Helo leo ninayo furaha kutambulisha kwako kitabu cha Nguvu ya vitu vidogo kuelekea mafanikio makubwa. Ni kitabu cha kipekee sana. kabla sijasema mengi kuhusu kitabu hiki, nataka nikupe kwanza utangulizi wa kitabu ili uweze kuuusoma. Karibu
Hivi umewahi kujiuliza kuwa vitu vidogo vinaweza kukusaidia kitu gani maishani mwako?
Hivi kwa mfano, kitu kidogo kama kuamka asubuhi na mapema kinaweza kukusaidia nini maishani mwako kikifanywa kila siku na kwa mwendelezo? Au je, kitu kidogo kama kuwekeza au kuweka akiba kikifanywa kila mara kwa muda mrefu kinaweza kukusaidia nini? Kwenye kitabu hiki hapa tunaenda kuona nguvu ya vitu vidogo na jinsi nguvu hii inavyoweza kukusaidia wewe kufikia mafanikio makubwa maishani mwako.
Mara nyingi sana watu huwa wana ndoto kubwa na malengo makubwa ya kufikia kifedha, kimahusiano, kibiashara au kikazi. Lakini cha kushangaza ni kwamba huwa hawafanyii kazi hizo ndoto kubwa walizonazo bali huwa wanasubiri itokee siku moja ya muujiza ambapo ndoto yao itatimia kwa asilimia zote.
Kitu kama hiki hapa hakiwezekani. Ni wazi kuwa lengo lako la mwaka haliwezi kutimia siku ya mwisho ya mwaka baada ya wewe kuwa umekaa mwaka mzima bila ya kufanya kitu chochote, badala yake kama kweli utaweka kazi na kufuata hatua zote unazopaswa kufuata ili kulifikia hilo lengo lako la mwaka basi utalifikia kwa kufanya vitu kidogo kidogo kila siku.
Kitu chochote kikubwa kinaweza kufanikishwa kwa kuchukua hatua ndogondogo na kwa mwendelezo na hatimaye kuzifanya ziwe hatua kubwa. Mafanikio makubwa siyo kufanya vitu elfu moja mara moja, ila kufanya vitu vidogo mara elfu moja, yaani, kwa mwendelezo na bila kuchoka. Hivi vitu vidogo hatimaye vinapelekea kitu kikubwa na mafanikio makubwa.
Confucius, mwanafalsafa wa Kichina aliwahi kunukuliwa akisema kwamba, “safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja”. Hii ndiyo kusema kwamba mambo makubwa siku zote huwa yanaanza kwa hatua ndogondogo kisha kuendelea kukuzwa. Hakuna kitu kikubwa ambacho unakiona leo hii ambacho kilianza kikiwa kikubwa hivyohivyo. Ndiyo maana wahenga walisema kwamba; “hata mbuyu ulianza kama mchicha.” Jogoo anayewika kuna siku alikuwa kifaranga.
Ukitaka kugundua kwamba vitu vikubwa huanza kwa udogo basi unaweza kuangalia ujenzi wa ghorofa. Huwa unaanza kwa hatua ndogo ndogo za kuchimba msingi, baadaye huwa wanaanza kuweka jiwe au tofali moja baada ya jingine hatimaye kitu kilichokuwa chini huwa kinaendelea kusimama na kufikia hatua ya kuwa kitu kikubwa sana.
Siku moja nilikuwa nasoma historia ya jengo ambalo limo kwenye maajabu saba ya dunia. Jengo hili siyo jingine bali ni jengo la Taj Mahal. Hili ni miongoni mwa majengo yaliyojengwa kwenye karne ya 15, na jengo lenye historia ndefu na kubwa sana. Unajua jengo hili lilijengwa kwa miaka mingapi? Unaweza kuwa sahihi. Lilijengwa kwa miaka ishirini na mbili (22). Kila siku watu walikuwa wanaweka tofali moja, siku nyingine tofali jingine, siku nyingine nondo, hatimaye lile jengo lilikamilika baada ya miaka 22!
Wajenzi hawakusubiri mwaka wa 22 ili wajenge hilo jengo. Ila walikuwa wakilifanyia kazi hilo jengo hatua kwa hatua kila siku bila kuchoka. Hili nalo litupe picha ya kuwa vitu vikubwa vinawezekana kufanyika na kuja katika uhalisia endapo vitafanyiwa kazi kwa kuanza kidogo kidogo, na kwa mwendelezo na kupewa muda ili viweze kuanzia chini na kukua.
Usidharau vitu vidogo. Kuna mfano, wa nyuki aliyeingia kwenye sikio la tembo na kuanza kupiga kelele. Tembo yule alianza kuruka huku na kule ili nyuki yule atoke kwenye sikio lake ila nyuki hakutoka. Tembo alianza kuangusha miti na kujibamiza kwenye miti pengine akidhani kwamba huyo nyuki atatoka ila huyo nyuki hakutoka. Baada ya muda mrefu wa kuhangaika, tembo alianguka na hivyo akawa amepoteza maisha. Kinaweza kuonekana kama kitu cha kushangaza, ila vitu vidogo muda mwingine huwa vina madhara makubwa sana.
Mbu ni wadogo, ila madhara yake ni makubwa. Sindano ni ndogo sana ila ikikuchoma, wewe mwenyewe ni wazi kuwa utakipata cha mtema kuni. Kwa hiyo basi, nikuombe kuwa ujenge utaratibu wa kuheshimu vitu vidogo maana vinaweza kukupelekea kwenye mafanikio makubwa au la vikakupelekea kwenye anguko kuu maana kuna nguvu katika vitu hivi vidogo. Nguvu hii inaweza kukuinua ukiitumia vizuri ila ukiitumia vibaya itakuangusha. Na nguvu hii ndiyo tunaenda kuiona kwenye kitabu hiki hapa.
Endapo utakisoma kitabu hiki na kuanza kufanyia kazi yale utakayojifunza, sipati picha jinsi ambavyo utaanza kujenga six packs ambazo umekuwa unatamani kwa siku nyingi, akiba utakayoweka, vitabu utakavyoweza kuandika, utakavyoweza kukamilisha majukumu yako kwa wakati, jinsi utakavyoboresha mahusiano yako na mengine mengi.
Kila la kheri
Godius Rweyongeza
Februari 15,2020
Morogoro-Tz