Hii ni maalumu tu kwa ajili ya yule ambaye anahitaji mafanikio makubwa kama ambavyo anahitaji hewa
Siku moja kijana mmoja almfuata Socrates akimwomba amfundishe siri ya mafanikio. Socrates hakuwa mchoyo, hivyo alichofanya alimpangia miadi siku iliyofuata.
Kweli bwana, kijana alitokea kama ambavyo alikuwa amepangiwa. Socrates alimwambia kijana yule kwamba nifuate. Kijana alimfuata Socrates nyuma. Baada ya mwendo wa maili kadhaa walifika kwenye mto. Socrates aliingia kwenye maji huku akimwambia kijana amfuate, kijana aliendelea kumfuata kwa umakini. Walipofika katikati ya maji, Socrates alimshika kijana kwa nguvu na kumzamisha kwenye maji. Kijana hakutegemea kufanyiwa kitu hicho. Hivyo alianza kutapa tapa ili walau aweze kutoka kwenye maji. Lakini bado, Socrates aliendelea kumshikilia kijana yule kwenye maji kwa nguvu zake zote. Kijana alipoona kwamba hapa asipojinusulu anakufa maji. Alijikomba komba na kutumia nguvu zake zote, kumsukuma Socrates kisha akafanikiwa kutoka ndani ya maji.
Baada ya kutoka kwenye maji, Socrates alimwuliza, ni kitu gani ulikuwa unahitaji sana ulipokuwa majini. Kijana yule aliwambia kwamba alikuwa anahitaji zaidi kupata hewa. Basi Socrates alimwambia kwamba, kama una mpango wa kufanikiwa, hakikisha unatafuta mafanikio kwa bidii kama ambavyo ulikuwa unatafuta Pumzi wakati upo majini. Siri ya mafanikio ya ikawa imetolewa tayari.
Sasa tunajifunza nini kutokana na kitu hiki hapa.
Kuna vitu vingi sana vya kujifunza kutokana na kisa hiki hapa, ila kwa siku ya leo kuna vitu hivi
1. kama kuna kitu ambacho unahitaji kukipata, basi unapaswa kuweka nguvu zako, akili yako, mawazo yako na kila rasilimali uliyonayo kuhakikisha kwamba unakifia kitu hicho hapo. Kijana ameonesha hilo pale alipoona kwamba hataweza kuachiwa na atakufa maji. Amejikomba kwa nguvu alizokuwa nazo ili aweze kujiokoa/ kujinasua.
2. ukihitaji mafanikio kama ambavyo unahitaji kupumua basi ni wazi kwamba hakuna mtu ambaye atakuwa na uwezo wa kukuzuia kupata mafanikio ambayo wewe unataka. Maana ukihitaji mafanikio kwa kiwango hicho maana yake, utaweka nguvu zako zote, akili yako, mawazo yako, na kila rasilimali.
3. Mwanafunzi anapokuwa tayari, basi mwalimu hutokea. Ni wazi kamba Socrates kama mwalimu alikuwepo muda wote, ila yule mwanafunzi hakuwa tayari. Ila kipindi alipokuwa tayari basi huo ndio ulikuwa ni mwanzo wa yeye kupata mwalimu sahihi.
Vivyo hivyo kwako, maarifa unayohitaji sasa hivi, yapo yamekusubiri tu. ukiwa tayari kujifunza kuhusu kitu fulani ndio waalimu hutokea.
Rafiki yangu upo tayari kuendelea kujifunza kanuni za mafanikio basi BONYEZA HAPA ili uendelee kupata kanuni hizi kila siku.
4. unahitaji kuwa na mshauri ambaye atakuonesha uhalisia wa safari ambayo unaiendea. Kijana alimfuata Socrates ili aweze kumsaidia kwa kile ambacho alihitaji kufanikisha. Wewe pia kuna nyakati utamhitaji mtu.
5. kuna nyakati unaweza kwenda kutafuta kitu kikubwa maeneo mengine kumbe kitu hicho unacho. Kijana alienda kutafuta jibu la kufanikiwa kwa Socrates, kumbe jibu lenyewe lilikuwa ndani yake. Hivyo ni muhimu kuwa unajipa muda wa kukaa na wewe na kujiuliza maswali mengi bila huruma kuhusu hali yako ya maisha. Hali yako ya kazi. kwa nini unafanya kazi kwa namna ambavyo unafanya sasa hivi? Kwa nini unaingia mtandaoni bila mpangilio?
Jiulize maswali haya kisha ukipata majibu yafanyie kazi bila kuchelewa.
Rafiki, naamini kwamba kidokezo hiki hapa kimeweza kukufundisha mengi ambayo na wewe pia unaenda kufanyia kazi. nikusihi sasa uyaweke kwenye matendo haya mambo uliyojifunza.
Kila la kheri.
SOMA ZAIDI: Hii ni kwa wale wanaohitaji mafanikio kama vile wanavyohitaji kupumua
umekuwa nami rafiki yako
Godius Rweyongeza