Mashindano ya olympiki ni miongoni mwa mashindano yenye nguvu sana. Yanapendwa na watu lakini pia washiriki wake huwa wanajiandaa kwa kipindi kirefu kabla ya mashindano yenyewe. Washiriki wa mashindano hayo wanajiandaa kila siku kwa kipindi cha miaka minne kwa ajili ya shindano ambalo linadumu kwa dakika kadhaa kisha kupotea. Na ndani ya dakika hizo ndipo mshindi huwa anapatikana na kupewa zawadi nono.
Sasa swali langu kwako siku ya leo ni kwamba je, na wewe upo tayari kuweka kazi na juhudi kwa kipindi cha miaka minne, mitano sita mpaka kumi mfululizo kabla ya kupata matokeo na kula vinono ambavyo ungependa kupata? Unapaswa kuwa tayari kufanya hivi kwa sababu mafanikio makubwa huwezi kuyapata kwa usiku mmoja tu. Mafanikio makubwa ni matokeo ya vitu vidogo vidogo ambavyo unafanya kila siku vikiunganishwa kwa pamoja. Usiidharau siku moja na kukaa ukisubiri ufike mwisho wa mwaka ambapo utapata mafanikio makubwa, badala yake fanya kitu leo. Ukiunganisha hivi vitu vidogo vidogo, mwishoni mwa mwaka utakuwa umeweza kufanya makubwa.
Kazi ya kufanya siku ya leo.
Andika chini vitu vidogo ambavyo unaenda kufanya siku ya leo kulingana na lengo lako la mwaka huu. Kisha vifanyie kazi. endelea kufanya hivyo kila siku kwa siku 365 zijazo.