Jinsi ya kufanyia wazo majaribio kwenye soko


Nakumbuka nikiwa mwaka wa kwanza wa masomo yangu ya shahada ya kilimo cha bustani, nilikuwa napenda sana kupiga hesabu za mazao mbalimbali ya kilimo na baadhi ya rafiki zangu kwa wakati huo. Kila tulipokuwa tukikaa na kupiga hesabu za zao fulani, ilikuwa inaonekana faida tu, tena faida kubwa sana. Nakumbuka kwa mfano siku moja tulipiga hesabu za kilimo cha nyanya,

  • gharama za kuweka zikawa kama milioni nne na nusu,
  • hlafu fedha yote iliyokuwa inapatikana baada ya mauzo ilikuwa ni milioni saba na nusu hivi,
  • ulipokuwa ukitoa gharama zote ulikuwa unabaki na kama milioni tatu au milioni na mbilinusu hivi.

Hizo zilikuwa ni hesabu za kwenye karatasi, “tena unapata hela yako ndani ya miezi mitatu tu”, tulikuwa tunajiambia. Ukipiga hesabu hizo na kuona fedha inavyopatikana unaweza kesho yake kuamkia benki kuwaambia wakupe mkopo wa milioni tano, kwa uhakika kuwa utarudisha hela yao na ya ziada ndani ya miezi mitatu tu.

Usicheke kuna jamaa baada ya kupiga hesabu kama hizi alienda baa kujipongeza kwanza, akawa amekunywa fedha yote ikaishia huko…Tutacheka baadaye ngoja tuendelee kwanza.

Kama umewahi kuwa na wazo lolote lile maishani, utakuwa unakubaliana nami kuwa wazo ni kitu kimoja na kulifanyia na kuliweka kwenye uhalisia ni kitu kingine. Mara nyingi ukiwa na wazo la biasahra utakuta kwamba kinachokuja kwenye akili yako kwanza ni upande wa faida, unafikiri na kuona ni kwa namna gani utapata faida, unaona kwamba ukifanyia kazi wazo lako na kufanya kitu fulani na kitu fulani muda siyo mrefu utakuwa uemeweza kutengeneza fedha nyingi sana.

Lakini sasa ajabu ni pale unapoamua kuingia kwenye ulingo wa kufanyia kazi kile ambacho umeamua kufanyia kazi, hapo ndipo utakutana na uhalisia. Mambo mengi ambayo hapo mwanzo hukuyatarajia yatatokea. Ndiyo maana wahenga wanasema kwamba utamu wa ngoma sharti uingie ucheze.

Ukifuatilia takwimu za kibishara zinaonesha kwamba asilimia 5 tu ya biashara huwa zinaendelea kuwepo baada ya mwaka mmoja. Yaani, kama zikianzishwa biashara 100 biashara 95 huwa zinakufa ndani ya mwaka mmoja na ni biashara tano tu ndizo huwa zinaweza kuendelea baada ya kipindi hicho.

Unajua kwa nini?

Kuna sababu nyingi sana ambazo zimetolewa kuelezea jambo hili hapa ila mojawapo ya sababu ambazo unapaswa kuifahamu ni kuwa ni rahisi kuwa na wazo ila unapoanza kulifanyia kazi ndio unaona uhalisia wa kitu hicho na hapo ndipo watu wengi huwa wanakimbia. Unaweza kuona kwamba ukitengeneza bidhaa fulani itakuwa yenye manufaa na kuwasaidia watu, ukipiga hesabu za kwenye karatasi unaona unaenda kupata hela nyingi sana ila sasa ingia mchezoni uone…

Asa ufanyeje unapokuwa na wazo/

KITU CHA KWANZA KABISA NI KULIFANYIA KAZI.

Ukiwa na wazo, hakikisha kwamba unalifanyia kazi na kuliweka kwenye uhalisia. Kwa vyovyote vile hata kama bado hujawa anza kulifanyia kazi. utajifunza mengi zaidi kadiri utakavyokuwa unalifanyia kazi kuliko pale ambapo utakuwa hujalifanyia kazi.

Kwa mantiki hii nitachukulia kuwa una wazo la kuandika kitabu au kuwa mwandishi mbobevu. Unafanyaje? Kitu cha kwanza ni wewe kuanza kulifanyia kazi wazo lako la kuandika. Anza kuandika hata kama ni makala fupi na kuziweka mtandaoni. Fungua blogu na weka makala zako huko. Usisubiri mpaka uwe tayari, wewe anza tu.

Mpaka hapo umeshafaulu

PILI Pata mrejesho na ufanyie kazi

Kadiri utakavyokuwa unafanyia kazi wazo lako watu wataanza kukupa mrejesho, kuna wale ambao watakuuliza maswali. Kuna ambao watataka kujua zaidi kuhusu kitu fulani, na mengineyo. Pokea hiyo mirejesho na kisha ona ni kwa namna gani unaweza kuifanyia kazi.

Kwa mfano wetu wa wewe unayetaka kuwa mwandishi, pale ambapo utakuwa umeanza kuandika kwenye blogu, watu wataanza kuuliza maswali, haya maswali utakuwa ukiyajibu na utaona kwamba kuna aina fulani ya maswali yanaulizwa zaidi. Utayafanyia kazi hayo maswali na hata kutengeneza kitabu chako.

Hapo sasa utakuwa umejibu maoni ya wasomaji wako kitalaam.

TATU; Kusanya mawasiliano ya watu ambao wanaweza kuwa wateja wako wa wa kwanza. Kama unaandika ni rahisi sana, unaweza kutengeneza mfumo wa barua pepe wa kupokea makala ambapo watu wanajiandikisha ndipo wanapata makala hizo .

NNE, tengeneza bidhaa kisha ijaribishe kwa watu wachache wa kwanza

Baada ya kuwa umeanza kufanyia kazi wazo lako na kupata mrejesho, sasa kifuatacho ni wewe kutengeneza bidhaa kulingana kile ambacho umekuwa unafanya sasa kwa muda. Na bidhaa hiii unaweza kuitengeneza kulingana na maswali ambayo watu wamekuwa wanakuuliza kwa wingi sana. kwa hiyo kama sehemu ya kujibu maswali haya hapa tengenez bidhaa yenye suluhisho.

Na vile ulishakuwa na orodha ya watu ambao unaweza kuanza kuwaauzia sasa unaweza kuwattumia hawa watu

TANO, uza bidhaa kwa watu wengi zaidi

Sasa baada ya kuwa umefuata hizo hatua zote hapo juu kifuatacho ni wewe kuhakikisha unaenda mbali na kuuza bidhaa yako kwa watu wengi zaidi. na hapa unaweza kwenda mpaka kuanza kuitangaza bidhaa yako kwa watu wengine zaidi

Kama unavyoona, hizo ni hatua muhimu unazopaswa kufuata kulitoa wazo katika wazo na kulileta uhalisia. Hatua hizi zinatekelezeka, ni jukumu lako sasa kuhakikisha kwamba umeziweka kwenye uhalisia.


2 responses to “Jinsi ya kufanyia wazo majaribio kwenye soko”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X