Sababu Sita Zisizopingwa Kwa Nini Unapaswa Kuendeleza Kiapaji Chako


KIPAJI NI DHAHABU
Ili kupata kitabu hiki, wasialiana na mi kwa 0755848391 sasa

Kwenye kitabu cha Acres of Diamond, mwandishi ameeleza historia ya jamaa ambaye aliambiwa kuwa ukiwa na almasi yenye ukubwa kidole unaweza kuimiliki dunia. Huyu jamaa kusikia hivyo, aliamua kusafiri kwenda kuitafuta dhahabu ambayo mwisho wa siku hakuipata!

Siku hizi bado watu wanatafuta dhahabu! Utasikia watu wanapeana stori kuwa ukienda kwenye machimbo ya Geita au Mererani basi wewe kutoka kimaisha ni njenje tu! lakini ukiachana na hayo ni ukweli kuwa  mbali na hayo madini na hizo dhahabu ambazo unaweza kupata kutoka kwenye hayo maeneo, kuna dhahabu  ambazo watu wanazo ila wanaonekana kutozitumia vizuri na dhahabu hizi siyo nyingine bali ni uwezo na vipaji tulivyonavyo. Ukifahamu thamani ya kipaji, utajihidi kuhakikisha kwamba unatumia kipaji chako kwa nguvu zako zote bila kuacha. KIPAJI NI DHAHABU. Na unapaswa kukinoa vizuri rafiki yangu.

Kwa leo nataka niingie kwa undani na kukueleza sababu sita kwa nini hasa unapaswa kunoa kipaji chako, ili kiweze kuwa chenye manufaa kwako wewe mwenyewe.

Sababu ya kwanza ni Umezaliwa Nacho Wewe Ila Siyo Chako

Huwa napenda kuwaambia watu kuwa unapewa kipaji sio kwa manufaa yako, bali kwa manufaa ya jamii nzima. Na kuthibitisha hili hapa huwa napenda kutolea mfano wa mwanamziki.

Mwanamziki akiimba wimbo wake sio tu kuwa unamnufaisha yeye peke yake, bali wimbo huo unakufaisha hata wewe ambaye unausikiliza. Tena unakuta kwamba wewe msikilizaji ndiye unasikiliza ule wimbo kuliko hata mwanamziki mwenyewe. Kwa hiyo, wewe unapokuwa na kipaji unapaswa kukifanyia kazi sio tu kwa ajili ya manufaa yako bali kwa manufaa ya watu wengine pia.

Kuna watu wengine ili waweze kufanikisha vipaji vyao wanahitaji wewe ufanyie kazi kipaji chako kwanza. Ebu chukulia mfano wa mtu kama Albert Einstein. Huyu ni mtu ambaye alikuwa na kipaji cha hesabu mpaka akaweza kuja mlinganyo maarufa sana kwenye fikizia wa E=Mc2. Lakini Einstein sio baba wa fikizia!

Inawezekana kama akina Newton na Galileo wasingeweka njia, basi kipaji cha Einstein kisingeonekana. Kwa hiyo hakikisha unatumia kipaji chako, kwa ajili ya manufaa yako, kwa ajili ya manufaa ya jamii, na kwa ajili pia ya kuhamasisha watu wengine.

Mwaka 2007 ulikuwa ni wa kipekee kwenye ulimwengu wa kidigitali. Ni mwaka ambao kwa mara ya kwanza simu janja (smartphones) zilivumbuliwa na kuletwa kwenye umma wa watu. hata hivyo, cha kushangaza ni kwamba, aliyegundua simu hizi, alishalala zamani ila simu hizi zimeendelea kuwa zenye faida na manufaa kwa watu wengine zaidi yake. Hiki kitu kikuoneshe na wewe kuwa kipaji au huo uwezo ulio nao ndani yako siyo tu kwamba ni wa kwako peke yako, bali upo pia kwa ajili ya manufaa ya watu wengine.

Leo hii watu wengi wananufaika kwa kutumia simu janje pengine kuliko hata aliyetengeneza simu hizo. Simu zinawaingizia watu fedha, simu zimetumika kuwaunganisha watu walio mbali, simu zimewezesha kuwatumia fedha ndugu zetu walio mbali…

Kuna watu wameweza kugundua vitu vingine kwa sababu tu walikuwa na simu au walikuwa wanajua kuna simujanja. Kwa mfano, hizi app za simu zimetengenezwa mara tu baada ya kuwepo kwa simu. Kuna watu maisha yao yanategemea app za simu tu.

Sasa ebu jiulize kama aliyetengeneza simujanja angeamua kufa na uwezo wake, leo hii hawa watu ambao maisha yao yanategemea app za simu peke yake wangekuwa wapi?

Kumbe muda mwingine kipaji chako kinaweza kuwa kimebeba ajira za watu wengine ila wewe hujui tu. Ebu kifanyie kazi siyo tu kwa ajili ya manufaa yako, bali kwa ajili ya manufaa ya watu wengine pia.

Sababu ya pili ni kuwa kuna watu wanaweza kubadlil maisha kwa sababu ya kipaji chako. Endapo utafanyia kazi kipaji chako na kukifanikisha kuna watu ambao watajifunza kwako na watataka kunoa vipaji vyao ili wawe kama wewe.

Hujawahi kusikia mtu anasema nikikua nataka niwe kama mtu fulani. Sasa kuendeleza kipaji chako kunawafanya  watu watamani sana  kuwa na maisha kama ya kwako.

Kuna watu wengine watanoa na kufanyia kazi vipaji vyao kwa sababu wanajifunza kwako.

Ngoja ni kwambie kitu rafiki yangu. ujue kitu kimoja kwenye maisha ni kuwa kwa vyovyote vile, popote pale ulipo kuna watu ambao wanajifunza kitu kutoka kwako. Inawezekana nyuma yako kuna watu wawili au mmoja ambao ni mashabiki wako, sasa hawa watu wakikuona wewe unafanyia kazi kipaji chako, ni wazi kuwa wenyewe watatamani sana kuweza kunoa kipaji chao na kukifanikisha,

Kuna watu wamekuwa wanamziki baada ya kuwa wamemwona mtu wa mtaani kwao kwenye runinga au kumsikia kwenye redio. Hiki kitu kimewapa hamasa kubwa na hivyo wao wakapambana ili na wao waweze siku moja kuonekana kwenye redio na runinga.

Na mimi nina uhakika leo hii ukifanyia kazi kipaji chako, kuna watu nyuma yako watapenda na watakuwa tayari kutaka kufuata nyayo zako. usiwaangushe, noa kipaji chako. Kiendeleze mpaka kiimarike.

Sababu ya tatu ni kuwa utaishi maisha ambayo unayapenda. Utafiti maarufu ni kuwa watu wengi huwa wanakufa jumatatu asubuhi. Kwenye utafiti huu wanaonesha kuwa wengi wa wale ambao huwa wanakufa siku ya jumatatu ni wale ambao huwa hawapendi kazi zao. Yaani, mtu anaenda kazini lakini kazi yenyewe anayoifanya siyo ile ambayo anapenda.

Hivyo akishakula bata siku za wikendi, halafu akaamka jumatatu akiwa anafahamu kuwa anaenda kufanya kazi ambayo hapendi, anakata tamaa na kupoteza maisha.

Rafiki yangu, kipaji chako ni kitu ambacho unakipenda. Unapofanyia kazi kipaji chako, maana yake unakuwa unafanyia kazi kile ambacho wewe mwenyewe unapenda. Sijui umenielewa mpaka hapo.

Hiki kitakufanya uishi miaka mingi na kheri duniani! Watu wanaofanya kile wanachopenda wana furaha, wana amani ya mwili na roho, wanajiamini kwenye kazi zao na hawana msongo

Ila kama unafanya kazi ambayo huipendi matokeo yake yanakuwa ni tofauti. Na utafiti mwingine unaonesha kwamba watu wanaotumia uwezo na vipaji vyao wanafanya vizuri zaidi kwenye kazi kuliko wale ambao hawatumii vipaji na uwezo wao.

Sababu ya nne ni kuwa utatengeneza fedha kutoka kwenye kipaji chako

Kadiri utakavyokuwa unakitumia kipaji kuna watu wataona kwamba wanaweza kunufaika na kipaji chako, na hivyo kuwa tayari kulipia ili wapate vitu vingi zaidi kutoka kwako

Sababu ya tano ni kuwa utaacha alama inayodumu milele. Kwa kazi ambazo utazifanya kutokana na kipaji chako, mwisho wa siku unaenda kuacha alama ambayo itadumu kwa siku nyingi hata baada ya wewe kuwa umeaga dunia.

Sababu ya sita kujiondolea majuto. Usipofanyia kazi kipaji chako, kuna siku utaanza kujuta kwa nini hukufanyia kazi kipaji chako. Kwanza, utasikia kwenye vyombo vya habari kwamba vijana machachari sehemu fulani, wameweza kufanya mambo makubwa. Wakati nawe, ulipaswa kuwa kijana machahari kama hao wanaotajwa. Hiki kitu  kitakuumiza na kukukatisha tamaa.

Pili, utaanzisha usemi utakaokuwa unautoa kama hadithi kwa watoto mpaka kwa wajukuu wako. Utaanza kuwaambia, bwana mnamwona fulani, nilisoma naye ila sasa hivi hashikiki. Kama si hivyo huenda ukasema kwamba, nilikuwa ninakaa naye darasa moja ila sasa hivi amefanikiwa sana. Utasema, kuna kipindi huyu mtu alikuwa na maisha mabaya ila sasa hivi maisha yake yamebadilika sana. Au pengine utasema, mimi ndiye nilikuwa kinara darasani na huyu jamaa hakuwahi hata kuonekana kwenye zile kumi bora. Binafsi, nimekuwa ninawavumilia sana wazee ambao wanasema hivi. Ila wewe, sitakuvumilia hata kidogo.

Nitakuuliza, wakati hawa wanapambana wewe ulikuwa wapi? Ni kitu gani kilikuzuia wewe kufanya makubwa? Je, hawa watu walikufunga kwenye mti wakaanza kuchapa kazi, sasa ndiyo wamekuja kukufungua? Kiukweli sitakuvumilia.

Rafiki yangu, hizo ni sababu zangu sita kwa nini wewe unapaswa kufanyia kazi kipaji chako tena, kuanzia leo hii. rafiki kama kuna zawadi unapaswa kujipa wewe mwenyewe kwenye maisha, basi ni zawadi ya kufanyia kazi kiapji chako. Halafu ujue kwamba nina zawadi ya kitabu ya kitabu. Kipokee kitabu chenyewe kwa kujaza taarifa zako hapa chini

kitabu cha maajabu ya kuweka akiba


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X