya pesa, tofauti ni wazi zaidi. Mtu anayetafuta pesa akipata faida kidogo, huanza kuitumia kuonyesha mafanikio—anasa, matumizi ya haraka, au kuwaringishia watu. Mfanyabiashara huirudisha pesa kwenye biashara: kuboresha huduma, kuongeza uwezo, au kujenga mfumo imara. Anajua biashara si mashindano ya kuonekana, bali ni safari ya kujenga.
Zaidi ya yote, mfanyabiashara ana subira. Anaelewa kuwa biashara si mkato, bali ni mchakato. Mtu anayetafuta pesa anakosa subira, kwa sababu lengo lake ni pesa yenyewe. Anapotokupata haraka, hukata tamaa. Ndiyo maana wengi wanabaki kwenye mzunguko wa kuanza na kuacha, wakati wachache wanaendelea kujenga mpaka wanapoona matokeo makubwa.
Kabla hujaanza au kuendelea na unachokifanya, jiulize kwa uaminifu: mimi ni mfanyabiashara au natafuta pesa tu? Jibu la swali hili litaamua kama utadumu au utachoka njiani.
Kama ungependa kuondoka kwenye fikra za kutafuta pesa na kuingia kwenye fikra za ujenzi wa biashara, vitabu hivi vitakusaidia sana:
- MAISHA NI FURSA – Kukusaidia kubadilisha mtazamo wako kuhusu kazi, pesa na fursa.
- MAMBO 55 ya Kuzingatia Kabla ya Kuanza Biashara – Mwongozo wa vitendo kwa yeyote anayechukua biashara kwa uzito.
- TENGENEZA PESA KWA KUUZA UNACHOJUA – Jinsi ya kujenga biashara kwa kutumia maarifa na ujuzi ulionao.
Kwa mawasiliano ya moja kwa moja na mwandishi au kupata vitabu vilivyopendekezwa (hardcopy, softcopy au audiobook):
👉 WhatsApp 0755 848 391
https://wa.me/255755848391
👉 WhatsApp 0684 408 755
https://wa.me/255684408755
Achana na kutafuta pesa tu—anza kujenga biashara yenye mwelekeo na maana.