Je, kuuza vitu vya bei rahisi ni njia kutengeneza fedha nyingi kwa sababu bidhaa zinatoka kwa haraka?


Mara kwa mara nimekuwa naandika kwenye blogu yangu na kutolea mfano namna ambavyo Bakhresa na Mo Dewji wanauza bidhaa za bei ya chini. mfano watu hawa unakuta wanauza mpaka viberiti, chumvi, pipi na vinginevyo ambavyo vinauzwa shilingi 50, 100, 200 mpaka 500.

Nimekuwa nikitumia mfano huu kuhamasisha vijana mbalimbali kwamba wasidharau fedha kwenye maisha, badala yake kama mtu haoni sehemu yoyote ile ya kuanzia kwenye maisha kabisa, basi unaweza kuanza hata kwa kuuza kitu chochote kile cha bei ya chini kwa watu.

Lengo likiwa ni kwamba kijana aanze kujishughulisha na hata kuingiza kipato. Nimekuwa nasema hivi kwa sababu, kwa mtu anayeanza, ni rashisi sana kwenda kwa watu kuuza bidhaa ya bei rahisi kuliko kwenda kwa watu kuuza bidhaa ya bei kubwa.

 Mtu anaponunua bidhaa ya bei ya chini labda (elfu moja), hajiulizi mara mbilimbili kama anapaswa kutoa fedha yake mfukoni au anapaswa kuendelea na maisha mengine. Tofauti na mtu anayenunua bidhaa ya laki moja. huyu kidogo ataanza kujiuliza na utahitaji kutumia nguvu kumshawishi.

Sasa nadhani kutokana na msisitizo wangu huu wa kusisitiza vijana kuanza hata kuuza bidhaa za bei ya chini, umemfanya rafiki yangu kuuliza swali kama linavyoonekana hapa chini,

Anasema je, kuuza bidhaa za bei rahisi ni njia rahisi ya kuvutia wateja na unaweza kutengeneza pesa nyingi pia kwa sababu huenda bidhaa zinatoka kwa haraka??

Jibu ni hapana.

Kuna njia kadha wa kadha za kutengeneza fedha na kuufikia utajiri kwa hiyo sidhani kama hii ni njia RAHISI.

Unapokuwa unauza bidhaa za bei ndogo maana yake unavutia wateja wengi na matatizo yako yatakuwa mengi pia. Iko hivi, ukiuza bidhaa ya shilingi mia moja, utatakiwa kuuza kwa watu 100 ili ufikishe elfu kumi. Wakati huohuo mtu anayeuza bidhaa ye elfu tano, atatakiwa kuuza kwa watu wawili tu ili afikishe hiyo elfu kumi. Na kama unavyojua kushughulikana watu hakuwezi kukosa changamoto. Kwa hiyo, changamoto anazokuwa nazo mtu ambaye anauza bidhaa kwa watu mia moja ni tofauti kabisa na changamoto anazokuwa nazo mtu anayeuza bidhaa kwa watu wawili.

Kuuza bidhaa za baei rahisi ni njia ya kuanza nayo kwa ajli ya kukuweka kwenye mwendo, lakini siyo kwamba ndiyo mwanzo na mwisho. Hata Bakhresa mwenyewe siyo kwamba anauza pipi ya 100 kama pipi ya 100. Badala yake hizo pipi zake anaziuza kwa jumla kwa watu wanaoenda kuuza kwa rejareja huko mtaani. Hivyo, yeye hashughuliki moja kwa moja na wale wateja wengi wanaonunua pipi ya 100. Bali wateja wachache wananunua mzigo wa bei kubwa.

Kwa uzoefu wangu, wateja wanaoununua vitu vya bei rahisi huwa ni wasumbufu sana ukilinganisha na wateja wanaonunua vitu kwa bei kubwa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X