Kila mwaka kuna idadi kubwa sana ya wanachuo wengi sana wanaohitimu kutoka vyuo vikuu mbali mbali hapa nchini.
Idadi ya wanachuo wanaohitimu kila mwaka ni kubwa sana ukilinganisha na idadi ya watu wanaoajiriwa. Hivyo kufanya vijana wengi waliohitimu chuo kuzurura mitaani, wakizunguka huku na kule kutafuta ajira.
Wapo wanaobahatika na kupata ajira hizi hata hivyo huja kuangua vilio baada ya siku chache, pale wanapopewa barua za kuachishwa kazi kwa sababu ya kukosa ujuzi, kutojituma, uzembe, n.k
Kwa hakika hali hii inaleta kitendawili ambacho ni kigumu kukijibu. Hali kama hii imewasukuma wanachuo wengi kujihusisha na ujasiliamali. Hata hivyo bado kilio cha wanachuo walio wengi sana ni mtaji.
Wapo pia wengine ambao hawapendi kuajiriwa ila wanapohitimu wananajikuta wakihangaika huku na kule bila kazi ya kumpatia kipato, kisingizio kikuu kikiwa ni mtaji.
Sasa je, kuna shida gani? Je, kuna jinsi ambavyo mwanachuo anaweza kupata mtaji wa kuanzia akiwa bado anasoma?
Jibu langu ni NDIO. Inawezekana kwa mwanachuo yeyote kupata mtaji akiwa bado chuo. Hata hivyo atahitaji kujitoa, kuwa na nidhamu na kuhakikisha anachoamua ameamua kweli, sio kila mara anayumbishwa na kutumia ile pesa yake aliyoiweka akiba.
Kwa vyuo vya Tanzania shahada nyingi huchukua miaka mitatu, minne au mitano.
Stashahada huanzia miaka miaka miwili , wakati astashahada huanzia mwaka mmoja.
Miaka hii ya chuo, unakuwa ni muda mzuri wa mwanachuo kuweka akiba na kutengeneza mtaji wa kuanzia anapohitimu maana ni bora kujiandalia kwa ajili nyakati za njaa na zisitokee kuliko kutojiandaa na nyakati hizi zikaja kutokea.
Kwa wanachuo muda wa chuo ni muda wa kujiandaa kwa nyakati za njaa, au nyakati za baada ya chuo na kupata cheti (maarufu sana kama semester ya 7 kwa wanachuo wengi)
Hivyo ndani ya kipindi hiki akiba yako unaweza kuiweka kama ifuatavyo:
Moja kuhakikisha kwamba siku zako zote za chuo unaweka akiba ya shilingi elfu moja (1,000/-)
Kama utaweka akiba ya shilingi elfu moja kila siku kwa mwaka utakuwa umeweka kiasi ambacho ni sawa na laki tatu na elfu sitini na tano (365,000/-). Kama utaweka akiba kwa miaka miwili maana yake utapata kiasi cha laki saba na elfu thelathini (730,000/-)
Elfu moja kama elfu moja ni hela ndogo sana ila kama utaamua kuiweka akiba kwa mkusanyiko kama huu mpaka unahitimu chuo kama ni miaka miwili au mitatu utakuwa umepata akiba kubwa sana ya kukuwezesha wewe kupata mtaji wa kuanzia.
Na isitoshe mkiungana vijana wawili au watatu wenye moyo wa kufanya makubwa na mkaweka akiba kwa mfumo huu, hii ndio kusema mpaka mnahitimu chuo mnaweza kuwa na akiba inayofikia milioni mbili na zaidi. Kwa hakika huu ni ushindi mkubwa sana kwa mwanachuo na hapa utapata mtaji mzuri sana wa kuanzia baada ya kuhitimu.
Pili, wewe kama mwanachuo unapaswa kupunguza matumizi ili upate pesa ya kuweka akiba.
Tumezoea kwamba chuo kinazungumziwa kama sehemu ya kula bata. Ila sasa kama kweli una ndoto za kupata mtaji wa kuanzia baada ya kuhitimu, bata unaweza kuziweka pembeni na kuamua kwanza kuweka mtaji. mwisho wa siku utakuja kula bata na mayai yake.
Kama ulikuwa na tabia ya kutoka kila mwisho wa wiki, sasa ni wakati wako wa kujibana na kuhakikisha unaacha kabisa maana hutapungukiwa na kitu. Lengo ni wewe upate mtaji. Kwa hiyo jambo hili unalifanya kwa manufaa yako wala sio kwa manufaa ya rafiki zako au mimi.
Tatu, punguza vifurushi unavyonunua.
Kuna wanachuo mnanunua vifurushi vya muda wa maongezi kwa fujo. Unakuta una laini tatu na zote zina vifurushi tena sio vifurushi vya bei rahisi. Yaani vifurushi kweli kweli.
Sasa kweli kama wewe upo makini, vifurushi vya laini tatu vyote vya nini?
Kwa nini usipunguze matumuzi hapa ukapata hela ya mtaji wa wewe kuanzia utakapohitimu chuo?
Na tena unakuta kwa wiki unajiunga mara tatu au mara nne na zaidi. Kiukweli hapa mwanachuo unaweza kufanya kitu ili uweze kupata mtaji wa kuanzia utakapohitimu.
Kwa bahati nzuri kuna maeneo hapo hapo vyuoni unaweza kupata mtandao wa intaneti bure kabisa (Free WIFI). Unaweza kuyatumia . kupunguza matumizi ya vocha za kila siku. Mwanachuo funguka wakati ndio huu.
Nne, mnaweza kuungana kikundi cha wanachuo.
Hapa mnaweza kuamua kuanza kuweka akiba kwa pamoja. Hii itakupa nidhamu zaidi haswa kama wewe una ugonjwa wa kuweka akiba na ndani ya muda mfupi ushaitoa kwenda kuitumia. kikundi hiki kitaweza kutunza pesa na wewe hutaweza kuzipata kama ambavyo ungefanya ukiwa peke yako. Lakini hii pia itaongeza ukubwa wa mtaji na kuufanya uwe mkubwa zaidi kulinganisha na pale ambapo ungekuwa peke yako.
Tano, usinunue vitu ambavyo hutumii kwa sasa.
Ni mara nyingi sana watu huwa wananunua vitu na kuanza kujilalamikia kwamba wametumia/wamepoteza pesa yao bure. Kwa hiyo wewe mwanachuo jiepushe na mtego huu. Ukiona umenunua kitu ambacho hukitumii kabisa, iwe ni nguo, kiatu, simu au chochote, jua umepoteza pesa ambayo ungeiwekeza. Nakushauri kabla ya kununua kitu ujiulize swali, je, kama sitanunua kitu hiki nitakufa? Kama huwezi kufa kwa sababu ya kukosa hicho kitu, basi kiache na hiyo pesa iweke kama akiba.
HITIMISHO
Ewe mwanachuo funguka sasa, maana siku zenyewe hazigandi. Leo hii upo chuo, kesho utakuwa mtaani. Na hapa ndipo utapaswa kuanza kujitegemea na kuishi wewe kama wewe. Jamii itakuangalia kama wewe ulivyokuwa unaingalia wakati unasoma.
Lakini kama ulifikiria nje ya kumi na nane wakati upo chuo, basi huu utakuwa muda wako muafaka wa kuanza biashara yako.
Asante sana
Tukutane kwenye jukwaa la wanamafanikio
One response to “Hivi Ndivyo Unaweza Kupata Mtaji Wa Biashara Ukiwa Bado chuo”
[…] Hivi Ndivyo Unaweza Kupata Mtaji Wa Biashara Ukiwa Bado chuo […]