NGUVU YA KUFANYA MAZOEZI


Ukitoa jasho jingi wakati wa mazoezi, utavuja damu kidogo wakati wa vita

Siku moja rafiki yake Kobe Bryant alimtembela Kobe,  sasa wakati wanaongea wakawa wamekubaliana kuwa kesho yake alfajiri yule rafiki yake Kobe ambaye pia alikuwa kocha angekuja kushirikiana na Kobe kwenye kumsaidia kufanya mazoezi. Wakawa wamekubaliana muda wa kukutana ambao ulikuwa ni saa kumi alfajiri sana. Kisha wakaagana, wakati wanaagana yule rafiki yake Kobe Bryant alimwacha Kobe anafanya mazoezi.

Rafiki yake Kobe Bryant alikuwa na uhakika kuwa Kobe hawezi kuamka na kuwahi kesho muda huo waliokubalilana, hivyo hata kesho yake alivyokuwa akielekea uwanjani alikuwa na uhakika kabisa kuwa Kobe hawezi kuwa amefika uwanjani, ila cha kushangaza ni kuwa alikuta kobe tayari ameshafika uwanjani akiwa anafanya mazoezi. Lakini kilichomshangaza zaidi ni kuwa Kobe Bryant alionekana kama mtu ambaye alikuwa akifanya mazoezi kwa muda mrefu kabla yake. Kadiri rafiki yake huyo alivyofuatilia alikuja kugundua kitu kimoja kikubwa sana, aligundua kuwa kobe Bryant alikuwa ni mmoja wa watu ambao walikuwa wanathamini sana mazoezi na hivyo alikuwa anaweka nguvu kubwa sana kwenye kufanya mazoezi.

Moja ya kitu ambacho watu wengi huwa wanachukulia poa sana ila nimekuja kugundua kuwa watu ambao wanafanya vizuri karibia kwenye kila sekta wanakitumia ni kufanya mazoezi ya kutosha nyuma ya pazia. Hiki ni kitu cha kushangaza sana, ila ni kitu ambacho kinafanya kazi na ni kitu ambacho wewe mwenyewe unahitaji kuhakikisha kwamba unakifanyia kazi kwenye maisha yako.

Lakers at Wizards 12/3/14

Kobe Byrant

Mazoezi yanakujenga

Sina shaka umewahi kusikia usemi kwamba practice makes perfect. Yaani, kwamba mazoezi ndiyo yanakuimarisha na kukufanya kuwa bora zaidi. kuna siku nilikuwa nasoma kitabu cha Steve Jobs, kinaitwa Presentation Secrets of Steve Jobs.

Ujue Steve Jobs ni miongoni mwa watu ambao walikuwa akitoa hotuba za kipekee sana kwenye maisha yake. Hotuba zake zilikuwa zikivutia watu kiasi kwamba watu walikufunga safari kutoka mbali na tena wengine walikuwa wakilipia miezi mingi kabla ya siku yake ya kutoa hotuba ili tu wapate viti vya mbele siku anapotoa hotuba.

Hata leo hii ukifuatilia hotuba zake mtandaoni, utagundua kuwa ni miongoni mwa hotuba chache ambazo zimeangaliwa mara nyingi zaidi kuliko waneni wengine. Sasa nini siri iliyo nyuma ya hotuba hizi? Siri kubwa sana iliyo nyuma ya hotuba hizi ni kuwa, Steve Jobs alikuwa akifanya mazoezi na kujiandaa kwa siku nyingi kabla ya siku yenyewe ya tukio. Unaambiwa alikuwa akijiandaa kwa siku `100 kabla ya siku yenyewe ya hotuba.

Mtu akikukwambia siku 100 za maandalizi kabla ya siku ya hotuba unaweza kuchukulia poa, ila ukweli ndio huo. Mazoezi ni moja ya kitu muhimu zaidi kwenye kitu chochote kile unacahofanya.niambie kitu chochote kile unachotaka kufanya, nami nitakwambia kwamba fanya mazoezi.

 • Unataka kufaulu mitihani, basi fanya mazoezi mengi kabla ya siku za mitihani.
 • Unataka kujifunza lugha ya kigeni kama kiingereza, kifaransa, kichina au kiarabu, basi fanya mazoezi ya kutosha.
 • Unataka kunoa kipaji chako na kukifanya kiwe bora zaidi, fanya mazoezi.
 • Unataka kuandika maandiko mazuri kama mimi, basi fanya mazoezi.

Kwa kitu chochote kile unachotaka kufanya na kukifanikisha kwa viwango vikubwa basi fanya mazoezi.

Kijana mmoja siku moja alisikia stori ya Michael Jackson, ujue michae Jackson ni mmoja wa wasanii ambao wameacha alama kubwa mpaka leo na mpaka leo hii bado anakumbukwa sana kwa miziki yake na jinsi ambavyo alikuwa akitikisha dunia kwa miondoko yake kwenye muziki.

Sasa kijana huyu aliambiwa kuwa Michael Jacksoni alikuwa akifanya mazoezi kwa saa zaidi ya 8 kila siku, alishangaa sana. Tena alianza kubisha kwa kusema kwamba Michael Jackson alikuwa mchezaji (dancer) kwa asili hivyo hakuhitaji kufanya mazoezi. Ila ukweli unabaki kuwa mazoezi ndiyo mama wa kila kitu.

Watu wengi unaowaona kwamba wana vipaji vya asili kabisa, au vipaji vya kuzaliwa navyo, siyo kwamba walizaliwa wakiwa hivyo, bali ni mazoezi ya kutosha ndiyo yanawafanya waweze kuwa walivyo.

Unachopaswa kufahamu ni kuwa kuna watu wengi sana ambao wana vipaji ila hawajaweza kufanya vizuri kwa sababu tu hivyo vipaji vyao hawakuvifanyia mazoezi. Mazoezi kwenye maisha ndiyo kila kitu.

Ebu chukulia mfano tu wa kawaida wa mchezaji wa mpira aliye kwenye timu ya taifa ni wazi kuwa kabla ya kucheza kwenye timu ya taifa anakuwa tayari ameshachezea timu nyingi sana huku nyuma ya pazia. Na kama ni mazoezi anakuwa ameshafanya mengi na ya kutosha, lakini kadiri anavyokua anakuwa ndivyo anaongeza mazoezi zaidi kwenye kile anachofanya.

Ndiyo maana utasikia kuwa timu ya taifa imeweka kambi eneo fulani, lengo lake likiwa kwamba wachezaji wake waweze kufanya mazoezi.

Wachezaji kama akina Ronaldo au Messi, mbali na umaarufu wao wote, ila bado leo hii wanaendelea kufanya mazoezi mengi na ya kutosha bila ya kurudi nyuma. Hiki kitu kinatuonesha kuwa kama kuna siri ya pekee ambayo tunahitaji kuikumbatia basi ni kufanya mazoezi.

Mazoezi yanakujengea kujiamini

Kadiri unavyofanya mazoezi zaidi, ndivyo unavyoongeza kujiamini kwenye kile ambacho unafanya. hivyo basi kama unataka kujiamini zaidi, ongeza mazoezi ambayo unafanya. Na hili lipo wazi kabisa, kama kuna watu wawili ambao wanapaswa kusimama mbele ya watu na kuongea, mmoja akajiandaa kwa siku nyingi nyuma ya pazia.

Akafanya mazoezi kwa kujiuliza maswali ambayo watu wanaweza kumuuliza wakati anawasilisha mada yake na hata kuyaandalia majibu, akajipanga atakavyowasilisha pointi moja baada ya nyingine, lakini pia akajipanga mpaka namna atakavyovaa siku ya tukio. Na mwingine akapuuzia kufanya maandalizi na mazoezi, mpaka dakika za mwisho kabla ya kusimama mbele ya watu ndio akaanza kujiandaa. Ni wazi kuwa aliyejiandaa kwa siku nyingi atakuwa anajiamini zaidi kuliko yule ambaye hakujiandaa.

Mazoezi yanakujegea kujiamini

Kanuni muhimu kwenye mazoezi

Kama kuna kitu muhimu sana ambacho unahitaji kukifahamu linapokuja suala zima la mazoezi ni kuwa, usifanye mazoezi unapojisikia kufanya mazoezi. Usifanye mazoezi mara moja kisha kusahau na kuja kufanya mazoezi siku nyingine nyingi za baadaye.

Mazoezi yanapaswa kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku. Kadiri kitu unavyokuwa ukiyafanyia kazi ndivyo ambavyo unakuwa unazidi kuimarika zaidi na zaidi kwenye hicho kitu. Hivyo, kitu kikubwa na cha msingi ni kuwa usisubri mpaka siku ambapo utaweza kufanya mazoezi kwa mara moja, tu endelea kufanya mazoei kila siku bila ya kurudi nyuma. Yafanye mazoezi kuwa sehemu ya pili ya maisha yako.

Fanya mazoezi kwa bidii zako zote, ila unapoenda kuonesha kitu ulichofanyia mazoezi kifanye kama vile umezaliwa nacho.

Tayari tumeona kuwa hakuna mtu ambaye anazaliwa akiwa anajua kila kitu kiasi kwamba hatahitaji kufanya mazoezi. Tayari tumeona kuwa watu wote wanaofanya makubwa kwenye kila sekta wanafanya mazoezi makubwa nyuma ya pazia. Yaani, wanafanya mazoezi mpaka ile dakika ya mwisho.

Sasa siku siyo nyingi kuna kitabu nilikuwa nasoma, japo sikumbuki vizuri ni kitabu gani na wala sikumbuki jina la mhusika aliyedokezwa kwenye kile kitabu, ila ninachokumbuka kwenye kile kitabu walikuwa wakimwonglea mwigizaji mmoja ambaye alikuwa akifanya vizuri sana.

Yaani, kuna igizo moja ambalo alikuwa akiliigiza kwenye kila jukwaa, na watu wengi walikuwa wakilipenda. Sasa baada ya igizo hilo kuwa maarufu, mwandishi wa habari alienda kumhoji ili aweze kupata mawili matatu, kutoka kwa mwigizaji yule.

Hivyo, mwandishi alienda nyuma ya pazia (eneo ambapo waigizaji wanakaa kabla ya kuingia jukwaani kuigiza). Kilichomshangaza mwandishi wa habari ni kuwa alikuta mwigizaji yule akiwa bado anafanya mazoezi kwenye zile dakika za mwisho kabla ya kuonekana kwenye jukwaa. Hivyo, mwandshi wa habari alipaswa kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kuonana na mwigizaji, pale mwigizaji alipomaliza kufanya mazoezi, akiwa anaelekea jukwaani, ndipo mwandishi wa habari alipata kumuuliza swali. Inakuwaje unafanya mazoezi wakati umekuwa ukiigiza igizo hilohilo kila mara?

Yule mwigizaji alisema, kwa sababu mazoezi ndiyo yananifanya kuwa imara zaidi na yananifanya nijiamini ninapoenda kuigiza.

Rafiki yangu,  unaona ee, mazoezi yana nguvu kubwa sana.

Kama kuna vitu vitatu ambavyo ninaweza kukwambia uvipe kipaumbele kwenye maisha yako, kipaji chako, biashara yako n.k. basi vitu hivyo vitakuwa kama ifuatavyo,

 • Kwanza yatakuwa ni mazoezi
 • Pili ni mazoezi na
 • Tatu ni mazoezi

Naam, nne ni mazoezi tena. Usipuuze mazoezi maana mazoezi yana nguvu kubwa sana, hivyo usiyachukulia poa hata kidogo.

Kitu kimoja nilichokuja kujifunza kuhusiana na mazoezi ni kuwa unapaswa kufanya mazoezi ya kutosha nyuma ya pazia, ila unapoenda mbele ya watu wasilisha kama vile ulizaliwa hivyo. Wasilisha kama vile huwa hufanyi mazoezi.

Kufanya mazoezi ni mama wa kujifunza

Wakati nasoma O-level kuna mwalimu  mmoja ambaye alikuwa akipenda sana kutwambia usemi wa kilatini. Usemi huu unasema hivi, repetitio est mater studiorum. Ukimaanisha kuwa mazoezi ndiyo mama wa kujifunza au kusoma. Kadiri unavyofanya mazoezi zaidi, ndivyo unaimarika na kuwa bora zaidi, na kadiri unavyopuuzia mazoezi ndiyo unazidi kudorora.

Kiwango kimeshuka

Sina shaka umewahi kusikia watu wakisema kwamba mtu fulani kiwango chake kimeshuka siku hizi. Na hasa kwa wachezaji. Wengi huwa unakuta kwamba kiwango chao kinashuka kwa sababu tu kupunguza kufanya mazoezi au kutofanya mazoezi kabisa.

Mwingine huwa unakuta kwamba anapokuwa chini anakuwa anajituma sana anafanya mazoezi, ila kadiri anavyokuwa anazidi kukua na kufikia viwango vya juu, basi analewa ule umaarufu na fedha kitu ambacho kinamfanya aache kufanya mazoezi na mwisho wa siku anajikuta ameshuka kiwango.rafiki yangu, usikubali kiwango chako kishuke kwa sababu ya kutofanya mazoezi. Kumbuka mazoezi ndiyo mama wa ujuzi wowote unaotaka kujenga.

Upo tayari kujiandaa kwa miaka minne?

Mashindano ya olympiki ni miongoni mwa mashindano yenye nguvu sana. Yanapendwa na watu lakini pia washiriki wake huwa wanajiandaa kwa kipindi kirefu kabla ya mashindano yenyewe. Washiriki wa mashindano hayo wanajiandaa kila siku kwa kipindi cha miaka minne kwa ajili ya shindano ambalo linadumu kwa dakika kadhaa kisha kupotea. Na ndani ya dakika hizo ndipo mshindi huwa anapatikana na kupewa zawadi nono.

Sasa swali langu kwako siku ya leo ni kwamba je, na wewe upo tayari kuweka kazi na juhudi kwa kipindi cha miaka minne, mitano sita mpaka kumi mfululizo kabla ya kupata matokeo na kula vinono ambavyo ungependa kupata? Unapaswa kuwa tayari kufanya hivi kwa sababu mafanikio makubwa huwezi kuyapata kwa usiku mmoja tu. Mafanikio makubwa ni matokeo ya vitu vidogo vidogo ambavyo unafanya kila siku vikiunganishwa kwa pamoja. Usiidharau siku moja na kukaa ukisubiri ufike mwisho wa mwaka ambapo utapata mafanikio makubwa, badala yake fanya kitu leo. Ukiunganisha hivi vitu vidogo vidogo, mwishoni mwa mwaka utakuwa umeweza kufanya makubwa.

Siku moja Piccasso alikuwa akitembea mjini, alikutana na mama mmoja ambaye alimwomba amchoree picha. Kwa harakaharaka yule mama alichukua penseli na karatasi , kisha akampa Picasso. Picasso alichora hiyo picha ndani ya sekunde 30, ikawa imekamilika. Ilikuwa inapendeza sana. Sasa baada ya kuwa amemaliza kuchora hiyo picha, Picasso alimwambia yule mama kuwa hii picha ina thamani ya dola milioni moja.

Yule mama alishindwa kujizuia na kumwuliza, unafanyaje kuchora picha ndani ya sekunde 30 yenye thamani ya milioni. Na mimi ningependa kujifunza huu ujuzi ili niwe nalipwa milioni ndani ya sekunde thelathini.

Huku akiwa na tabasamu usoni, Picasso alijibu kwa kusema kuwa, imemchukua miaka thelathini ya mazoezi kuweza kuchora picha ndani ya sekunde 30 yenye thamani zaidi ya dola milioni moja.

Lada hapa swali langu kwako ni kuwa je, upo tayari kuweka muda wa kutosha kufanya mazoezi ili uweze kubobea kwenye ujuzi na kile ambacho umeamua kufanyia kazi?

Pablo Picasso katika ubora wake

Hivi Ndivyo Mazoezi Yanaweza Kukufanya Ule Meza Moja Na Mfalme

Katika mazingira yetu ya sasa hivi wafalme sio watu waliozoeleka sana kulinganisha na kipindi cha nyuma. Zamani kidogo ulikuwa unakuta kabila au nchi fulani ina mfalme wake ambaye watu wote wanamsikikiza na sauti yake iko juu kwenye masuala ya utawala.

Lakini pia mfalme kama kiongozi alikuwa anapata vitu vyote vizuri. Yaani kwake nguo zilikuwa ni nguo bora sana kuliko mtu mwingine, chakula chake kilikuwa ni chakula bora sana, malazi yake yalikuwa ni ya kipekee sana. Sio hivyo tu hadi usafiri wake ulikuwa ni wa kipekee, ardhi ya mfalme ilikuwa ni ardhi yenye rutuba kweli kweli. Kwa mazingira ya sasa hivi mfalme ndio raisi wa nchi.

Lakini kwa mantiki ya andiko hili mfalme sio rais tu. Naomba nitoe maana ya mfalme kulingana na ujumbe wa leo. Mfalme ni mtu ambaye amefikia mafanikio makubwa iwe ni kiuchumi, kiuongozi, kiroho, kimahusiano, n.k

Mtu ambaye wewe ungependa kukutana naye au pengine umekuwa na shauku ya kukutana naye kwa siku nyingi sana ila hutapata nafasi hiyo kutokana na utofauti uliopo kati yako na yeye kimafanikio.

Hawa ni watu ambao stori za kitaani huwa tunaishia kusema walikuwa na bahati. Pengine huwa tunasema walibahatika kurithi mali za mjomba, baba, shangazi au ndugu fulani. Au ni wale watu ambao wengine wanasema alikutana na jini likampenda basi likampa utajiri. Hahaha.
Na pengine wapuuzi wengine wanasema amejiunga freemason.

Je, kuna watu ambao umewahi kusema maneno kama haya juu yao. Je, kuna watu wa namna hii ambao ungependa kukutana nao ila hujui utawezaje? Leo hii ninakuja kwako na namna rahisi sana ya kukuwezesha kukutana na watu hawa na pia mbinu hizi zitakuwezesha kuwa mmoja wao.

Moja anza kwa kujiuliza una nini? Ni kitu gani ambacho unaweza kuanza nacho kikakusogeza mbele. Je, una kisomo fulani? Au una kipaji fulani? Au utaalamu fulani?

Ukishajua kile ulichonacho kinachofuata ni wewe kuamua kuwa gwiji kwenye hicho kitu. Usihangaike na mengine. Ebu tuchukulie mfano umejikuta wewe una ujuzi na kisomo cha sheria. Basi unaamua kukomaa hadi kuwa gwiji wa sheria. Mpaka kieleweke. Hakikisha kama katika nchi hii wanatafuta wanasheria watatu mabingwa basi na wewe unakuwepo. Suala hili halitakuchukua mwaka mmoja au miwili. Ni suala la muda mrefu. Kuanzia miaka saba mpaka kumi na tano!!!!!!!!!

Lakini ukiweza kutoboa hapa. Jua utakula meza moja na wafalme. Kwanza utakuwa mtu ambaye anafutwa sana jambo ambalo litapelekea wewe kulipwa sana. Jambo ambalo litapelekea wewe kupata vizuri sana ambavyo ulikuwa unatamani (gari, nyumba, n.k)

Jambo hili halitawasili kwako kirahisi rahisi kama unavyofikiri, litahitaji kuwekeza katika kusoma. Litahitaji pia uwekeze katika kufanya mazoezi ya kitu hicho.

Ebu tuchukulie mfano wetu hapo juu. Umejikuta una kisomo cha sheria, basi utapaswa kufanya mazoezi ya masuala ya sheria kila iitwayo leo. Utahitaji kusoma sana vitabu vya sheria kuliko mtu mwingine aliyekuzunguka. Kumbuka, ukitoa jasho jingi sana wakati wa mazoezi, utatoa damu kidogo wakati wa vita.

Huwezi kuwa komando kwa mazoezi ya mgambo

Wakati naelekea kumalizia andiko langu, ningependa kusistiza kitu kimoja. Kwa vile nimesema unapaswa kufanya mazoezi, usiishie tu kujionesha kuwa na wewe unaweza kufanya mazoezi, kama utaamua kweli kufanya mazoezi basi unapaswa kuwa tayari kufanya mazoezi kwelikweli kulingana na kitu chako. Ufanye mazoezi kulingana na kule unapotaka kufika. Ni wazi kuwa huwezi kuwa komando kwa kufanya mazoezi ya mgambo. Huwezi kuwa mwana

Sasa kabla sijamalizia kuna vitu muhimu hapa ambavyo ningependa kusisitiza kuhusu kufanya mazoezi.

 • Mazoezi yanaweza kukusaidia kufanya yasiyowezekana yakawa yanayowezekana.
 • Ukifanya mazoezi ya kutosha wakati wa amani, utatoka damu kidogo wakati wa vita.
 • Mazoezi yanakufanya kuwa imara zaidi.
 • Mazoezi yanaweza kukufanya ufikie kitu chochote kile unachotaka.
 • Mazoezi yanaweza kumfanya kilaza kuwa gwiji, yanaweza kumfanya mchezaji wa kawaida kuwa mchezaji wa kimataifa, mwimbaji wa kawaida kuwa  mwimbaji mwenye jina kubwa,  na yanaweza kufanya maajabu kwako pia. Na hapa huhitaji konekisheni, wala kipaji bali unahitaji mazoezi.
 • Kujifunza peke yake bila mazoezi hakuna maana Ebu fikiria ukae ujifunze kuhusu mbinu zoote za kushona suti, bila kuzifanyia kazi. Au ujifunze kuhusu kucheza kucheza kinanda bila ya kufanyia mazoezi haya maarifa uliyojifunza. Ni wazi kuwa kwa vyovyote vile huwezi kubobea, hivyo raha ya maarifa na kila kitu unachojifunza ni kukifanyia mazoezi.
 • Unapofanya mazoezi ni sawa na mtu ambaye anakuwa anafanya uwekezaji. Muunganiko wa mazoezi yale unayokuwa unafanya mara kwa mara baada ya muda unaleta matokeo makubwa.

Katika andiko linalofuata tutaona dhana ya saa elfu kumi kwa undani zaidi na jinsi ambavyo unaweza kuitumia hii dhana kwa manufaa makubwa kwako.


One response to “NGUVU YA KUFANYA MAZOEZI”

 1. Imekaa vizuri sana hongera sana mwalimu wangu umeandika vizuri mno kuhusu mazoezi nimepata kitu kikubwa sana kupitia uandishi wako na mafunzo ambayo yamenisisimua mwili wangu Asante Mwalimu…. Mungu akubariki sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X