Ninaandika hii makala tukiwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa waislam.
Kwa kawaida baada ya mfungo wa Ramadhan ndio huwa zinafuata sherehe za Idd. Hakuna mwaka hata mmoja nimewahi kusikia waislam wamesherehekea Idd bila ya kufunga kwanza. Haijawahi kutokea na wala haitakuja kutokea.
Kwa kawaida siku ya Idd huwa ni sikukuu kubwa, ambayo inatanguliwa na siku 30 za kufunga kwanza.
Hiki kitu kinanifunza kuwa hakuna zuri ambalo huwa linatokea tu hivihivi bila ya kuandaliwa. Badala yake kila zuri huwa linaandaliwa tena siyo kwa siku moja, huwa linaandaliwa kidogokidogo.
Hakuna mtu AMBAYE anaweza kususa kufunga, halafu akasubiri siku moja kabla ya Idd na akafunga kwa ajili ya siku zote za nyuma ambazo hakufunga. Badala yake unapaswa kufunga kila siku kwa siku 30 mfululizo. Hiki kitu kinanifundiaha kuwa fanya ufanyavyo, kwa majukumu ambayo unapaswa kuyafanyia kila siku, usikose kuyafanya.
Hiki kitu pia kinatumika kwenye maisha ya kawaida. Huwezi kwa mfano kuweka malengo yako ya mwaka. Na kukaa chini ukisubiri uje kuyafanyia kazi mwishoni mwa mwaka. Ni lazima kila siku ufanye kitu kuelekea kwenye malengo yako. Ule muunganiko wa vitu vidogo unavyofanya kila siku, ndio mwisho wa siku unakuwezesha wewe kufikia malengo yako.
Kwa hiyo kwa kitu chochote kikubwa ambacho unataka kufanya, fikiria namna ambavyo unaweza kuanza kukifanya kwa kuanza kidogo, Kisha ukakiendeleza zaidi na zaidi ya hapo.
Vitu vyote vikubwa Kuna wakati vilikuwa vidogo. Walau mfano mzuri tu ambao watu huwa wanatokea ni mfano wa Mbuyu, kuwa ulianza kama mchicha.
Kikawaida Mbuyu ni mkubwa, Ila huwa hauoti kwa siku moja tu. Unaota kwa siku nyingi sana. Hakuna siku moja kwenye ukuaji wa Mbuyu ambayo inaweza kujigamba kuwa yenyewe ndiye ilifanya mti ukue. Maana uwepo wa siku moja ndio chanzo Cha uwepo wa siku nyingine na ndio ukuaji wake unaendelea.
Kuna watu wamekuwa wanabeza suala zima la kuanza kidogo kwa kutaka waanzie juu. Na wengine kwa kutaka wafanye makubwa kimiujiza. Kama kuna muujiza unauhitaji kwenye maisha yako, Basi Ni muujiza wa kutumia vizuri siku moja moja unayokutana nayo maishani mwako.
Kila siku weka akiba hata Kama ni kidogo. Baada ya muda hicho kidogo litakuwa kikubwa
Kila siku soma kitabu hata Kama ni kurasa kidogo, baada ya muda hizo kurasa chache zitakuwa nyingi na zitakuongea maarifa ya kutosha. Nashauri uanze kwa Kusoma kitabu cha JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO. Kutakusaidia sana kufanya makubwa.
Ni Mimi rafiki yako
Godius Rweyongeza kutoka SONGAMBELE
Tuwasiliane kwa 0755848391
Morogoro-Tz