Vitu Vitano (05) Ambavyo Hupaswi Kuridhika Navyo


Habari ya siku hii ya leo rafiki na ndugu msomaji wa makala haya katika blogu yako ya SONGA MBELE. Imani yangu leo ni siku njema sana kwako na unaenda kufanya kazi kwa juhudi nguvu na kujituma. Hakikisha mpaka siku hii ya leo inapofikia mwisho haulali na kitu ambacho ulipaswa kuwa umekifanya leo. Kama kuna jambo la kufanya leo hii, basi hakikisha kwamba unalikamilisha. Kulala na kitu ndani yako, ni sawa na kufa na mziki ndani yako ambao hujaufanyia kazi. Ni sawa na kufa na wazo kubwa sana la kibiashara.

Kwa kawaida binadamu huwa anapenda sana kuridhika. Yaani akiwa anatafuta vitu fulani, basi akisha kuvipata basi maisha ni mazuri hata hajisumbui tena. Mpaka pale itakapokuwa imetokea hali ya hatari ndipo atakuja kustuka na kukimbizana tena ili apate kile anachokikosa. Akikipata tena basi anatulia. Ndivyo ilivyo. Kuna sheria moja ya NEWTON ambayo inasema hivi kila kitu kitaendelea kuwa katika nafasi yake mpaka pale kani itakapokuwa imekipitia. Basi kuna watu wanaridhika na maisha mpaka pale kani inapokuwa imebadilisha mwelekeo wao.
Rafiki yangu kuna vitu vya kuridhika navyo na vitu ambavyo hupaswi kuridhika navyo,  hapa ninakupa orodha ya vitu vitano ambavyo hupaswi kuridhika navyo

1. MSHAHARA
Kama wewe umeajiriwa na chanzo chako cha kipato ni mshahara tu, basi hapo hupaswi kuridhika hata kidogo. Fanya ufanyalo ili uongeze mfereji mwingine wa ziada kuanzia sasa. Huwezi kuijenga kesho bora kama utaendelea kuridhika na kufanya vitu kwa namna ileile. Mshahara tu ni utumwa. Maana utakunyima uhuru wa maisha. Lakini pia utakunyima Uhuru wa kutoa maoni na haswa pale unapoona vitu haviendi vizuri. Basi utakuwa kila wakati unafikiri kwamba ukitoa maoni basi ndio unafukuzwa kazi. Utafumbwa mdomo hata pale unapoona wazi wazi kwamba ulipaswa kutoa maoni. Si hivyo tu chanzo hiki kikiingia dosari basi jua kwamba ndio umepoteza kila kitu. Au kikichelewa na wewe una mpango mwingine, basi jua kwamba na wewe unachelewa. Kamwe usiridhike na chanzo kimoja tu cha pesa, kamwe usiridhike na mshahara hata kama ni mkubwa kiasi gani. Mshahara ni utumwa.
Hapo mwanzo mishahara haikuwepo. Lakini kadri siku zilivyoendelea hasa wakati wa maendeleo ya viwanda ndipo mishahara ilitokea. Wakaanza kuwalipa watu asilimia 10 tu kati ya asilimia 100 ambayo mtu alikuwa kazalisha. Kwa hiyo kama wewe unalipwa milioni jua kwamba kazi uliyoifanya ni zaidi ya milioni kumi na wewe umetolewa asilimia kumi tu! Sasa kwa nini unaendelea kuridhika na hali hii wakati unaweza kuzalisha milioni kumi zaidi. Hakikisha hauridhiki na hali kama hii hata kidogo.

2. GARI
Ukiongea na vijana wengi sana, basi utasikia maneno kama haya hapa, “mimi nikishapata kazi tu, kitu cha kwanza ninaenda kuchukua mkopo ili nichukue gari langu”. Ukimuuliza baada ya hapo, basi atakwambia mimi nitaanza kula misele. Rafiki yangu gari si kitu cha kuridhika nacho. Wewe ni zaidi ya gari. Kile kilicho ndani ya wewe ni kikubwa 1000*1000 zaidi.
Usitulie na kidogo ambacho utakipata sasa. Endelea kutengeneza kesho bora. Na isitoshe kama wewe unanunua gari la kutembelea, ni kitu ambacho hakiingizi pesa mfukoni mwako, hivyo hupaswi kukimbilia gari maana kila wakati litakuwa linatoa pesa ya mafuta mfukoni, mara limetoa pesa ya service nakadharika nakadharika. Usiridhike tu kwa sababu una kijigari na pengine unekipata kwa mkopo. Endelea kupiga kazi ili uweze kufanikisha kazi yako na kupata maendelek makubwa zaidi ya hapo.  Haswa kuwa na vyanzo vingi vya kipato.

3. MTOTO KUSOMA SHULE ZA MEDIUM
Nchini Tanzania kwa sasa shule tumeziweka katika makundi mawili. Moja ni kundi la shule za bodafasta. Maarufu sana kama shule za kata au senti kayumba. Pamoja na shule za MEDIUM. Mtu anapokuwa amempeleka mtoto wake shule ya medium. Basi anaona kwamba ndio kamaliza kila kitu. Anaona kwamba mtoto amemtengenezea future yote na yeye hana shida ya kuanza kuhangaika tena. Rafiki yangu, jambo hili halipaswi kukupa usingizi na wewe ukalala fofofo. Mtoto wako kusoma shule za medium ni hatua nzuri sana ambayo umepiga lakini haupaswi kuishia hapo. Unapaswa kuendelea kuweka juhudi ili hata pale mtoto wako atakapoenda chuo uwe na uwezo wa kumsomesha bila shida yoyote. Sio anafika chuo, ndio unaaanza kuhangaika ili apate mkopo. Kumbe wewe ulikuwa na muda wa kumtengenezea mkopo japo uliutumia ndivyo sivyo. Jambo la kuondoka nalo hapa ni kwamba usiridhike tu na watoto kusoma shule za medium.

4. KUCHEZA KAMARI
Bwana bwana weee! Siku hizi kuna haka ka mchezo ka kubeti! Sijui kametoka wapi? Yaani kanaingia kwa kasi sana nashangaa. Watu wanakakumbatia kama vile ni fursa ya kijaaanja ambayo imegunduliwa. Kumbe ni kamchezo ka kamari kalikuwepo tangu zamani zile ila leo kamekuja kwa njia ya kidigitari. Yaani huwa nawashangaa sana watu. Eti mtu anabeti kwa sh. 500/- ili apate milioni hamsini. Hahaha! Vijana huu ndio mufa wa kubadilika. Zama zimebadilika.  Tafuta njia nzuri ya kuwekeza lakini sio kwa kubeti. Kubeti ni kamari hata kama utasema inalipa Kofi. Kulipa kodi hakuondoi ukweli kwamba kubeti ni kamali. Jihadhari sana kijana. Mwalimu Nyerere aliwahi kunukuliwa mara nyingi sana akisema hivi RUSHWA NI ADUI WA HAKI. Sasa leo hii Mimi Godius Rweyongeza naomba ninukuliwe kama ifuatavyo “KUBETI NI ADUI WA MAENDELEO”. Jiepushe sana na hili.

5. KULA BATA KILA WIKENDI
Ile mmenda bar na mmekunywa mbili tatu na umewanunulia washikaji bia za kutosha, basi unajiona mjaaanja! Hujui hapo unajipiga Bomu bila huruma. Kama kiukweli upo makini na maendelep nakushauri hivi achana na vilevi kwa asilimia 100%. Anza kufanya kazi za kimaendeleo. Vilevi vinakufanya mteja. Kuna kazi nyingi sana unaweza kufanya badala ya vilevi. Chukua pesa uliyokuwa unanunua bilevi basi itumie kuwekeza. Kuna watu wamenogewa na ulevi kiasi kwamba hata ukimpa chakula kitamu basi ataishia kukushukuru, maana kwake kutulia kwake ni pale napokunywa kilevi cha aina fulani. Badilika sasa.

Tukutane siku nyingine hapa hapa safuni!
Ulikuwa nami
Godius Rweyongeza
Jipatie  sasa nakala ya vitabu vyangu, TATIZO SI RASILIMALI ZILIZOPOTEA na KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI kwa pamoja kwa bei ya sh. 14,000tu badala ya sh. 20,000.
Tuma pesa kwenda nambari 0755848391 jina GODIUS RWEYONGEZA
baada ya hapo nitumie ujumbe wa njia ambayo ungependa nikutumie vitabu hivi, inaweza kuwa wasap, telegram au email.
Karibu sana.
Bei ya kitabu kimoja kimoja
1. TATIZO SI RASILIMALI ZILIZOPOTEA (6,000)
2. KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI (8,000).
bei hizi ni kwa siku chache tu baada ya hapo kila kitabu kitakuwa kinapatikana kwa sh. 10,000


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X