UCHAMBUZI WA KITABU; THE 5 AM CLUB, Miliki asubuhi yako, miliki maisha yako


Kitabu Cha THE 5 AM CLUB kilitoka katikati ya mwezi Wa 12, 2018. Binafsi, nilianza kukisoma wiki moja baada ya kutoka na nimekuwa nikikifanyia uchambuzi katika kundi LA HAZINA YETU TANZANIA.

Mpaka ninaanza uchambuzi Wa Kitabu hiki nimesoma vitabu vingi sana, ila usomaji Wa Kitabu hiki umekuwa Wa kipekee sana.
Kwa Mara ya kwanza nimeandika mambo mengi sana ambayo nimejifunza kwenye Kitabu hiki kuliko ambavyo nimewahi kuandika kwenye Kitabu kingine.

Imefikia hatua nikaacha kuandika maana kila kitu  kilikuwa ni pointi. Nimeandika mambo 120 ambayo nimejifunza kwenye Kitabu hiki. Ila kwa Leo nitakushirikisha mambo 50! Ukitaka kusoma mambo mengine 70 basi utapaswa kujiunga na kundi la HAZINA YETU TANZANIA.

Karibu kwa uchambuzi huu.

UCHAMBUZI WA KITABU; THE 5 AM CLUB,

Miliki asubuhi yako, miliki maisha yako.

Mwandishi Robin S. Sharma

Robin Sharma amekuwa ni mwandishi wa vitabu ambavyo vimegusa maisha ya watu wengi sana. Uandishi wa Robin ni uandishi wa hadithi ambao unavuta watu wengi sana. Vitabu vyake vya
1. The Monk Who Sold His Ferrari,
2. The Leader Who Had No Title na
Vinginevyo vingi vimekuwa ni vitabu bora sana kwa watu wengi sana.

Binafsi nashauri kila mwenye kiu ya kufanikiwa asome vitabu hivyo, ikiwa ni pamoja na
👉Who Will Cry When You Die
👉 The Greatness Guide
👉The Litlle Black book of Stunning Success.

Sasa leo hii Robin Sharma anakuja kwako kupitia Kitabu cha The 5 Am Club. Karibu sana kwa uchambuzi, ikiwa Ni sehemu ya kwanza.

1. Kuna watu wanaishi wiki moja mara elfu, lakini bado hayo wanayaita maisha!

2. Kuna watu wanakufa wakiwa na miaka 30 na kuzikwa wakiwa na miaka 80

3. Maisha yoyote utakayoamua kuishi lazima utakutana na changamoto tu.

4. Kamwe, usikubali vikwazo vya jana na leo viharibu kesho yako inayong’aa

5. Kama unaona maisha yako hayafai sasa hivi basi jua kwamba uoga wako umekuwa na nguvu kubwa sana kuliko imani yako ya kusonga mbele.

6. Kila changamoto ambayo umekutana nayo, kila mtu ambaye amekuwa akikurudisha nyuma, kila kitu ambacho uliona ni kibaya, kilikuwa ni njia ya kukufanya wewe uwe jinsi ulivyo leo.

7. Wewe  hujatokea kama ajali hapa duniani. Kuna sababu maalumu. Nguvu iliyokuleta haikupotea bure, kuna sababu.

8. Mawazo hayana maana yoyote labda yawekwe kwenye vitendo.

9. Kuishi maisha ya viwango vya juu sio suala la mchezo mchezo. Linahitaji kujitoa.

10. Uwezo mkubwa unaupata kuanzia pale mazoea yako yanapoishia.

11. Mafanikio makubwa yanahitaji kujitoa. Na ukitaka kujua hili waangalie akina Darwin, akina Michael Angelo, akina Newton. Hawa ni watu waliojitoa haswa kuhakikisha wanafanya kile walichoamua.

12. Jamii yetu inatuaminisha kwamba kutaka kuwa mkubwa ni ujinga. Ila inatuaminisha kufanya ujinga ndio ujanja. Ndio maana ukiwa mtu wa mitandao utaonekana bingwa ila ukiepukana na mitandao utachekwa sana.

13. Haijalishi watu wanakukataa mara ngapi, usikate tamaa songa mbele.

14. Huhitaji watu millioni kukufanya utimize makubwa, anahitajika mtu mmoja kukwambia songambele.

15. Sehemu ambayo wewe unakuwa na hofu kubwa sana ya maisha yako hapo hapo ndipo kwenye mafanikio makubwa sana ya maisha yako.

16. Kama unakufa, basi kufa ukiwa unafanya kitu cha kishujaa sana.

17. Usiogope kufanya kitu leo eti kwa sababu hakikubaliki. Kisichokubalika leo, kitakubalika kesho.

18. Katika maisha usikubali kuzungukwa na vilaza. Huwezi kuwa gwiji ukiwa umezungukwa na vilaza.

19. Maisha ni mafupi kuyatumia na watu Wa kawaida sana. Tumia muda wako na watu wanaofanya makubwa, ishi na watu wanaokufanya uzidi kusonga Mbele. Tembea na watu ambao wanakufanya upate nguvu zaidi Kila wakati. Kula vyakula vinavyokupa nguvu, tembelea sehemu ambazo hata watu wakikukuta waseme kweli unatembelea sehemu za maana sana.

20.  Unapaswa kuweka nguvu yako katika kutumikia zaidi. Pesa na  umaarufu vitafuata Nyuma yako.

Soma Zaidi; UCHAMBUZI WA KITABU: WEALTH OF NATIONS-11

21. Ulipokuwa mtoto ulikuwa unaishi uwezo wako. Ila dunia ilipoanza kukuaminisha kwamba wewe hauna maaana, wewe huwezi kufanya makubwa, wewe huwezi kusonga Mbele, basi hapo ndipo umeanza kuishi maisha ya kawaida.

22. Ukitoa jasho sana kwenye mazoezi, utatoa damu kidogo wakati wa vita.

23. Ushindi mkubwa unapatikana asubuhi, Kila mtu akiwa amelala.

24. Tunasikia kile ambacho tupo tayari kusikia, kujifunza kwetu ni matokeo ya utayari wetu. Mwanafunzi anapokuwa tayari, mwalimu hujitokeza.

25.  Kila mtaalamu unayemwona leo Kuna siku alikuwa anajifunza.

26. Huwa tunawashangilia watu maarufu kwa kudhani kwamba wamezaliwa na vimelea vya kipekee. Ila ukweli ni kwamba Nyuma ya USHINDI wao, kuna kujituma, Kutoka jasho, kuumia na kuanguka.

27. Mtu wa kawaida anaweza kufanya mambo yasiyo ya kawaida endapo ataamua kupangilia mambo yake vizuri.

28. Elimu ndio mwangaza wa maisha, Ila elimu binafsi ndiyo elimu pekee unayoihitaji.

29. Kila mtu amezaliwa kuacha historia, japo historia itatofautiana kati mtu mmoja na mwingine. Kwa mwingine historia inaweza kuwa ni kuwa baba bora au mama bora, kwa mwingine ikawa ni kuwa ni mwandishi bora, kwa mwingine ikawa ni kuwa meneja bora. Tafuta eneo lako ambalo utaacha historia yako, tafuta eneo ambapo utaandika jina lako.

30. Kuna watu wanajitahidi kadri ya uwezo wao kuhakikisha kwamba wanaficha uwezo wao, ukuu wao na majina yao. Hakikisha sio wewe.

31. Usitumie muda mwingi kujionesha kwamba upo bize, fanya vitendo.

32. Kuna wakati utapaswa kuwaachia watu waendelee na maisha yao, kwa sababu watu ambao ni muhimu katika hatua moja ya maisha, kuna wakati huwa wanapoteza umuhimu wao na hivyo unahitaji kuwatafuta wengine.

33.  Unapofanya kitu, kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Usikubali kuacha kitu kama ambavyo umekikuta.

34. Hakikisha kila siku unajifunza kitu kipya, jifunze jifunze jifunze. Siku ukiacha kujifunza itakuwa siku uliyoamua kujichimbia kaburi.

35. Mtu pekee wa kulalamikia maishani mwako ni wewe mwenyewe.

36. Kila mara toa huduma kubwa zaidi ya vile unavyolipwa.

37. Kama unatumia simu yako kwa muda mrefu sana jua kwamba kuna vitu vingi sana vya kibunifu unavivyima muda wako.

38. Vikwazo sio kitu, isipokuwa ni majaribio ambayo yameandaliwa ili wewe uweze kudhihirisha ni kiwango gani unahitaji kile unachohitaji.

39. Vikwazo vinakuandaa ili pale utakapokutana na mafanikio uwe katika hali ya ya kuyapokea kwa mikono miwili.

40. Watu wanafikiri kuibadilisha dunia ila hawafikirii kujibadili wenyewe. Kama unataka kuibadili dunia anza kujibadili mwenyewe.

41. Kama haukui kila siku, kuna sehemu utakwama katika maisha.

42. Kitu kibaya kwenye maisha sio kifo, ila kile kitu kile tunachoruhusu life kikiwa ndani yetu.

43. Ukitaka kuwa na uhusiano mzuri na watu, anza kuwa na uhusiano mzuri pamoja na wewe.

44.  Watu wengi hupoteza muda wao wakiangalia runinga. Madhara yake sio kupoteza muda tu, Bali hata kufukarika kichwani na mfukoni.

45. Kama mambo hayakaa sawa jua mwisho wako haujafika. Songambele.

46. Muda mzuri wa kuishi ndoto zako ni sasa hivi. Kuna watu wanaishi zaidi ya nusu karne wakijaribu kuwavuta watu kwao, wakiishi ndoto za watu wengine, wakitafuta kukubalika n.k
Muda mzuri wa kuishi ndoto zako ni sasa hivi, bila kujali upo katika mazingira gani.

 47.  Mabadiliko yote ni magumu mwanzoni, yasiyotamanika katikati ila rahisi mwishoni.

48. Kama kitu hakijawahi kufanyika haimaanishi hakiwezi kufanyika. Kinaweza kufanyika na mtu wa kukifanya ni wewe.

49.  Kila siku katika maisha yako utakutana na nafasi ambayo unahitaji uoneshe uongozi wako. Hapa utapaswa kuuonesha kweli

50. Watu wengi wanakosea kwa kudhani kwamba uongozi ni cheo, ofisi, vitu vizuri na mafaili ya kila aina. Huo sio uongozi.

Ndimi,
Godius Rweyongeza
0755848391

KUPATA KITABU CHA KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI BONYEZA HAPA


HUDUMA NYINGINE UNAZOWEZA KUPATA KWANGU HIZI HAPA

KUPATA MAKALA MAALUM KWA WATU MAALUM KILA WIKI BONYEZA HAPA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X