Moja kati ya kitu ambacho nimekuwa nikiwaambia watu wengi ni kuwa tuna bahati ya kuishi kwenye ulimwengu wa leo tunaoishi. Mababu zetu wangekuwa wanarudi leo hii na kuona fursa kibao zilizotuzunguka, ni wazi kuwa wenyewe wangetuonea gere.
Mambo ambayo miaka hiyo yalikuwa hayawezekani, leo hii yanawezekana, tena siyo kwamba yanawezekana kidogo, yanawezekana sana tu.
Ebu chukulia kwa mfano jinsi ilivyokuwa kazi ngumu kunoa kipaji chako miaka ya nyuma. Tusiende mbali sana, tuongelee miaka michache hii baada ya uhuru. Kiukweli, kunoa na kuendeleza kipaji chako ilikuwa ni moja ya kazi ngumu kitu hiki kilifanya watu wengi washindwe kunoa na kuendeleza vipaji vyao. Na hata wengine kwa kukosa maarifa sahihi kama ambayo nimeandika kwenye kitabu cha KIPAJI NI DHAHABU, walishindwa kabisa kujua vipaji vyao.
Ebu tuchukulie mfano kuwa ulikuwa na kipaji cha kuimba, miaka hiyo na labda ulikuwa mkoa wa Mtwara. Kwanza ili kurekodi wimbo ulipaswa kwenda studio na kuwasilisha wazo lako, ambapo studio wazo lako lingeweza kukubaliwa au kukataliwa, lakini pia ulipaswa kuwa na hela kubwa ya kukusaidia kurekodi wimbo wako.
Baada ya kuwa umerekodi huo wimbo ulipaswa kuwa na mtu wa kusambaza hizo nyimbo zako na hata wafadhili wa kukupiga tafu kwenye kazi zako.
Siyo hilo tu, kama miaka hiyo ulitaka kutangaza wimbo wako, njia za kipekee na za uhakika za kutangaza wimbo huo, zilikuwa ni kupitia vyombo vya habari. Kwa kuwa vyombo vingi vya habari vilikuwa Dar, wewe uliyekuwa Mtwara, ulilazimika kusafiri mpaka Dar ili ukutane na watu hawa wa vyombo vya habari au la kutangaza kipaji chako kwenye hivi vyombo vya habari ilikuwa ni ngumu sana.
Na hata baada ya kukutana nao kutokana na mfumo uliokuwepo wangeweza kukukubali au kukukatalia au hata kutaka uwape rushwa kubwa ili wakufanyie tangazo.
Sasa chukulia hiyo hali na jinsi mambo yalivyo sasa hivi, kwa sasa hivi mambo yamebadilika kwa asilimia 100. Huo mchakato wote umevunjwa kiasi kwamba unaweza kufanya hayo yote bila kizuizi kikubwa.
Kama una wimbo au kipaji cha kuimba na ukatunga wimbo wako. Unaweza kwenda studio na kurekodi wimbo wako
- kwa gharama nafuu sana na
- bila vikwazo
Pengine unaweza ukawa hauna hela ya kurekodi, ukaamua tu kuanza kutumia simu yako kurekodi wimbo wako na hata baadaye ukautoa.
Kama nakuona vile unavyoguna kuwa haiwezekani kurekodi wimbo kwa kutumia simu!
Ila kabla hujakataa kabisa hilo wazo kuna vitu viwili ambavyo ningependa kukwambia.
Kama unatumia simu janja (smartphone), simu yako ina uwezo mkubwa kuliko kompyuta iliyopeleka mtu mwezini. Huo ni ukweli nambari moja. Sasa ebu fikiria kompyuta iliyopeleka mtu mwezini ilikuwa na uwezo mdogo kuliko simu yako janja, je,unadhani kompyuta zilizokuwa zinatumika kurekodi nyimbo miaka hiyo zilikuwa zinafananaje? Ni wazi kuwa uwezo wake ulikuwa ni mdogo zaidi. Kumbe simu yako hiyo ni mgodi mkubwa sana ambao umeulalia, jitahidi sana ili uweze kuutumia mgodi huu.
Niendelee au nisiendelee!
Ukweli nambari mbili ambao utakufungua macho zaidi ni juu ya vijana wa Nigeria waliorekodi movie kwa kutumia simu. Vijana hawa kutoka Nigeria Kaskazini, walikuwa na simu moja hivi ambayo imekwaruzwakwaruzwa kwenye kioo. Ila waliitumia hiyo hiyo kama kamera kuhakikisha kwamba wanarekodi tamthiliya.
Kumbe kama una simu kubwa, maarufu kama simu janja au smartphone basi jua wazi kuwa umelalia hazina kubwa sana ambayo haupaswi kuichezea rafiki yangu. Ni hazina ambayo mababu zetu hawakuwa nayo, ila wewe una bahati ya kuwa nayo. Usiitumie ktu kuchati, bali itumie kwa manufaa.
Kuna watu wamerekodi video na kuziweka kwenye mitandao kama youtube na tiktoka na hatimaye kunufaika na kupata fedha. Kuna watu wametengeneza kazi mbalimbali za sanaa kwa kutumia simu zao. Mimi nimeitumia simu yangu kuandika vitabu na kuendesha mitandao ya blogu yangu ya songambele (www.songambele.co.tz). Rafiki yangu badala ya kusubiri siku ambayo utakuwa na rasilimali kubwa na za kipekee hakikisha kwamba unaanza kuzitumia hizi rasilimali za kawaida ulizonazo. Ukiweza kuzitumia vizuri hizi rasilimali kidogo ulizonazo, ukipata rasilimali kubwa ni uhakika kuwa utaweza kufanya makubwa zaidi ya hapo.
Bado unafikiri haiwezekani kurekodi muziki wako kwa kutumia simu? Kama unafikiri kitu hiki hakiwezekani basi fikiri tena!
Kwenye mtadao wa Tiktok kuna kijana mmoja maarufu sana ambaye ana wafuasi wengi kuliko watu wote kwenye mtandao huo. Kijana huyu si mwingine bali ni kijana Kaby Lame. Huyu kijana ni raia wa Senegali anayeishi Italia. Mpaka mwaka 2020 alikuwa ni mmoja wa wafanyakazi kwenye kiwanda kimojawapo pale nchini ITALIA, wakati wa kipindi cha Corona kampuni aliyokuwa nafanyia kazi ilipunguza wafanyakazi. Akiwa haelewi ni kitu gani ambacho angeweza kufanya katika kipindi kama hiki, aliamua kuchukua simu yake na kuanza kurekodi video fupifupi alizokuwa akifanya kama uchambuzi fulani hivi wa tamthiliya.
Alianza kidogo kidogo, na mara punde hizi video zake zilianza kushika kasi. Leo hii ni mmoja wa vijana wenye ushawishi mkubwa sana kwenye mtandao wa TIKTOK, lakini kitu kikubwa ambacho alianza nacho ni simu yake aliyokuwa nayo.
Leo hii najua vijana ambao wana ndoto na vipaji vikubwa, ila wanasubiri kupata mfadhili kutoka maeneo ambayo wenyewe hawajui kama atatokea.
Miaka kadhaa nyuma kabla hata sijajua kama kuna watu waliweza kurekodi movie kwa kutumia simu na kabla sijajua kuwa kuna akina Khaby Lame ambao wanarekodi video fupifupi kwa kutumia simu, nilikuwa nikiongea na mmoja wa ndugu zangu wa karibu ambaye moyoni mwake alikuwa akipenda kuigiza.
Nilimweleza namna ambavyo angeweza kuanza kufanyia kazi kipaji chake cha kuigiza huku akijirekodi kwa kutumia simu yake. Nilipomwambia wazo huyu ndugu alilikataa kabisa, huku akisema kwamba haiwezekani kufanya kitu kama hico. Leo hii kile alichokuwa anasema kwamba hakiwezekani kuna watu wameweza kukifanya kwa manufaa na kujulikana duniani.
Pengine yeye leo hii asingekuwa maarufu kama hawa, lakini angekuwa anafanya kitu anachopenda. Lakini mpaka ninavyoandika hapa, bado amesubiri muujiza fulani wa kumnyanyua na kumfanya aigize. Anasubiri awe na kamera za kisasa na timu ya kumrekodi.
Hiki kitu kinanikumbusha usemi wa kuwa, pale unaposema kwamba haiwezekani, anatokea mtu mbele yako ambaye anakifanya. Wewe ukiendelea kusema kwamba haiwezekani, basi jua kwamba muda si mrefu kuna watu mbele yako ambao watatokea na kufanya kile kitu ambacho wewe mwenyewe ulikuwa unasema kwamba hakiwezekani.
Baada ya kuwa umeanza kufanyia kazi kipaji chako, hakikisha kwamba hauishii tu kwenye kuanza kukifanyia kazi. lakini kuwa na mwendelezo wa kile unachofanya. Hiki ni kitu ambacho huwa kinawaangusha watu wengi. kuna watu kadha wa kadha ambao huwa wanaanza kufanyia kazi vitu ila huwa wanaishia njiani. Rafiki yangu, usifanyie kazi kipaji chako mara moja kisha ukatulia. Kuwa na mwendelezo kwenye kufanyia kazi kipaji chako. Usifanyie kazi kipaji chako mara moja, kifanyie kazi mara kwa mara.
Hii ni njia bora ya kujitangaza bila kutumia gharama kubwa. kuna watu wanaweza kupuuza kazi zako kadhaa za kwanza, ila wakiona unaendelea kuweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya inafikia hatua wanaanza kufuatilia kazi zako, na hivyo unakuwa umewateka na kuwaleta kwako.
Kuna watu watafuatilia kazi zako na kuwaambia watu wengine juu yako. Kwa jinsi hii,kazi zako zinakuwa zinakutangaza zaidi kwenye maeneo mbalimbali
Wekeza kwenye kipaji chako. Pale unapokuwa unapata hela, usitumie zote kwa pamoja. Badala yake toa kiasi fulani ambacho utakirudisha kwenye kipaji chako. Utakirudisha kwenye kipaji kwa kununua vifaa vya kisasa zaidi ambavyo zitakusaidia kutoa kazi ambazo ni bora kadiri siku zinavyoenda. Utawekeza tena kwenye kipaji chako kwa kukitangza ili kiweze kwenda mbali kuliko ilivyokuwa mwanzoni. Na kujifunza vitu mbalimbali ili uzidi kubobea zaidi.
Na kwenye ulimwengu wa leo kuna njia lukuki za kutangza kipaji chako.
Unawezakutengaza kipaji chako kwenye mtandao wa intaneti . Google wana mfumo wao wa kutengeneza matangazo ambapo hayo matangazo unayaonesha mbele ya watu wanaoendana na tangazo lako. Lakini pia kuna mitandao kama youtube ambapo unaweza kutangaza kipaji chako huku.
Mtandao kama instagram pia ni mtandao mzuri kwa ajili ya kutangaza kipaji chako, ambapo kwa gharama kidogo tu unaweza kuwafikia melfu kwa maelfu ya watu. Hiki kitu kilikuwa hakiwezekani miaka ya nyuma. Ebu chukukulia miaka ya nyuma kama ungependa kujitangaza kwenye gazeti. Gharama tu kuchukua nusu ukurasa kwenye gazeti, ni kubwa sana. na hii siyo kwa miaka ya nyuma tu, bali mpaka leo hii. Bado ukitaka kutangaza kipaji chako kwa njia magazeti au redio na runinga, gharama yao ya kutangaza kazi yako au kipaji chako ni kubwa ukilinganisha na mitandao kama facebook, twitter na instagram. Ambapo kwa gharama kidogo tu unaweza kufanya matangazo ambayo yatawafikia watu wengi
Kwa leo naishia hapa.
Kesho nitaendeea
Mimi ni rafiki yako Godius Rweyongeza
0755848391
Morogoro-Tz