Jinsi Ya Kuanza Biashara Na Mtaji Kidogo Mpaka Kuikuza Kuwa Bisshara Kubwa


Siku moja nilikuwa naangalia mtandaoni, nlikutana na picha iliyokuwa inaonesha kampuni ya azam ilivyoanza kama mgahawa, ambao ulikuwa unahudumia katika mkoa wa Dar Es Salaam. Ambapo walikuwa wanafanya huduma za Catering na huduma nyingine zinahousisha hilo.

Picha hiyo ilikuwa ni picha ya tangazo ambalo walifanya mwaka huo. Kama sijakosea ule mwaka uliooneshwa kwenye ile picha ulikuwa ni 1984. Sijaweza kupata  tena ile picha wakati naandika makala hii hapa, lakini endapo utaipata unaweza kuituma kwangu kupitia whatsap 0755848391 au godiusrweyongeza1@gmail.com

Sasa leo hii nataka niongelee jinsi na wewe unavyoweza kuanza bishara na mtaji kidogo na kuikuza kuwa biashara kubwa

Kwa wenginen wanaweza kuona hili kama ndoto fulani ya Habunwasi …

Wanaweza kuonakama vile ni kitu ambacho hakiwezekani. Yaani, kwa wengine hata ufanyeje, mafanikio yamewekwa kwa ajili ya watu wachache na wengine wapo hapa duniani kuhangaika.

Kitu hiki siyo kweli hata kidogo, wewe mwenyewe unaweza kuanzisha biashara hata kama utaanza nayo kidogokidogo, lakini bado ukaweza kuifikisha kwenye viwango vikubwa. zifuatazo ni hatua ambazo unapaswa kufuata kwenye hili hapa.

KUWA NA NDOTO KUBWA

Ili biashara ndogo iweze kufikia kuwa biashara kubwa unapaswa kuwa na ndoto kubwa kwanza. Watu wengi hawawezi kukuza biashara zao kwa sababu tu wanakuwa hawana maono makubwa tangu wanapoanzisha biashara.  Wengi wa watu ambao unaona kwamba biashara zao ni za kawaida miaka nenda miaka rudi ni kwa sababu tu wanakuwa hawana ndoto kubwa tangu wanaanzisha biashara hizo.

Unakuta mtu anaanzisha biashar kwa ajili tu ya kupata hela ya kula na kutunza familia yake. Biashara ya aina hii ni ukweli kwamba usitegemee itafika mbali. Badala yake itaendelea kuwa biashara ya kawaida kila wakati.

Na muda mwingine hata itakuwa inafilisika na mwenye biashara anatakiw kuanza upya kwa kuingia mfukoni kutoa hela ili kuiamusha tena. Sisemi kwamba ukiwa na ndoto kubwa kitu kama hiki hatitatokea, ila ninachotaka ufahamu ni kwamba, usipokuwa na ndoto kubwa, kila kitu ambacho utafanya kitakuwa ni cha kawaida kwa sababu tu huna ndoto kubwa.

KUANZA KIDOGO

Ndio unapaswa kuwa na ndoto kubwa, ila ndoto kubwa peke yake tu haitoshi. Ndoto inapaswa kuwekwa kwenye vitendo kwa kufanyiwa kazi.

Kuwa na ndoto kubwa kuhusu biashara yako, ila anza kuifanyia kazi kidogo kidogo kadiri unavyokuwa unaenda.

TUNZA HESABU ZA BIASHARA YAKO

Mali bila kalamu huisha bila habari. Hiki ni kitu kikubwa ambacho huwa kinawafanya wafanyabiashara wengi waendelee kufanya biashara zao kwa namna ambayo ni ya kawaida sana kwa siku nyingi kiasi kwamba wanakuwa hawapati matokeo ambayo wanatakiwa kupata.

Biashara ni hesabu. Mara zote na muda wote tunza hesabu za biashara yako.

Kama unakwama na unajiuliza wapi unaweza kuanzia kwenye kutunza hesabu za biasahara yako, anza na kutunza hesabu za mapato na matumizi. Kiasi ambacho unaingiza na kiasi ambacho kinatoka, hivyo tu. Fanya hiki kwa mwezi mmoja, utakuwa tayari umeshakuwa mtaalamu wa biashara yako.

Tayari utakuwa unajua fedha inayoingia na fedha ambayo inatoka kwenye biashara yako. Na hicho ndiyo kitu kikubwa ambacho unahitaji walau kwa kuanzia.

FANYA BIASHARA KWA UTOFAUTI NA WASHINDANI WAKO WANAVYOFANYA

Angalia vitu ambavyo washindani wako wanafanya kwa namna ambayo ni ya kawaida, kisha wewe anza kuvifanya kwa namna ambayo ni ya tofauti kidogo. Kwa mfano, suala la kutunza mawasiliano ya wateja wako na kuwasiliana nao mara kwa mara linaweza kuleta matokeo na utofauti mkubwa kwenye biashara yako.

Lakini pia kama washindani wako wanachelewa kufungua na kuwahi kufunga, wewe kwako hili linaweza kuwa jambo la faida pia. Unaweza kuitumia nafasi hiyo kuanza kufungua mapema na kuchelewa kufunga kidogo ili kuwanasa wateja wanaokuwa wanadamka au wale wateja wanaofanya manunuzi wakiwa wamechelewa.

JIFUNZE KWENYE BIASHARA NYINGINE

Maisha yetu ya kila siku yanatufanya twende kwenye biashara nyingi sana. unapopanda daladala ujue kwamba unakuwa umepanda biashara ya mtu. Na hapo unaweza kujifunza kwa konda ambaye kwake kila mtu anayemuona ni mteja wake. anamkaribisha kwenye gari ili waondoke. Utasikia kondakta anasema unaenda dada, au kaka au mjomba

Muda mwingine unaweza kushuka kwenye gari na bado konda akakukaribisha tena upande ili mwende ruti nyingne. Wewe pia, kuwa mtu wa kuwakaribisha watu.

Jifunze kwa mtu wa mapokezi kwenye ofisi yoyote utakayoingia.

Ukienda kwa mama ntilie akakuwekea chakula kingi, jifunze kwake pia huku ukijua kwamba kwenye hoteli kwa hela hiyohiyo usingeweza kupata chakula kingi kama hicho.

Ukienda sehemu ukapata huduma nzuri, jifunze na wewe unaweza kuitumia kwenye biashara yako pia.

Ukienda sehemu ukapata huduma mpya mpaka ukachoka, jifunze hapo pia na lifanyie kazi hilo ili lisije kujitokeza tena kwenye biasahara yako.

Na kwa hapa kwetu Tanzania biashara zenye huduma mbaya ni nyingi, hivyo ukijifunza kutokana na mabaya ambayo biashara nyingine zinafanya na kuyafanya kuwa mazuri kwenye biasahra yako, utaweza kufika mbali sana.

IWEKE BIASHARA YAKO MTANDAONI

Tunaishi kwenye ulimwengu ambapo karibia kila biashara inapaswa kuhamia mtandaoni. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu sasa hivi wakitaka kitu, sehemu ya kwanza kabisa ambapo wao wanakimbilia ili kupata taarifa ni mtandaoni

Wewe kwa sasa unaweza kuona kwamba biashara yako haistahili kuingia mtandaoni, ila siyo kweli. Ndio maana kitu cha kwaza kabisa unapaswa kuanza na maono, hivyo kitu kikubwa tunachokiangalia, siyo biashara yako ya sasa hivi, ila biashara ya miaka kumi ijayo. Ndio maana tumesema uwe na maono makubwa.

SOMA ZAIDI:

KUZA BIASHARA YAKO KWA ASILIMIA MOJA KILA SIKU

Ukifuatilia kampuni kubwa, utagundua kwamba huwa zinatoa ripoti ya mwenendo wake kila baada ya miezi mitatu. Wewe pia unapaswa kufanya hivi.

Ndio maana nimekwambia kwamba unapaswa kutunza hesabu za biashara yako. Huo utakuwa ni mwanzo wa wewe kuona hatua unazopiga.

Lakini pia jenga utaratibu wa kujiwekea malengo ya utakayofanyia kazi ndani ya miezi mitatu ijayo.

Weka malengo ya kufanyia kazi ndani ya mwezi ujao na wiki moja ijayo.

Usisahau kuweka malengo ya kila siku.

Ukiwa na malengo, lazima tu utafika mbali, ila usipokuwa na malengo, jua kwamba kila kitu unaenda kukifanya kwa namna ya ukawaida, na hapo utakwama kwenya safari yako na hutafika mbali.

KUWA MTU WA KUJIFUNZA NA KUTUMIA MAARIFA UNAYOPATA

Biashara yako itaweza kukua kulingana na kiwango cha maarifa uliyonayo. Hivyo penda sana kujifunza mara kwa mara. Soma vitabu, vitakuwezesha wewe kupata maarifa utakayoweza kutumia kwenye biashara yako.

Mkurugezi wa kawaida anakadiriwa kusoma vitabu 52 kwa mwaka. Sasa jiulize wewe unasoma vitabu vingapi kwa mwaka?

Anza na kusoma kitabu hiki cha BURE HAPA

Rafiki yangu, hivi ni  baadhi ya vitu kidogo vinavyoweza kukusaidia wewe kukuza biashara yako na kuifanya kuwa kubwa. unaweza kuviona vya kipuuzi hivi, ila ni hivi hivi vinavyotofautisha kati ya wafanyabiashara wanaokuza biashara zao na wale ambao wanazidi kubaki pale pale mwaka hadi mwaka.

Ebu nenda uvijaribu kwenye biashara walau kwa mwezi mmoja tu, halafu uje hapa kutupa mrejesho.

Bila kuongeza la ziada, napenda kukushukuru sana kwa wakati wako. Nakushauri sana usome kitabu cha MAMBO 55 YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZISHA BIASHARA, KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI pamoja na kitabu cha JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO.

Mimi ni Godius Rweyongeza

0755848391

Morogoro-Tz


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X