KUTOKA SIFURI MPAKA UBILIONEA (Mbinu Kumi Zitakazokuinua Mpaka Ubilionea)


Habari ya siku hii njema sana rafiki yangu. Hongera sana kwa siku hii.
Karibu sana kwenye makala hii ya leo tujifunze ni kwa jinsi gani tunaweza kutoka sifuri mpaka ubilionea.

Hivi umewahi kufikiri juu ya kuwa na maisha ambayo utakuwa huwazi juu ya pesa ya kula?
Maisha  ambayo hufikirii na kuumiza kichwa ni wapi utapata ada ya mtoto?
Je, umewahi kufikiri juu ya kuwa na maisha ambayo huna hofu ya kufukuzwa kwenye nyumba na mwenye nyumba kwa sababu ya kutokuwa na pesa ya kodi?
Je, umewahi kufikiri juu ya maisha ambayo utakuwa na ndege yako binafsi na kwenda unapotaka muda unaotaka?
Je, umewahi kumwona mtu anahangaika ukataka kumsaidia ila ukajikuta una 200 tu mfukoni? Na bado 200 hiyo wewe unaihitaji?
Je, umewahi kuwaza juu ya kutembea dunia hii kutoka kasikazini, kusini mashariki mpaka magharibi?

Umewahi?

Rafiki yangu kama kuna sehemu hapo juu umejibu ndio. Basi kwa haraka haraka nikwambie suluhisho la hayo yote ni KUWA NA PESA.  Ukiwa na pesa utaweza kufanya hayo yote bila kuzuiliwa na mtu na utaweza kufanya zaidi.

Pesa ina mkondo wake. Ili kuipata pesa unapaswa kutengeneza mkondo huo. Ambao mwisho wa siku utakuwezesha kufanya utakacho. Pesa ni zao la kufikiri na kuwa na mawazo bora. Mawazo ya namna fulani yatakuwezesha wewe kuweza kupata pesa na kuondokana na umasikini na mawazo ya namna fulani yatakuangusha.

Sasa rafiki yangu ili upate pesa ya kukutosha kiasi cha kwamba hutakuwa na hofu, basi unapaswa kuwa na malengo makubwa sana.
Ndio malengo makubwa yaani ya kukufikisha kwenye ubilionea.

Sasa leo hii nimekuandalia makala yenye mbinu zitakazokutoa hapo ulipo na kuweza kukufikisha kwenye ubilionea.

Ninamamisha nini ninaposema KUTOKA SIFURI?
Sifuri ni hapo ulipo. Kwa kipato hicho ulichonacho kwa kipaji hicho ulichonacho
Kwa namna ya kufikiri hii uliyonayo
Kwa utendaji wako wa sasa
Kwa ufanisi wako wa sasa.

NINAPOSEMA KUTOKA SIFURI simaanishi
Kwamba hauna kitu.
Simaanishi kwamba hauna senti. Unaweza ukawa na pesa kidogo, nasema pesa kidogo kwa maana kulinganisha na kule ambapo unapaswa kwenda bado una safari ndefu sana. Bado una njia ndefu ya kuchukua. Hivyo kwa sasa jichukulie kwamba upo sifuri, ila anza kutumia mambo yatakayotolewa hapa chini ili utoke hapo mpaka ubilionea.

NINAPOZUNGUMZIA UBILIONEA;
 Ninaamaanisha kuwa na pesa zinazofikia trilioni 1.5 za kitanzania ambazo kwa dola za marekani ndio bilioni moja. Sitaniii!!

Ninamaanisha kwamba uwe na kiasi cha kukutosha kununua unachopenda bila kuhofu.

Sasa rafiki yangu fanya haya hapa ili uweze kuufikia ubilionea.

1. KUAA NA MAONO MAKUBWA
Kwa kawaida ili uweze kuishi macho ndio hutusaidia kuona vitu kadha wa kadha. Macho yetu yana uwezo mkubwa sana wa kuona vitu vyenye rangi mbalimbali. Macho yetu yanaweza kutofautisha kati ya kitu kilicho mbali na karibu. Macho yetu yanaweza kutofautisha kati ya kirefu na kifupi. Hivi vyote hutokea kwenye hali ya kawaida ya maisha. Hata hivyo tunapoishi kwenye ulimwengu wa biashara MAONO ndio yanafanya kazi.
Katika biashara unapaswa kuwa na maono makubwa sana.

Maono katika biashara hayonekani kwa macho. Tunatumia akili ya kufikiri kupata maono.

 Usiogope kuwa na ndoto kubwa sana. Maana kama ambavyo Napolleon Hill amewahi kuandika, kama unafikiri huwezi, huwezi. Hivyo usikae na kuanza kufikiri na kuwa na maono madogo. Kuwa na maono makubwa sana. Ona uzuri wa maono yako. Kila wakati piga hatua na hakikisha unasonga mbele.

Naomba nikwambie kitu rafiki yangu. Kama hutakuwa na maono maana yake utatembea katika giza. Na mwisho wa siku utapotea. Au kiufupi ni kwamba bila maono basi kwako kila sehemu iliyopauriwa ni njia.

Na kama mambo yako ndio hayo hapo basi upo njiani kupotea.

2. WEKA NGUVU YAKO SEHEMU MOJA MPAKA KIELEWEKE
Tupo kwenye dunia yenye kelele nyingi kweli. Tupo kwenye dunia ambapo ukianza kufanya hiki huyu anapita anafanya kile. Ukitaka kutuliza akili yako mara mitandao ya kijamiii inakuita. Yaani tupo kwenye dunia ambayo sisi vijana tunaiita VURUGU MECHI. Yaani usumbufu ni wa kila aina.

Kwenye dunia hii hii bado unaweza kufanya makubwa sana. Kitu kikubwa ni  KUWEKA NGUVU NA AKILI YAKO SEHEMU MOJA MPAKA UNAPOIKAMILISHA.
Au kwa lugha nyingine tunaweza kusema hivi, kufanya kitu kimoja mpaka kikakamilika.

Rafiki yangu kwenye dunia hii ukiamua kufanya kitu. Usirudi nyuma. Hakikisha unaweka nguvu yako pale mpaka kiishe. Usiishie tu kukigusa na kwenda kufanya kingine. Kifanye, kifanye mpaka kieleweke.

3.CHUKUA HATUA.
Kila wakati hakikisha unachukua  hatua kufanya kitu fulani ambacho ulikuwa hujawahi kufanya.
Chukua hatua kuwekeza,
Chukua hatua kuanzisha biashara mpya
Chukua hatua na utumie kipaji chako.

Dunia inawalipa watu wanaochukua hatua zaidi kuliko inavyowalipa wazembe.

4. KUBALI KUBEBA MAJUKUMU
Kati ya kazi ambazo watu wengi sana wanakwepa basi ni kazi ya kubeba majukumu.  Ndio maana utawaona walio wengi wanawatulia wengine mpira haswa linapotokea kosa mahali kwenye utendaji ili wao  waonekane ni wasafi.

Rafiki yangu, majukumu yako yawe ya kwako na kubali kuyabeba.  Pale unapokosea usimtupie mwingine mpira. Jifunze na songa mbele.

5. FUATILIA BIASHARA YAKO
Ni rahisi sana kwenye ulimwengu huu kufuatilia masuala ya watu wengine. Ni rahisi sana kwenye ulimwengu kujua kinachaoendelea taifa jingine kuliko kwenye taifa lako mwenyewe.

Ila nakuomba kitu kimoja, FUATILIA BIASHARA YAKO KULIKO UNAVYOFUATILIA KITU KINGINE.
Usipoteze muda kufuatilia maisha ya watu wengine. Usipoteze muda kugoogle nani anatoka na nani?

Ipende sana biashara yako kiasi kwamba muda wako mwingi unautumia kuifanya.

6.KUWA TAYARI KUSHINDANA.
Dunia imejengwa kwenye misingi ya kiushindani.
Miti hushindana kwa ajili ya chakula, maji na virutubisho. Hali hii haiishii kwa miti tu. Hata kwenye biashara. 

Ushindani kwenye biashara ndio unaleta ubunifu mpya, teknolojia ya kisasa.

Kumbuka ushindani sio jambo la lazima nishinde la sivyo sitamwelewa mtu (win at all cost). Muda mwingine ushindani ni jambo la kumfanya kila mtu ashinde kwa upande wake (win-win situation)

7. VUMILIA MPAKA KIELEWEKE
Linapokuja suala zima la ubinifu basi yamesemwa  mengi. Ndio maana utasikia misemo kama, maisha yakikupa limau tengeneza juisi. Au utasikia, ukifanya kitu fulani bila mafanikio basi fanya tena.

Misemo hiyo yote inatuasa kuwa watu wa kuvumilia mara nyingi tuwezavyo. Yaani inatutaka kuwa wagumu linapokuja suala la mafanikio.

8. KUWA NA AKILI YA UKUAJI
Katika dunia kuna watu wenye akili ya ukuaji na watu wenye akili iliyosimama.

Watu wenye akili ya ukuaji ni watu ambao kila wakati wapo tayari kujifunza kitu kipya. Wapo tayari kulipa gharama ya maarifa.
Wapo tayari kuonekana wajinga kwa dakika tano kwa manufaa ya miaka ijayo. Hivyo wanauliza na wanasoma katika mchakato wa kutaka kukua zaidi.

     Watu wenye akili iliyosimama (akili mgando), wanapenda sana kuonekana makini (smart). Hawapendi kuonekana wajinga. Wala hawapendi kuuliza. Hawana muda wa kusoma wala kujifunza. Mwisho wa siku wanapitwa na wakati.

Rafiki yangu kama kuna kitu unapaswa kukichagua, basi wewe chagua kuwa na akili ya UKUAJI.

 
9. TENGENEZA MTANDAO
Ukitaka kwenda kasi basi tembea peke yako, ukitaka kwenda mbali basi tembea na watu, hii ni methali ya Kiafrika. Methali hii inanikumbusha usemi mmoja wa wahaya unaosema “akagenda konkai, kaba akomwirungu”. Kwa tafsiri isiyo rasmi ikimaanisha, kitu kinachotembea peke yake ni mnyama wa porini.

Kama unavyoona wahenga wetu wa afrika walishatuasa juu ya kutengeneza timu ya watu tunaowahitaji kufikia mafanikio.
Unahitaji timu ya watu kwenye biashara kama zilivyo timu za mpira.

Mtandao wako unaofahamiana nao ndio utatuambia ni watu gani unafanya nao biashara, mtandao wako utatuambia wewe una mawasiliano na watu gani. Lakini pia mtandao wako utakupa washirika pamoja na wateja.

Kadri unavyoongeza mtandao ndivyo kila kitu kinavyoongezeka. Na kadri mtandao wako unavyopungua ndivyo unajiweka hatarini.

Kumbuka mambo haya matatu wakati wa kutengeneza mtandao

>>kila unapokutana na watu iwe ni kwenye semina au mkutano wa kibiashara inakuwa ni nafasi yako kutengeneza mtandao
>>Pili tambua, uwepo wa watu wengine na hivyo waheshimu na wasikilize
>> Tatu mtendee kila mtu kama ambavyo wewe ungependa kutendewa (kanuni ya dhahabu) .
>>Na nne kumbuka uaminifu ni falsafa bora sana ya maisha ambayo unapaswa kuishi.

10. JIAMINI NA JIKUBALI
  Kuwa na mawazo makubwa ya biashara haitoshi. Unatakiwa kujiamini kwa kiwango kikubwa.  Jimini kwa kuchukua hatua ya kwanza. Jiamini kwa kuendelea kufanya hata kama watu wengine wote wanakucheka.
Kujiamini huleta mafanikio na mwisho wa siku mafanikio hujenga kujiamini zaidi.

Nakushukuru sana kwa kuweza kufuatilia somo hili mpaka mwisho. Umekuwa nami rafiki yako wa ukweli Godius Rweyongeza

Hakikisha Umesubscribe kwenye Channel yangu ya youtube kwa KUBONYEZA HAPA

Jiunge na mfumo wa kupokea makala maalumu kwa njia ya barua pepe kwa KUBONYEZA HAPA

Jipatie nakala za vitabu vyangu vya kiswahili kwa KUBONYEZA HAPA

Kama ungependa kujifunza kuhusu uandishi wa vitabu kutoka kwangu wasiliana nami kwa 0755848391

 Kupata nakala ngumu ya kitabu cha KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI na kitabu cha JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO basi tuma ujumbe au piga kwa 0755848391

Kutengenezewa blogu yako kitalaamu tuwasiliane kwa 0755848391

kila la kheri

Kunialika kwa ajili ya kutoa mafunzo au semina kwenye kikundi chako, taasisi, kongamano n.k. wasiliana nami kwa email: songambele.smb@gmail.com au simu 0755848391


2 responses to “KUTOKA SIFURI MPAKA UBILIONEA (Mbinu Kumi Zitakazokuinua Mpaka Ubilionea)”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X