UKIANGUKA SIMAMA TENA


Usijivunie kuwa hujawahi kushindwa, bali jivunie kuwa ulisimama tena baada ya kuwa umeanguka-Ralph Waldo Emerson

Ni vibaya kushindwa, ila ni vibaya kama hujwahi kujaribu na kushindwa-Theodore Roosevelt

Mtu pekee ambaye hajawahi kufanya makosa ni yule ambaye hajawahi kufanya chochote-Theodore Roosevelt

Sikushindwa mara 10,000 bali nilijifunza njia 10,000 za kufanya kitu kwa usahihi-Thomas Edison

Mambo yakienda vibaya, yaache yaende peke yake-

Mtu aliyeshindwa kuliko wote ni yule ambaye hajawahi kujaribu kitu-Dr. Larry Kimsey

Ili mtoto aweze kutembea vizuri na kuwa mbobevu, basi anapaswa kuanza kwa kuanguka na kusimama tena na kuanguka tena. Hakuna mtu ambaye huwa anamcheka mtoto kwa sababu ameanguka chini wakati akijaribu kutembea. Kila mtu huwa anafurahia kwamba mtoto huyu ameweza kujaribu kutembea, japo ameanguka. Hiyo ni ishara kwamba huyu mtoto ana uhai ndani yake.

Ila mtoto ambaye hata haoneshi dalili za kutembea ni wazi kuwa anawatia mashaka wazazi wake. Sasa hili linapaswa pia kuwa kwako.

Ukiona kwamba hauna changamoto wala hujashindwa kwa lolote, basi fahamu kuwa kuna sehemu unakosea. Kuna hatua hauchukui. Kufanikisha ndoto zako sio kitu rahisi.

Kuna mtu mmoja aliwahi kunukuliwa akisema kwamba; nilipogundua kwamba katika vitu tisa ninavyofanya ninafanikisha kitu kimoja tu, basi niliongeza juhudi katika vile vitu ambavyo nilikuwa nafanya.

Pengine na wewe unaweza kukuta kwamba unapaswa kufanya vitu mara kumi ili kufanikiwa kwa kishindo mara moja. Usichoke kuinuka hata baada ya kuanguka na kuendelea mbele.

Kitu pekee unachopaswa kuondoka nacho kwenye kuanguka kwako ni somo la kufanyia kazi. Kumbuka kwamba kushindwa sio mwisho wa safari bali unakuwa unajifunza njia sahihi za kufanikisha hicho kitu. Mafanikio ni asilimia 1 ya kushindwa ambako ni asilimia 99, kama alivyowahi kusema Thomas Edison mgunduzi wa karne ya 21.

Sasa inashangaza kwenye maisha ya kila siku kwamba kuna watu ambao wanaogopa kuanguka na hivyo kuficha makosa ili wasionekane kwamba walishindwa au kuna wakati walifanya uamuzi mbovu. Hata ukiangalia wasifu wa watu mbalimbali, huwa ni wasifu chanya wakionesha vitu ambavyo watu hao wameweza kufanikisha na kufanya kwa ubora na huku wakiepuka kutaja vile vitu ambavyo walifanya hovyo. Ila ukweli ni kuwa hata kwa vile vitu ambavyo huwa unafanya hovyo, huwa kuna kitu cha kujifunza na kuchukua hatua.

Hivyo, ukianguka au ukifanya kitu hovyo, usianze kutafuta sehemu ya kujificha ili usionekane. Badala yake jiulize ni kitu gani ambacho umejifunza kutokana na kuanguka huko, kitu ambacho kitakusaidia wewe kusonga mbele na kufanya mambo mengine makubwa zaidi. Ukijifunza kutokana na kushindwa kwako unakuwa hujashindwa. Kitu kingine unachopaswa kufahamu ni kuwa kushindwa ni tukio ila sio wewe. Pia, unapaswa kufahamu kuwa kuna watu wengi ambao hata hawajajaribu kufanya hicho ulichoshindwa.

Baba mkubwa wangu aligombea udiwani 2010 akashindwa, aligombea tena 2015 akashindwa, alirudia tena 2020 na kushindwa. Watu wengi walikuwa wanamcheka na kusema kwamba anapoteza muda na fedha zake. Hata hivyo, nilikuja kugundua kuwa asilimia kubwa ya watu waliokuwa wanamcheka kuwa ameshindwa na anapoteza fedha zake hawakuwa watu ambao wangeweza kuchukua hatua kama zake. Hivyo, kwangu alikuwa mshindi mara mia zaidi ukilinganisha na hawa watu waliokuwa wanakaa vjiweni kumbeza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X