Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Mtaji Tanzania


Utangulizi

Vijana wengi wamekuwa wakitamani kuanzisha biashara zao ila sasa wamekuwa wanakwama jinsi gani ambavyo wao wenyewe wanaweza kuanzisha hizo biashara bila ya mtaji.  Kila  ninapoongea na vijana nagundua kuwa wapo wengi wenye ndoto kubwa za kufanya makubwa ila kuna ambao kama bado wamefungwa hivi. Na kitu ambacho kimewafunga walio wengi ni kufikiri kuwa bado unahitaji mtaji fedha mkubwa ili kuanzisha biashara.

Zama Zimebadilika

Kwenye zama za viwanda mtaji fedha kilikuwa kitu muhimu sana kilichokuwa kinahitajika. Ili kununua vifaa na kila kitu kilichokuwa kinahitajika viwandani, ulipaswa kuwa na fedha nyingi za kukusaidia kufanikisha hilo.

Ila sasa mabadiliko mengi yanetokea kwenye zama za sasa. Ni kweli bado kuna biashara ambazo bado zinahitaji mtaji fedha mkubwa. Ila pia kuna biashara ambazo zinahitaji mtaji fedha kidogo na nyingine hazihitaji mtaji fedha kabisa.

Kama huwezi kuanza biashara kwa ukubwa, Anza kwa udogo

Kwa kawaida watu huwa hatukosi visingizio. Watu wana visingizio kwa nini maisha yao ni mabaya, kwa nini hawajatoboa…
Kuna watu wana kisingizio mpaka kwa nini hawakuwahi kulala jana usiku, wakati walikuwa wanaangalia tamthiliya, loooh!

Ngoja nikwambie kitu, visingizio haviwezi kuleta chakula mezani. Unachopaswa kufahamu wewe ni kwamba, pale unapogundua kuwa una ndoto kubwa au lengo kubwa la kufanya biashara,  ila kwa sasa unaona  mtaji fedha hautoshi.

Fanya hivi, amua kitu kimoja. Amua kwamba ninaenda kufanya hiki kitu hata kama Ni kwa udogo.
Kama huwezi kufanya kitu kwa ukubwa, amua kukifanya kwa udogo. Huwezi kushindwa vyote.

Juzi nilikuwa nasoma ujumbe wa Ryan Holiday. Kwenye ujumbe huo akawa anaeleza kwamba alikuwa na ndoto ya kuanzisha duka la vitabu.  Ila alipoingia mtandaoni akaona gharama zilizokuwa zinahitajika kifungua duka la vitabu ni kubwa, akaamua kuwa kwa lengo lake ni kuanzisha duka la vitabu. Bado tu atapaswa kulianzisha Hilo duka. Na kwa kuwa hawezi kuanzisha duka la vitabu kwa ukubwa , anaweza ataanza kwa udogo huohuo alionao. Na atautumia udogo huohuo kuwafyekelea mbali washindani wake.

Unaona eeh…

Yaani, kwake hiyo ikawa tayari fursa…

Na wewe udogo wa mtaji wako ni Fursa.

Badala ya kufikiri uanzishe biashara itakayoshughulika na kila kitu. Anzisha biashara ambayo utajikita kwenye kitu kimoja au viwili ambavyo vinapendwa sokoni. Kisha pambana….

Nakumbuka mwaka mmoja wa nyuma hivi nilikuwa naongea na rafiki yangu Edius Katamugora.

Akawa ananiambia kuna mtu ana duka la vitabu linalouza kitabu kimoja tu…

Yaani, yeye ukiingia kwenye duka lake unakutana na aina moja ya kitabu. Kama ni KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI, Ni hicho tu. Kama ni JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO ni hicho tu.

Binafsi nimewaona watu wanaouza vitabu vya mwandishi mmoja tu.

Kwa hiyo Kama mtaji fedha kwako bado ni tatizo, FIKIRI TENA! Kuna njia nyingi ambazo unaweza kuanzisha biashara kwa udogo au hata bila mtaji kabisa.

Nadhani kinachokukwamisha wewe siyo mtaji
Maana mitaji unayo ya kutosha. Kinachokukwamisha wewe ni udhubutu.

Ungana na watu wenye mitaji

Kuna watu wana mitaji ila hawajui wanaweza kufanya nini. Unaweza kuungana na hawa watu na wenyewe wakakupa fedha. Hata hivyo, kwenye hili unapaswa kuwa umeonesha uaminifu wa hali ya juu. Vijana wengi wa siku hizi siyo waaminifu.

Nakumbuka mwaka juzi tu, kijana mmoja ambaye binafsi nilikuwa namfahamu vizuri. Alikusanya vijana wengine wanne, hivyo jumla wakawa watano. Wakaja na wazo la kuanzisha kampuni ya kilimo cha mboga. Wakaenda kwa mtu mwenye mtaji fedha Sasa. Wakampanga akapangika…

Wakakubaliana makubaliano ya kwanza…
Wakaelekezana kuwa vijana wale watano wangekuwa na umiliki wa asilimia 60 ya kampuni wakati mwekezaji akichukua asilimia 40.

Mipango ya kulima kitaalamu ikawekwa wazi na kazi ikaanza…

Kazi ilianza wakati mipango mingine ya kukamilisha kusajili kampuni ikiendelea..

Yule mwekezaji akatoa milioni saba ya kwanza na kumpa kiongozi wa wale vijana… Mara baada ya kiongozi kupokea hiyo fedha akatokomea kusikojulikana na hiyo fedha. .
Akawaacha wenzake solemba…

Mpango ukashindwa kufanyiwa kazi tena…

Moja ya zao walilopaswa kulima mwaka huo lilikuwa ni nyanya…
Na ninadhani sote tunakumbuka nyanya ilivyokuwa dili mwanzoni mwa 2020… Ila jamaa alishatokomea

Ninachotaka kusisitiza hapa ni UAMINIFU. Ukimpata mtu wa kuwekeza fedha kwako, zitumie vizuri fedha zake na kwa uaminifu.

Ukifanya vitu vidogo, kwa uaminifu vina uwezo wa kukufikisha mbali….

Tumia Mali kauli


Unaweza pia kutumia mali kauli kwenye kuanzisha biashara. Ukawa unachukua bidhaa za wafanyabiashara dukani kwao na kuziuza kwa faida kidogo, kisha ukawarejeshea fedha za bidhaa walizokupa.

Na hapa pia bado unapaswa kuwa mwaminifu.

Kama wewe siyo mwaminifu, Anza walau leo…

Kila la kheri..
Umekuwa nami
Godius Rweyongeza
0755848391
Morogoro-Tz


One response to “Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Mtaji Tanzania”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X