Katika moja ya semina ambazo Zig Ziglar alikuwa anatoa kuna mtu mmoja ambaye alihamaki siku moja na kumwuliza, “hivi kwa nini hizi hamasa zenu huwa hazidumu?” Huku akiwa ametulia, Zig Ziglar alijibu kwa kusema kuwa hamasa ni kama kuoga, ukioga leo unapaswa kuoga na kesho. Tena wakati mwingine ukioga asubuhi utapaswa kuoga mchana na jioni au hata zaidi ya hapo. Hakuna mtu ambaye huwa analalamika kwa sababu ameoga mara nyingi. Kiufupi ni kwamba, usipooga kila siku utajikuta kwamba unanuka. Wewe mwenyewe bila kuambiwa na mtu yeyote utajistukia na kuanza kuwaogopa watu. Ni kitu gani kinakufanya uogope watu na kushindwa kuchangamana nao. Jibu ni kwa sababu hujaoga na unatoa harufu. Sasa inapokuja kwa hamasa inakuwa hivyo hivyo. Hamasa haidumu, hivyo inapaswa kuchochewa kila siku. Kuna watu wengi wamesahau ndoto za maisha yao, kwa sababu tu ya kukosa hamasa ya kuziendea ndoto zao. Zipo njia kadha wa kadha za kuongeza hamasa, ila moja ya njia hizo ni kusoma vitabu ambavyo vinaokuongezea hamasa ya kufanya makubwa. Tayari nimeakuandikia kitabu cha Jinsi Ya Kufikia Ndoto Zako, kitabu ambacho kinaeleza kwa kina jinsi ambavyo unaweza kufikia ndoto zako. Sasa kwenye kurasa za kitabu hiki unaenda kukutana na tafakari fupi ambazo utakuwa unasoma kila siku kabla ya kwenda kufanyia kazi ndoto yako na hivyo kupata hamasa na nguvu ya kuendelea kufanyia kazi ndoto zako. Ikumbukwe kwamba, hamasa sio kitu ambacho kinadumu, hivyo kila siku utahitaji kuendelea kujihamasisha na kitabu hiki kitakuwa kimbilio lako mara nyingi tu.
Kwenye kitabu hiki kuna tafakari 366 sawa na tafakari za mwaka mzima mrefu. Kama unasoma kitabu kwenye mwaka mfupi, yaani, mwaka ambao tarehe 28 ndio mwisho wa mwezi wa pili, basi tafakari ya tarehe 29 mwezi wa pili utairudisha nyuma siku moja au kuipeleka mbele siku moja. Hivyo, kutakuwa na siku ambapo utasoma tafakari mbili.
Kila tafakari imeanza na nukuu na mwishoni mwa kila tafakari nimekuwekea hatua ya kuchukua. Hizi ni hatua ambazo unaweza kufanyia kazi mara moja tu.Yaani, kuanzia leo hii. Ni imani yangu kuwa ukifanyia kazi utakayojifunza humu basi utaweza kufika mbali sana. Kila la kheri.
Godius Rweyongeza
Morogoro
21 Novemba 2020