Limekuwa ni kama jambo la kawaida kusikia watu waliokuwa na vipaji na watu ambao wakati fulani walikuwa wakiingiza fedha nzuri kupitia vipaji vyao wakiwa hawana fedha. Vyombo vya habari, vimekuwa vikiripoti kuwa hawa watu hawana fedha na muda mwingine kupitisha mchango ili hawa watu waweze kupata mahitaji yao ya muhimu au hata kupata sehemu ya kukaa. Wengine huwa wanafukuzwa nyumba walipopanga na hivyo kuwaletea fedheha na kujenga picha mbaya kwa watu wenye vipaji. Kitu hiki kinafanya vyombo vya habari ndio visaidie kupitisha mchango ili watu hao waweze kuchangiwa.
Japo vyombo vya habari vimekuwa vikifanya hivi kwa mazoea, na vimekuwa vikifanya vizuri, ila hili siyo jambo ambalo tunapaswa kulifumbia macho na kuacha kulifundisha ili yeyote atayesikia la mkuu, asije akavunjika guu, halafu eti mkuu mwenyewe ni mimi, hahaha. Kama mtu ana kipaji chake na kipaji chake kinamwingizia fedha nzuri sasa hivi, basi hata miaka mingine mbeleni baada ya kustaafu, hapaswi kuendelea kulalamika wala kupungukiwa na kitu, ndio maana hii sura nimeiandaa maalumu kwa ajili ya hili jambo.
Kuna tatizo kubwa
Kuna sehemu kuna tatizo kubwa na hili tatizo tunapaswa kuhakikisha tunalifanyia kazi ili kuliondoa. Maana, ukiachana na watu wenye vipaji na ujuzi wao, hata wafanyakazi na watu ambao wamekuwa wanaingiza kipato kizuri kwa miaka yao yote ambayo wamekuwa wakifanya kazi, mara tu baada ya kustaafu unakuta kwamba wanakuwa na ukata mkubwa sana wa fedha. Sasa kumbe hili jambo tunapaswa kulipigia kelele, ili watu waweze kujua namna sahihi ya kuishi na hela zao, kuzitumia kwa manufaa, kuziwekeza ili hata baadaye watakapostaafu, waweze kustaafu kwa raha mustarehe, wakiwa na uhakika wa mzigo mkubwa wa hela nyuma yao.
Watoto wanaorithi mali
Wengi wamekuwa wakifananisha watu wenye vipaji (wakimbiaji wa mbio za marathoni, wanamziki, wanamichezo na wengineo) na watoto ambao wanarithi mali…
Yaani, kwamba wote hawa wana vitu viwili ambavyo vinafanana, kwanza ni kupata mali nyingi kwa wakati mmoja na pili ni kuzitapanya au kuzitumia hizo mali zote na baadaye kubaki bila ya fedha
Tafiti nyingi zimerudiwa mara kwa mara na kuonesha kuwa watoto ambao huwa wanarithi mali, asilimia kubwa sana ya watoto hawa wanaishia kupoteza hizo mali ndani ya muda kidogo na baadaye kuishia kwenye umasikini mkubwa sana. Kitu hiki pia kimekuwa kikitokea kwa watu wenye vipaji vyao. Mtu anakuwa ana kipaji anafanya vizuri, anapata fedha, na halafu hizo fedha anazitapanya na mwisho wa siku anabaki bila ya fedha yoyote ile. Hiki kitu baadaye kinamfanya aishiwe na hata kufikia hatua ya kuombaomba kwa watu na kwenye vyombo vya habari. Swali linabaki je, mzunguko kwa watu wote vipaji unapaswa kuwa hivi?
Yaani, ina maana kwamba kila mtu mwenye kipaji anapaswa kufikia hatua ambapo ataishiwa fedha na kuanza kuomba msaada li kujikimu na maisha yake?
Usiilalamikie serikali
Kuna wamekuwa wakiilalamikia serikali kuwa haiwajali baada ya kuwa wamestaafu kufanya kazi. sasa kabla hatujafika huko kote, ebu ngoja tuweke msingi wakati ukiwa unapokea fedha. Ili uweze kuitumia vizuri hii miaka yako ambayo uko kazini kwa ajili ya kuhakikisha kuwa hii miaka inakuwa yenye manufaa makubwa kwako, kiasi kwamba utakapostaafu au likitokea jambo lolote la kukufanya usiendelee na kazi basi uwe na chanzo cha uhakika cha kukuingizia fedha.
Na kitu kingine na muhimu cha kufahamu ni kuwa maisha ni wajibu wako, hivyo kama maisha ni wajibu wako, unapaswakuubeba huu wajibu wa maisha yako kwa asilimia 100.
Usisishindane kufanya starehe unapopata fedha
Wengi wanapokuwa na nguvu na wanapopata fedha basi kitu cha kwanza wanachofanya ni kuonesha kwamba wanazo hizo fedha. Utasikia watu wanasema kwamba tumia fedha zikuzoee. Au ponda mali kufa kwaja. Utasikia mwingine anasema kwamba hapa duniani tunaishi mara moja. ni kweli tunaishi mara moja hapa duniani, na unapaswa kufurahia maisha yako na uwepo wako hapa duniani, ila sasa usitumie fedha kiasi cha kupitiliza wakati hujajenga misingi ya kukuingizia fedha hata kama umelala.
Kama umewahi kufuatilia watu wenye fedha siyo watu ambao huwa wanatumia fedha zao hovyohovyo, badala yake ni watu ambao huwa wanaitumia fedha zao kwa manufaa kabisa.
Wanawekeza na wanajenga vyanzo vya kipato katika kuhakikisha kwamba wanakuwa na fedha zaidi. Na wewe fuata nyayo zao. Na hapa chini ninaenda kukuonesha ni kwa namna gani unaweza kufuata nyayo za hawa watu ili uweze kufanya makubwa.
Anza kufuata misingi ya fedha
Kila kitu kwenye maisha kina sheria na misingi yake. Daktari anayefanya matibabu kuna misingi na sheria ambazo anapaswa kuzifuata kwenye matibabu, hivyo hivyo kwa mwanasheria, kuna misingi na kanuni ambayo anaifuata kwenye kazi yake.
Kitu hiki mara nyingine huwa kinaitwa miiko ya kazi. hizi ndizo kwa kiingereza zinaitwa dos and donts. Yaani, vitu vya kufanya na vitu ambavyo siyo vya kufanya.
Sasa kuna misingi ya kukuza kipaji chako ambayo, kiuhalisia nimeielezea kwenye kitabu cha KIPAJI NI DHAHBU, nashauri sana uweze kupata kitabu hiki cha kipekee ila kwa leo tutaongelea upande wa fedha, upande ambao umekuwa ukiwasumbua watu wengi. ili pale utakapokuwa umeanza kupata fedha kutokana na kipaji chako basi, usije ukayumba wala kutetereka sehemu.
Kwanza kifanye kipaji chako kama biashara
Unajua kwa nini nasisitiza hili la kukifanya kipaji chako kuwa kama biashara
Kwanza ni kwa sababu watu wengi wamekuwa wakifanyia kazi vipaji vyao kama hobby. Hobby ni kitu unafanya tu ilimradi umefanya kwa ajili ya kujifurahisha.
Siku moja nilikuwa naongea na rafiki yangu mmoja kuhusiana na huduma nyingi ambazo tulikuwa tunapata kwa rafiki zetu wakati tuko chuoni, mtaani huduma hizohizo zinalipiwa gharama kubwa ila pale chuoni tulikuwa tunazipata bure kabisa. Kumbe hata hawa ndugu zetu wangeweza kuweka vipaji vyao katika mfumo wa kibiashara na hivyo kuweza kupokea fedha na hata kujenga biashara zaidi ambayo ingewafikia wengi.
Kwa kusema hili sIyo kwamba nakataza watu kutoa msaada au kusaidia. Ila msaada usipitilize kiasi cha mtu kujisahau.
Mfano wa huduma mojawapo ambayo tulikuwa tunapatabure pale chuoni ni huduma ya kutengenezewa simu na marafiki wa karibu pale inapoharibika. Unakuta mtu ana ujuzi wa kutosha kwenye hili kiasi kwamba simu yako ikiharibika anaitengeneza na kuirudisha kwenye uimara wake, anaitengeneza vizuri bure. Kitu ambacho ni kizuri. lakini walau angeweza kuchaji kiasi kidogo kwa ajili ya kuifanya hiyo huduma yake iweze kusongambele zaidi. Huduma hizihizi huku mtaani, tunazilipia, kwa mwanachuo pia unaweza kuweka kiasi kidogo tu cha watu kukulipa na hivyo kupata fedha za hapa na pale za kuendesha maisha chuoni na kujenga ukiwa chuoni au baada ya chuo.
Kitu kingine cha kuongezea hapa ni kuwa, mtu akikosa huduma ya kwako ya bure ataenda mtaani kwa mtu ambaye anatoza hela na ataitoa hela. Mfano simu yake ikiharibika na wewe kipindi hicho ukawa umesafiri, au unaumwa na huwezi kuitengeneza, kwa sababu anaihitaji kwa haraka ataenda kwa mwingine na atamlipa hela ili simu yake itengenezwe kwa haraka, sasa kwa nini na wewe usiwachaji watu kiasi kidogo ili wakulipe kwa hiyo huduma unayotoa. Fikiri kibiashara.
Lakini pia nasisitiza kwamba ufikiri kibiashara zaidi kwa sababu, ukishaweka mfumo kwenye biashara yako, ni wazi kuwa kipaji chako kitendelezwa baada hata ya wewe kuwa umezeeka au hata baada ya kufa. Kuna watu wengi wana vipaji vizuri vya kupika, ila wachache wameweza kufanya vipaji vyao kuwa biashara. Ebu chukulia mfano rahisi tu wa kupika maandazi. Kuna watu wengi wanapika mandazi, ila ni wangapi wameweza kusambaza mandazi yao kama Bakhresa? Sidhani hata kama Bakhresa ana kipaji cha kupika mandazi, hahaha. Ila tofauti kubwa kati ya Bakhresa na watu wengine wanaopika maandazi ni kuwa Bahkhersa yeye anafikiri kibiashara zaidi.
Hivyo, yeye ameweka mfumo wa kibiashara kwenye mandazi yake. Mfumo huu upo kuanzia kwenye kupika mandazi, kuyapaki, kuyasambaza mpaka kuyauza sokoni. Hiki kitu kinafanya maandazi yake yaweze kuuzika siyo kwenye eneo alipo yeye, bali yanauzika karibia nchi nzima. Wakati hapo mtaani kwenu kuna mama ambaye anapika maandazi na hayo maandazi hata hayajasambaa mtaa mzima mnapoishi.
Sijui unanielewa hapo. kumbe na wewe anza kufikiri kibiashara, anza kufikiri Bakhresa, Bakhresa ili na wewe kipaji chako uweze kukiwekea mifumo ya kibishara na kukifanya kweze kwenda mbali zaidi hata kama hautakuwepo.
Mfumo wa biashara utafanya kipaji chako kiweze kusogea. Unaanzaje sasa kuweka mfumo wa biashara kwenye kipaji chako,
Hivi hapa ndivyo unaweza kuanza
Kwanza anza wewe kufanyia kazi kipaji chako. Hiki sihitaji kukieleza zaidi, maana tayari nimeshakieleza kwa kin kwenye kitabu cha KIPAJI NI DHAHABU. Nakala ya kitabu hiki ni elfu tano tu. kupata nakala hii, tuma fedha kwa 0755848391 jina ni GODIUS RWEYONGEZA.
Pili, angalia majukumu yote ambayo unafanya kwenye biasahra yako. Kisha yagawe hayo majukumu, angalia yale majukumu ambayo ni ya muhimu sana na yanahitaji uwepo wako, wewe yafanye hayo. Majukumu mengine wape watu wakusaidie kuyafanya.
Tafuta watu kukusaidia kwenye hayo majukum ili nao waweze kufanya hayo majukumu huku wewe ukiweka nguvu kubwa zaidi kwenye yale majukuu ya muhimu sana kwako.
Nne, weka mfumo wa namna vitu vinavyofanyika. Kwa mfano kwamba wakati wa kutengenza mandazi, haya ndiyo mambo ambayo kila mtu anapaswa kuzigantia. Hii itakusaidia kiasi kwamba hata kama hautakuwepo, majukumu yako yataweza kuendelea mbele zaidi bila ya kurudi nyuma. Lakini pia hii itasaidia kwamba hata kama yule uliyemwajiri akitoka, bado utakuwa na uhakika kuwa shughuli zako zinaendelea bila ya kurudi nyuma tena kwa ubora ule ule.
Umeshawahi kuona watu wanakataa kununua chakula kwa sababu mhudumu fulani hayupo siku hiyo. Changamoto inakuwa pale ambapo mhusika mmojawapo kwenye biashara anaondoka, ubora unapungua, au kama ni huduma kwa wateja ndio siku hiyo inakuwa sifuri.
Sasa mfumo ni mwongozo. Unapaswa kufuatwa bila kujali wewe upo au haupo. Unapaswa kufuatwa bila kujali mtu fulani uliyemwajiri yupo au hayupo. Rafiki yangu lifanyie kazi hili kwenye kipaji chako pia.
Nne, simamia mfumo. Hapa hakikisha kwamba kila kitu kwenye mfumo kinaenda sawa kama inavyostahili.
Tano weka mtu wa kusimamia mfumo, hapa unaweka mtu wa kusimamia mfumo, huyu anasimamia kiasi kwamba hata kama haupo kila kitu kinaendelea. Ukiwa na mfumo mzuri hata ukifa, kila kitu kinaendelea. Ndio maana leo hii unaona kampuni kama cocacola zinazidi kusongambele. Unajua Cocacola ilianzishwa mwaka gani? Utakuwa sahihi, ni mwaka 1892. Ni zaidi y a miaka 100. Mwanzilishi wake alishakufa miaka mingi sana iliyopita, ila kitu kimoja kilicho nyuma yah ii kampuni na kinachoifanya iendelee kusonga mbele ni mfumo unaosimamia uzalishaji wa bidhaa zake. Hakuna hata siku moja utakunywa cocacola ukuta kuwa ile ladha imebadilishwa, ladha ni ileile kila siku. Ladha ni ileile ukiwa Tanzania, Uganda, Afrika kusini au kazikazini! Kwa nini? kwa sababu ya mfumo ulio nyuma ya utengenezaji wa soda hii. kuna vitu ambavyo unapaswa kuzingatia. Na ukizingatia hivyo tu, basi umemaliza. Na wewe unapaswa kufanya hivyo, tengeneza mfumo kwa ila kitu.
Tengeneza mfumo kwenye uzalishaji, watu wajue mchakato wote wanaofuata kwenye kutengeneza bidhaa au kutoa kitu. Mama anayepika maandazi mtaani kwako, anapika mandazi matamu sana, ila siku asipokuwepo kutengeneza mandazi yale, akaja mwanae ujue siku hiyo yanatengenezwa maandazi ya hovyo. Kwa nini? kwa sababu mama anajua mchakato wote wa kutengeneza mandazi, ia sasa ule mfumo haufahamiki kwa mtoto. Hakuna sehemu umeandikwa. Kwa hiyo uandike huo mfumo wako, ili kila anayefanya kazi kwenye kitengo husika akae akiujua huo mchakato wa kufuata.
Sita wakabe hao watu uliowaweka kusimamia mfumo
Saba ongeza juhudi zaidi kwenye kusimamia mfumo na kwend ambali zaidi.
Sambamba na kuweka mfumo sahihi wa kibishara kwenye kipaji chako unachofanya unahitaji pia kuweka mfumo sahihi wa kifedha kwenye kipaji chako. Na kwa kuanzia, anza na vitu rahisi tu. anza na kuhakikisha unajua mapato na matumizi. Yaani, fedha yote inayoingia ijulikane na fedha yote inayotoka ijulikane. Hiki kitu ni kidogo sana ile chenye nguvu kubwa sana.
Halafu hao watu hao ambao unawaita ili kukusaidia kazi za hapa na pale hakikisha kwamba unawaliipa. Niwazi kuwa na wao wana ndoto na malengo ambayo wanegependa kutimiza, hivyo kwa kile kiasi utakachowalipa, watakuwa na uwezo wa kuanza kufanyia kazi malengo na ndoto zao huku wakiendelea kukusaidia wewe. hivyo, walipe. Kazi yako kubwa itakuwa ni kuhakikisha kuwa unaajiri pale ambapo mtu atakuwa anahitajika kwenye biashara ili aweze kusaidia majukumu fulani, kitu ambacho kitakusaidia wewe na timu yako kuweka nguvu kwenye kukuza mauzo zaidi na hivyo kuweza kuwalipa.
Kwa hiyo utatoa kiasi utawalipa. Na wewe mwenyewe utajilipa mshahara wa kawaida.
Kisha faida itakayobaki iwekeze.
Na kwa kuwa nataka nikupe mwongozo kamili, sikiliza nenda kawekeze fedha yako kwenye mifuko ya uwekezaji ya pamoja, iliyo chini ya UTT.
Najua watu wengi watakushawishi kuhusu kuwekeza kwenye maeneo mengi mengi kama kilimo, bitcoin, na mengine mengi. Lakini kwa kuwa wewe nguvu yako kubwa unaiweka kwenye kipaji chako, huhitaji kuwekeza nguvu kubwa kwenye maeneo mengine, nguvu yako yote iwekeze kwenye kipaji chako na hata unapoongea na timu yako, wasukume wafanye vizuri zaidi ili kipaji chako kama bishara kiweze kufika mbali, ila kwa vyovyote vile hakikisha kuwa hautawanyi nguvu zako kwa kuziweka kwenyea maneo mengine ambayo huyafahamu, badala yake wekeza nguvu zako zote kwenye kipaji mpaka kifikie ngazi kubwa za kimataifa.
Kwa hiyo, uwekezaji wako wote ufanyie kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya UTTt
Najua utakuwa unajiuliza UTT ni kitu gani na hii mifuko ya pamoja inafanyaje kazi, hiki kitu sitaweza kukieleza kwa kina kwenye makala hii. Ila nimeandika kitabu kinaitwa maajabu ya kuwekeza kwenye hisa, hatifungani na vipande. Nashauri sana uweze kupata kitabu hiki cha kipekee, kwa kuwasiliana nami kwa 0755848391
Ngoja nikwambie kitu, unapowekeza kwenye hii mifuko unakuwa unaifanya fedha ikufanyie kazi hata kama wewe haupo, kitu ambacho kinakutengenezea maisha mazuri ya hapo baadaye. Lakini pia ni sehemu ya wewe kuweka akiba na kuteng eneza kesho yako bora.
Asante sana,
Nakutakia kila la kheri
Godius Rweyongeza (SONGAMBELE)
0755848391
Morogoro-Tz
SUBSCRIBE KWENYE CHANNEL YANGU YA YOUTUBE HAPA CHINI