Je, Kuna Haja Ya Kuendelea Kusoma Wakati Ajira Hakuna?


Jana kupitia Temino ya Clouds FM niliongea na wanachuo wote hapa nchini, huku nikiwasisitiza juu ya umuhimu wa kutumia bumu lao la chuo vizuri maana kuna maisha baada ya chuo.

Waendeshaji wa kipindi hicho ambao ni Harris Kapiga pamoja na Advovate Henry Mwinuka nao walisisitiza pointi muhimu sana kwa kusema kwamba kila mwaka kuna wahitimu zaidi ya laki nane ambao wanahitimu na miongoni mwao, ni wahitimu elfu themanini tu ambao wanapata ajira. Huku wahitimu laki saba na elfu ishirini wakibaki bila ajira. Na hizi usifikiri ni takwimu za kubahatisha. Hapana, ebu angalia screenshot hizi hapa chini

Hii nimeitoa kwenye tovuti ya bunge la Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania. Kama hujaweza kuona vizuri, ebu yasome hayo maneno hapa chini

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, kila mwaka takribani Wahitimu laki nane, kwa mwaka, na wanaoajiriwa ni elfu arobaini peke yake, kwa hiyo laki saba na sitini wanabaki mtaani. Ningependa kujua Serikali ina Mkakati gani wa ziada, kwa sababu Mkakati uliopo umeshindwa kukidhi vigezo vya kuweza kuwaajiri vijana wengi ambao wamehitimu? Ni Mkakati gani wa ziada ambao Serikali inao kwa ajili ya kuwasaidia Vijana hawa ambao wengi wako mtaani?

Screenshot nyingine hii hapa

hii nimeitoa kwenye tovuti ya gazeti la habari leo. Iliandikwa tarehe 28.12.2021

Sasa swali la mmoja aliyesikia huo ujumbe lilikuwa ni hili hapa

Habari bro mm naitwa mtima nimekusikia kwenye kipindi cha chimbo clouds FM mm nilikua naomba ushauli kama ajira ni chache je kunahaja ya kusoma maana unaweza kusoma na usipate ajira alafu ukawa umepoteza mda mm ni mwanafunzi naelekea kujiunga na kidato cha tano

Kama unavyoona hapo. Leo ninaenda kuwa najibu swali la je, kuna umuhimu wowote ule wa mtu kuendelea kusoma wakati ajira hamna? Kuna umuhimu wowote kweli, au ndio bora ukaanze biashara kabla hata ya kupoteza fedha na muda?

Eti kwa mfano wewe kwa maoni yako unasemaje?

Kwenye hili siendi kuongea sana, badala yake napenda kwanza nikupe stori.

Mwaka 2017 nikiwa chuoni, nilitaka kuacha chuo. Siriazi, nilitaka niache chuo, ili niende nikaanzishe biashara.

Niliongea na rafiki zangu na kuwapa taarifa kuwa ninaenda kuacha chuo, na baadaye nikaongea na wazazi ambao hawakupenda uamuzi huo kabisa. Wazazi wangu walikuwa wachungu kwenye hili kuliko hata mwimba.

Baadaye nikaongea na mshauri mmoja ambaye alinipa ushauri, ambao ningependa niutoe kwako pia.

Aliniambia hivi, Godius huna haja ya kuacha chuo na kwenda kuanzisha biashara. Badala yake pambana na vyote viwili. Anzisha biashara na soma chuo. Ukifanikisha kufanya vyote viwili ukiwa chuoni, utakuwa shujaa.

Kwangu huu ushauri niliupokea kwa mikono miwili, hivyo niliamua kukomaa na chuo na wakati huohuo nilianzisha biashara na kukomaa nayo.

Kwa hiyo kwanza kabisa ningependa kukwambia kwamba, USIACHE KUSOMA. SOMA KWA BIDII NA UFAULU. ILA SASA FIKIRI NJE YA MASOMO. Na hapa sasa ndipo nataka nikupe mbinu na vitu ambavyo huwezi kuvipata sehemu nyingine.

Labda tujiulize ni nini lengo la shule? Je, ni kukaririsha watu vitu wasivyovielewa? Ukiniuliza mimi nitakwambia hivi

#1. LENGO LA ELIMU NI KUTENGENEZA WATU AMBAO WANAWEZA KUTAFSIRI KILE WANACHOJIFUNZA KWENYE MAISHA YA KAWAIDA

Nakumbuka siku moja niliwahi kumsikia mkuu wa chuo cha SUA akihoji watafiti kuwa je, hizo tafiti mnazofanya zinawasaidiaje wananchi wa kawaida? Unaone ee.

lengo la elimu siyo kwamba ukariri kile unachojifunza darasani. Badala yake ni kwamba, uweze kutafsiri kile unachojifunza na kukileta kwenye maisha ya kawaida.

Nakumbuka tukiwa mwaka wa pili pale chuoni. Tulisoma kozi moja inaitwa SPICE PRODUCTION (uzalishaji wa viungo) Viungo si unavijua? Mambo ya iriki, tangawizi, karafuu…Mambo ya Pemba hayo yahe…

Hii kwangu ndio ilikuwa ni kozi ya kipekee iliyokuwa na vitu vingi ambavyo nilikuwa napenda. Niliona kuna vitu vingi ndani yake ambavyo ningeweza kuvitumia kwenye maisha ya kawaida ya kila siku. Na hivyo, nikawa nimeamua kwamba baada ya chuo, nitakuwa nashughulika na uzalishaji na usindikaji wa viungo. Kwa hiyo, nikawa nimeona fursa kutokana na kile nilichokuwa nimejifunza na sasa hivi nimefungua kampuni inayohusika na uzalishaji wa viungo.

Laiti ningeacha chuo nikiwa mwaka wa kwanza, hiki kitu nisingekaa nikakisoma mwaka wa  pili. Na sijui sasa hivi kampuni yangu ingekuwa inahusika na nini

Kwa hiyo, endelea kusoma, ila sasa jiulize kwenye kile ambacho unajifunza darasani, unawezaje kukitumia kwenye maisha ya kwaida ya kila siku. Huku mtaani, kuna watu wana shida na wanategemea wasomi wazitatue, siyo kwamba wasomi watatatua hizi shida kwa kuwapa hela. Hapana, bali kwa kuwaletea suluhisho sahihi.

Wewe hujawahi hata kumsaidia bibi kizee huko kijijini ambaye simu yake imejifunga tu, labda watoto walikuwa wanaichezea, ila kwa sababu hajui kiingerereza haelewi wapi pa kubonyeza. Mara paap akaileta kwako, ukasoma soma vitu viwili vitatu, ukaifungua akafurahi? Hujawahi? Mimi huwa inanitokea sana, na hiyo huwa inanipa picha kwamba hata matatizo mengine yanayokumba watu huku mtaani, ukiyatatua, watu watafurahi hivi hivi….

Kwa hiyo, kila mara unapaswa kuwa unajiuliza  nasoma chuoni. Lakini, hawa uliowaacha nyumbani kwenu. Wanawezaje kunufaika na hiki ninachosoma. Je, kuna namna ambavyo wanaweza kunilipa kutokana hiki ninachosoma kama ipo. Basi zama ndani, ukijue hicho kitu. Ili baadaye uje ukigeuze hicho kitu kuwa biashara.

Hivi Geometry ndio elimu ya maumbo ee…

Au basi siyo lazima uelewe kila kitu, vingine utaelewa siku ya mtihani…Hahaha

Ila ninachotaka kukwambia ni kwamba, Ben Carson anasema kaka yake aliona fursa kwenye hiyo elimu ya maumbo na akaamua kuitumia kwenye maisha ya kawaida ya mtaani.

Hiki ni kitu ambacho shuleni walimu wako hawakwambii, ila ukweli ni kwamba, kwa kila unachojifunza unapaswa kuangalia namna ambavyo unaweza kukitumia kwenye maisha ya kawaida ya huku mtaani. Maana huku, ndio kuna maisha yenyewe…

Siyo kila kitu kitakufaa wewe, na haipaswi kuwa hivyo, unahitaji kitu kimoja tu ambacho unaweza kutumia huku mtaani, vingine waachie wengine.

Sijui unanielewa….

Kama umenielewa basi, vuta pumzi kidogo wakati mimi nakunywa maji hapa….

Kafanyaje huyu?

#2. Imani ni yangu kuhusu chuo ni kwamba, chuo kipo kwa ajili ya kuandaa watu ambao watakuja kuajiri baadaye

Hii ni imani yangu na ni msimamo wangu, hata ukiniamsha saa nane usiku, na kuniuliza ebu niambie kazi za shule na vyuo ni vipi.

Nitakwambia vyuo vinapaswa kuandaa watu ambao watakuja kutengeneza ajira baadaye.

Kwa nini? Na kwa jinsi gani?

Kwa sababu elimu wanayoitoa shuleni, inapaswa kutafsiriwa kwenye maisha ya kawaida ya huku mtaani. Kwa hiyo kama kila mwanachuo, akitoka chuoni na kitu kimoja amnacho anaweza kupambana nacho huku mtaani, ataweza kuwasaidia hata wale aliowaacha nyumbani.

Sasa kinachotokea sasa hivi ni kwamba wale waliosoma, wanarudi tena nyumbani na wanaanza kuwategemea wale waliowaaacha.

Hiki kitu unaweza usiambiwe na walimu wako, lakini unapaswa ukijue. Jua kabisa kwamba unaposoma, hata kama mwalimu wako anakwambia soma bidii ili uje upate ajira. WEWE badili hilo liwe kwamba nasoma kwa bidii ili nije niajiri.

#3. Lengo la elimu ni kukusaidia kutengeneza konekisheni.

Iko hivi, unapokuwa unasoma kwanza unakutana na watu wengi. na kila mtu ana kipaji chake na uwezo wake. sasa hili ndilo lengo la shule. Kwamba liwakutanishe watu wenye vipaji vyenu, halafu muone namna ambavyo mnaweza kuunganisha vipaji vyenu kwa manufaa makubwa.

Ila sasa hili halitokei kwa sababu, vipaji na uwezo havipewi kipaumbele kwenye mfumo wa elimu uliopo. Ndio maana mtu anasoma mpaka chuo kikuu, lakini ukiumuuliza kipaji chake hajui.

Lakini, ukiweza kukutana na watu ambao wana vipaji na mkaweza kuunganisha nguvu kwa pamoja. YAANI, kiufupi mkaendana au mkaivana, basi ujue mtaweza kufika mbali.

Halafu konekisheni haiishii kwa wanafunzi wenzako tu, hata kukuunganisha na walimu wako na hata watu wenye fikra za tofauti kabisa na wewe. Hii yote inakusaidia wewe kuuona ulimwengu katika namna ya kipekee na kuchukua maamuzi sahihi.

Kuna konekisheni ambazo unaweza kuzitengeneza wakati wa kusoma zikaja kukusaidia baadaye. Pengine wewe kwenye kusoma umependa kuzama zaidi kwenye mambo ya uzalishaji wa viungo (spices) kama mimi. Na mwezako amependa kuzama kwenye sheria. Baadaye huyu mwanasheria anaweza kukusaidia wewe wakati unaajiri kwenye kuweka mikataba.

Hata kama utamlipa, lakini kwa kuwa ni miongoni kwa konekisheni ambayo uliwahi kuitengeneza wakati unasoma, basi utakuwa na uhakika kwamba hapa nasaidiwa na mtu sahihi. Na siyo magumashi, anaweza pia kukusaidia kupooza bei kidogo…

Hiki kitu ninachosema hapa unaweza usikielewe vizuri, lakini ulimwengu wa sasa umeanza kuonesha kuwa kweli hiki kitu kinafanya kazi kweli.

Mfano mzuri tu, siku hizi mtandaoni kuna hivi vitu tunvyoviita aplikesheni.

Unaweza kukuta kuna aplikesheni labda inayohusika na masuala ya uhasibu. Kama THL (watu wa THL mkisoma hapa, mnitumie vocha maana nimewarusha hewani leo)

Sasa kutengeneza aplikesheni kama hii ya THL inayohusika na utunzaji wa kumbukumbu za kihasibu, kunahitaji walau muunganiko wa watu wa aina mbili.

Kwanza ni wahasibu

Na pili ni watalaamu wa teknlojia.

Hizi ndizo konekisheni zenyewe, ambazo unaweza kuzipata ukiwa shuleni. Kwa hiyo wewe wakati unasoma, unaweza kugundua kwamba mtu fulani yuko vizuri kwenye kitu fulani, na mimi niko vizuri kwenye hiki kitu, basi tukiungana na kuunganisha haya maujuzi yetu, tunaweza kutengeneza kitu fulani ambacho kitakuwa na manufaa kwenye jamii.

Mimi ni daktari, na jamaa mwingine ni mtalaamu wa teknolojia, tunaweza kuunganisha udaktari na teknojia tukawasaidia watu wengi zaidi.

Daah, hapa nimemkumbuka jamaa mmoja. Ofcourse kinyozi. Hivi anaitwa kinyozi au fundi kinyozi, au basi…

Huyu jamaa alikuwa anataka kuunganisha utalaamu wake wa kunyoa na teknoljia. Yaani, kwamba ukienda saloon kwake anachukua namba yako, ukishaondoka tu kuna mfumo wa kiteknolojia unakutumia ujumbe wa kukushukuru kwa kuweza kufika ofisini kwake kunyoa, baada ya wiki mbili mfumo huo unakukumbusha urudi kunyoa maana zimepita siku tangu unyoe…

Sasa mtu kama huyu anahitaji konekisheni. Anahitaji kuunganishwa na mtu mwenye uelewa wa haya mambo ili amwezeshe kutengeneza mfumo wa aina hii…

Sijui unanielewa? Kama umenielewa mpaka hapo, gonga cheers!

#4. naamini kwamba chuo kipo kwa ajili ya kukupa maarifa sahihi unayoyahitaji kwenye maisha ya baada ya chuo.

#5. shuleni na chuo ni kwa ajili ya kukufundisha wewe kusoma na kuandika, sasa jukumu lako baada ya kumaliza shule ni kujiendeleza kwenye kusoma na kuandika.

Shuleni unafundishwa kusoma na kuandika. Si ndio? Tatizo la watu wengi wanapomaliza shule, ndio wanaona kwamba hakuna haja ya kusoma tena. Hawajifunzi kitu chochote kipya.

Kitu hiki kinawafanya waendelee kuwa na maarifa yaliyopitwa na wakati. Sikiliza. Shuleni unafundishwa kusoma na kuandika. Ila sasa kwenye maisha ya kawaida ya huku mtaani unapaswa kusoma na unapaswa kuandika pia.

Ebu fikiri amtu aliyesomea kompyuta mwaka 2010. Kama mtu huyu hajajiendeleza kuongeza maarifa na kujifunza zaidi, lazima tu ameshapitwa na wakati. unajua kwa nini? kwa sababu kompyuta zinabadilika kwa kasi, na na kuna vitu vingine vinazidi kugunduliwa sasa hivi.

Mtu aliyosoma kompyuta 2010 atakuwa hakujifunza mambo ya roboti kama yalivyo sasa hivi. lakini kama wewe ukiwa ni mtu wa kujiupdate na kujifunza zaidi kila siku. Hata baada ya chuo, hutahangaika, maana utakuwa unapata ujuzi na kuelewa kinachoendelea. Na utakuwa unaweza kutumia hiki kitu unachojifunza kwenye maisha ya kawaida.

Hayo ndiyo nilivyokuwa nayo moyoni kuhusu chuo na wqnachuo kwa leo. Nina mengi Ila sasa nikiyabwaga hapa tote, hayataleta maana. Nadhani siku nyingine jamaa akinichokoza kwabkuniuliza swali kamablanleo nitaandikia ena Kitu kingine.

Ila jamani nisitize. Endelea kusoma, soma kwa bidii ila fikiria nje ya ajira. Kama umenielewa share makala hii na watu wengine ili nao wanufaike.

Mpaka wakati mwingine

Mimi ni Godius Rweyongeza kutoka SONGEMBELE CONSULTANTANCY


4 responses to “Je, Kuna Haja Ya Kuendelea Kusoma Wakati Ajira Hakuna?”

  1. Sir Godius ( I have decided to call you sir ). What I can do is to say YOU’RE CHANGING MY LIFE” Thanks

  2. Habari kaka Godius, hakika mawazo yako yataendelea kuishi katika vizazi vingi hapa duniani… unazidi kutufumbua vijana kwa mawazo chanya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X