Ufanyeje unapopata fedha nyingi kwa wakati mmoja huku ukiwa hujui wapi unaweza kuiweka


Huwa inatokea mtu anapata fedha nyingi kwa wakati mmoja wakati akiwa hajui Cha kufanya. Sasa siku ya leo nataka tuone wapi unaweza kuweka fedha yako pale inapotokea umepata fedha nyingi kwa wakati mmoja.

Haijalishi fedha hiyo umeipata kutokana na kubeti 😂
Au labda wewe Ni mkulima umeuza mazao yako ila sasa unasubiri msimu.
Au pengine hata inaweza kuwa ni pensheni.
Au fedha ambayo umekuwa unaifanyia kazi kwa muda mrefu na sasa umepewa kwa siku moja.

Kuna vitu baadhi ambavyo unapaswa kuangalia kabla ya kuwekeza fedha zako.

Kwanza ni usalama wa fedha zako.
Pili Ni uharaka wa wewe kuipata ukiihitaji Tena
Tatu utaangalia usimamizi wa fedha zako ambazo ukiwekeza utakuwa chini ya Nani na uzoefu wake kwenye kusimamia fedha za watu wengine. Huwezi kumpa fedha ambaye hana uzoefu ili ajifunzie kwenye fedha zako.

Kitu kingine cha kufahamu ni kuwa Kuna maeneo mengi ya kuwekeza kama kwenye hisa, hatifungani, vipande, kilimo, madini, fedha za kidigitali (forex na crypto currency) na mengine mengi Sana.

Vigezo vichache nilivyokwambia hapo juu vinatumika kwenye maeneo hayo yote.

Makala hii haitoshi kujadili maeneo hayo yote kwa kina. Ninachotaka kukwambia leo ni eneo unapoweza kuwekeza fedha zako ikitokea umepata fedha nyingi kwa wakati mmoja. Basi.

Na mimi nasema hivi, ikitokea umepata fedha nyingi kwa wakati mmoja basi IWEKEZE KWENYE MFUKO WA UKWASI WA UTT AMIS

Mfuko huu wa ukwasi (liquid fund) ulianzishwa 2013 ukiwa na malengo makuu matatu ambayo ni:
(i)   Kulinda mtaji wako;
(ii) Kutoa ukwasi (liquidity); na
(iii) Kutoa mrejesho shindani kulinganisha na maeneo mengine ambayo unaweza kuweka hela  kwa muda mfupi.

Mfuko huu unampa muwekezaji uwezo wa kuweka hela zake kwa muda mfupi au mrefu. Mfano, kama muwekezaji amepata fedha ya ghafla au ambayo bado hana malengo nayo kwa wakati huo.

Mwekezaji anaweza kuiweka kwenye mfuko huu wakati anafikiri nini cha kufanya na fedha yake ikawa inapata faida ya ongezeko la kiasi cha pesa yake wakati hakatwi makato ya aina yoyote.

Hakuna uwezekano wa fedha hiyo kupungua kutokana na makato Fulani Fulani lakini mfuko wa ukwasi unaweza kukupa msaada sana hapa kwani utatuza fedha zako pasipo kupungua kwa fedha yako wakati wa kuichukua.

Mathalani, unaweza kuwa mkulima wa msimu (unategemea mvua) baada ya kuvuna na kuuza mazao pesa yako ya mtaji ambayo utatumia kwa ajili ya kilimo mwaka ujao unaweza kuiweka katika mfuko huu wakati unasubiri msimu hapa utapata faida ya ongezeko la mtaji bila kupoteza chochote.

Kumbe ukiweka fedha yako huku,
Hakuna makato utakayopata kwa kuweka fedha yako.
Hakuna makato ya kukutunzia fedha yako. Kikubwa zaidi utapata ongezeko la faida.
Na hakuna makato wakati wa kutoa fedha.

Halafu fedha yako ukitaka kuitoa unaipata kwa wakati. Ndani ya siku tatu tu fedha yako inakuwa tayari. Hii Ni tofauti na uwekezaji maeneo mengine kama kwenye hisa ambapo ukinunua hisa na baadaye ukija kuuza Kuna kiasi Cha fedha kinakatwa.

Au kwenye kilimo ambapo unaweza kuwekeza na fedha yako isirejee kwako Kama ilivyokuwa unatarajia kulingana na hali ya hewa.

Kitu kimoja Cha ziada. Ukitaka kufuatilia kujua taarifa kuhusu uwekezaji kwenye mfuko wa UKWASI, taarifa zake Ni rahisi kupatikana na hauchukui muda mrefu. Ila ukisema ufuatilie crypto currency mzee baba…utatuatilia mwaka mzima na bado hutaelewa.

Kwa leo wacha niishie tu hapo.  Hii makala Ni maalumu tu kwako wewe ambaye umepata fedha nyingi, Mara moja na unawaza wapi unaweza kuiwekeza. Ila Kama unataka kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji kwenye hisa HATIFUNGANI NA VIPANDE basi nashauri usome kitabu changu cha MAAJABU YA KUWEKEZA KWENYE HISA, HATIFUNGANI NA VIPANDE. Hutajutia kukisoma

Kila kheri

Godius Rweyongeza


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X